Yanga: CEO mpya ni mwanachama hai, ana kadi
Uongozi wa klabu ya Yanga umetolea ufafanuzi kigezo cha kuchaguliwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo kutokana na tangazo la maombi ya kazi kuainisha anatakiwa kuwa mwanachama hai wa Yanga.
Mchana wa leo Septemba 27, 2022 imemtambulisha Andre Mtine raia wa Zambia kuwa Mtendaji Mkuu huku baadhi ya watu mitandaoni wakihoji je ni mwanachama hai wa Yanga?
Mwanasheria wa Yanga, Simon Patrick ametolea ufafanuzi kupitia akaunti yake ya Instagram kwa kuandika; "Moja ya sifa ya kuajiriwa Yanga ni Uanachama, je Andre Mtine ni Mwanachama wa Yanga? ," ameendelea
"Ndugu zangu wana Yanga, kigezo cha Uanachama kwenye ajira ni takwa la Katiba ya Yanga na haliwezi kukiukwa,"
"Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Yanga imeidhinisha ajira ya Mr. Andre Mtine kama Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Yanga kwa mujibu wa ibara ya 37(1) ya Katiba ya Yanga 2021.
Ibara hiyo imeipa Kamati ya Utendaji mamlaka endapo itaona inafaa kuajiri mtaalamu kutoka nje kwenye nafasi yoyote ya kiutendaji basi kigezo cha Uanachama hakitazingatiwa.
Hivyo napenda kuwajuza kwamba kwa ajira za wataalamu kutoka nje sio lazima mwajiriwa awe Mwanachama.
Ukiachana na hilo, Mtine ni mwanachama hai na ana kadi ya Yanga, na kama mlivomsikia ni Yanga kindakindaki.
Yanga ni taasisi inayoongozwa kwa mujibu wa Katiba na sheria, na muda wote itaendelea kuheshimu na kufuata sheria zote zinazohusika.
Naipongeza Kamati ya Utendaji ya Yanga chini ya Rais injinia Hersi Said kwa kuendelea kuijenga Yanga kama taasisi,"