Baleke, Phiri waibukia Simba Day
Muktasari:
- Simba Day inafanyika kwa mara ya 18 tangu ilipoanzishwa mwaka 2009 chini ya uongozi wa aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali. Ukiachana na hilo, tamasha hilo linafanyika Uwanja wa Uhuru mara ya pili, ya kwanza ilikuwa wakati linazinduliwa mwaka 2009. Pia klabu hiyo inatimiza miaka 90 tangu ilipoanzishwa mwaka 1936.
KATIKA tamasha la Simba Day linalofanyika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, baadhi ya mastaa waliocheza Simba wamejitokeza huku wakielezea furaha yao ya kujiunga na Wanasimba wengine.
Simba Day inafanyika kwa mara ya 18 tangu ilipoanzishwa mwaka 2009 chini ya uongozi wa aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali. Ukiachana na hilo, tamasha hilo linafanyika Uwanja wa Uhuru mara ya pili, ya kwanza ilikuwa wakati linazinduliwa mwaka 2009. Pia klabu hiyo inatimiza miaka 90 tangu ilipoanzishwa mwaka 1936.
Mwanaspoti linakuletea walichozungumza mastaa mbalimbali kuhusiana na tamasha hilo.
JEAN BALEKE
Mshambuliaji raia wa DR Congo, Jean Baleke, amesema: "Nina furaha kuungana na Wanasimba katika tamasha la leo, natarajia kuona performance nzuri ya wachezaji wenzangu."
Baleke ambaye aliwahi kuichezea Simba msimu wa 2023-2024 na Yanga 2024-2025, ameongeza: "Nilipigiwa simu na viongozi wa Simba ndiyo maana nimesafiri kuja kujiunga nao, kwa sasa mimi ni mchezaji huru."
MEDDIE KAGERE
Mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo msimu wa 2018-2019 akifunga mabao 23 na 2019-2020 mabao 22, amesema: "Nimefurahi kupata nafasi ya kukutana na mashabiki wa Simba na wachezaji ambao nimewahi kucheza nao kama Emmanuel Okwi."
MOSES PHIRI
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Moses Phiri amefanya mazungumzo na Mwanaspoti akisema: "Sitaacha kuifuatilia Simba, ina historia kubwa na mimi, tamasha la Simba Day nakumbuka lilinikutanisha na mashabiki."
KAPOMBE ATAJWA
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescetius Magori, wakati anataja kikosi bora cha muda wote kwa upande wake kilichokuwa kimejaa majina ya wakongwe wengi, Shomari Kapombe alimpa heshima ya kipekee.
"Kapombe kaitumikia Simba kwa muda mrefu akicheza kwa kiwango cha juu, lazima nimpe heshima kubwa na anastahili," amesema Magori.
JOHN BOCCO
Nahodha wa zamani wa Simba, John Bocco amezungumzia tamasha hilo akisema: "Linawakutanisha Wanasimba pamoja na wachezaji kupata nafasi ya kuwaona mashabiki ambao wanajitoa kwa ajili yao."
BURUDANI ZINGINE
Mashabiki wa klabu hiyo licha ya kufurahia burudani zinaendelea ndani ya uwanja, nje kuna mtu aliyevaa mdori mkubwa ambao unawafanya baadhi yao kufurahia na wengine kupiga naye picha.