Kagere ana rekodi ya kipekee Simba Day
Muktasari:
- Kagere ambaye ni mchezaji aliyepata mwaliko leo sambamba na nyota wengine wa zamani wa timu hiyo wakiwemo Emmanuel Okwi na John Bocco, amepata nafasi ya kucheza mechi ya kirafiki iliyoshuhudia Simba ikishinda mabao 3-1 dhidi ya Equity.
WAKATI mashabiki wa Simba wakisherehekea miaka 90 leo katika kilele cha 'Simba Day', mojawapo wa nyota wa kukumbukwa kwenye kikosi hicho ni mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, raia wa Rwanda, Meddie Kagere.
Kagere ambaye ni mchezaji aliyepata mwaliko leo sambamba na nyota wengine wa zamani wa timu hiyo wakiwemo Emmanuel Okwi na John Bocco, amepata nafasi ya kucheza mechi ya kirafiki iliyoshuhudia Simba ikishinda mabao 3-1 dhidi ya Equity.
Kagere aliyejiunga na Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya msimu wa 2018-2019 ndiye anayeshikilia rekodi ya kipekee ya kufunga mabao matatu (hat-trick) katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 3-1 dhidi ya Power Dynamos ya Zambia 2019 kwenye kilele cha Simba Day.
Nyota huyo alifunga mabao hayo dakika za 3, 58 na 73 na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza katika tamasha hilo kufunga hat-trick, ikiwa ni rekodi inayoendelea kuishi hadi sasa hivi.
Katika Ligi Kuu Bara msimu kwanza 2018-2019, alifunga mabao 23 na kuibuka mfungaji bora, huku akiipiku rekodi ya aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe ya wachezaji wa kigeni kufunga mabao mengi msimu mmoja alipofunga 21 msimu wa 2015-2016.
Msimu wa pili wa 2019-2020 kwa staa huyo akiwa na Simba pia, alifunga mabao 22 na kutetea Tuzo ya Mfungaji Bora ikiwa pia ni rekodi kwani, haikuwahi kutokea kwa mchezaji yeyote iwe mzawa au wa kigeni kutwaa tuzo hiyo mara mbili mfululizo.
Rekodi hiyo ya Kagere ya kuibuka mfungaji bora mara mbili mfululizo inaendelea kuwatesa washambuliaji kwa sababu hadi sasa kwani licha ya mastaa wengi wazoefu kucheza kwa mafanikio makubwa ila hakuna aliyeifikia.