Waziri Junior: Ligi ya Kenya ni suala la muda
Muktasari:
- Junior, ambaye amejiunga na Mombasa United kwa ajili ya msimu wa 2026-2027, amesema uamuzi wake wa kwenda Kenya ni changamoto mpya kwake katika kuendeleza kipaji na kuhakikisha anakuwa sehemu muhimu ya kikosi hicho.
MSHAMBULIAJI Mtanzania aliyetua Mombasa United ya Kenya, Waziri Junior amesema anahitaji muda kuonyesha uwezo wake katika klabu hiyo, akisisitiza mpira wa miguu hujengwa zaidi na vitendo uwanjani kuliko maneno.
Junior, ambaye amejiunga na Mombasa United kwa ajili ya msimu wa 2026-2027, amesema uamuzi wake wa kwenda Kenya ni changamoto mpya kwake katika kuendeleza kipaji na kuhakikisha anakuwa sehemu muhimu ya kikosi hicho.
“Ni suala la muda kujua nitafanya nini katika msimu huu nikiwa na timu mpya. Mpira wa miguu hauoni maneno mengi zaidi ya vitendo uwanjani. Sijaona tofauti kubwa na ligi ya Tanzania,” amesema Junior.
Ameongeza, licha ya muda mfupi aliokaa Kenya, amegundua baadhi ya tofauti katika utendaji wa watu wanaohusika na soka, hasa namna wanavyotekeleza majukumu yao bila kusukumwa.
“Ingawa nilichokiona huku kwa muda mfupi ni watu ambao wanapenda sana kufanya kazi bila kusukumwa. Ndiyo maana nasisitiza muda utaongea, acha kazi iendelee kufanyika,” amesema.
Junior si mgeni wa kucheza nje ya Tanzania, kwani Februari 7, 2025 alijiunga na Al-Minaa ya Ligi Kuu ya Iraq kabla ya kurejea nchini na kutua Dodoma Jiji.
Katika msimu wa 2025-2026 akiwa Dodoma Jiji, Junior alifunga mabao matatu, baada ya kucheza kwa takribani miezi sita.
Mshambuliaji huyo alianza kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2014-2015 akiwa Toto Africans, ambapo aliweka rekodi ya kufunga bao pekee katika ushindi dhidi ya Simba, matokeo yaliyokuwa sehemu ya safari ya Yanga kutwaa ubingwa msimu huo.
Akizungumzia safari yake ya soka, Junior amesema hapendi kukimbia changamoto mpya, akiamini mazingira magumu humsaidia kukua kama mchezaji na mtu.
“Mimi ni kati ya wachezaji ambao hawahofii kupata chalenji mpya na kuanza upya ninapopitia changamoto, kwani naamini hizo zinanikomaza na kuwa mtu mwingine kabisa. Pia najifunza kwa watu ambao hawakati tamaa,” amesema.
Akimtaja nyota wa kimataifa wa Ureno, Cristiano Ronaldo, anayecheza Al-Nassr ya Saudi Arabia, Junior amesema mchezaji huyo ni mfano kwake wa mtu anayepambana na changamoto na kuendelea kutafuta mafanikio.
Kwa upande mwingine, Junior amesema bado anaendelea kuzoea baadhi ya maisha ya Kenya, akitaja vyakula kuwa miongoni mwa mambo mapya aliyokutana nayo.
Amesema moja ya mambo yaliyomshangaza ni namna baadhi ya watu wanavyokula ugali kwa kutumia vijiko, jambo ambalo kwake ni tofauti na alivyozoea Tanzania.
DATA ZA JUNIOR
Katika misimu yake ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Waziri Junior amekuwa na nyakati tofauti za ufungaji mabao, akianza msimu wa 2015-2016 akiwa Toto Africans, ambako alicheza mechi 13 na kufunga mabao saba.
Msimu uliofuata wa 2016-2017 alihamia Azam FC, akicheza mechi 17 na kufunga mabao saba, kabla ya msimu wa 2018-2019 kuichezea Biashara United, ambako alicheza mechi sita na kufunga mabao matatu.
Msimu wa 2019-2020 akiwa Mbao FC, Junior alifanya vizuri zaidi kwa kufunga mabao 13 katika mechi 17.
Msimu wa 2020-2021 alicheza Yanga, ambako alicheza mechi nne na kufunga mabao mawili, kabla ya kuhamia Dodoma Jiji msimu wa 2021-2022, akicheza mechi saba na kufunga mabao manne.
Msimu wa 2022-2023 alicheza KMC mechi tatu na kufunga bao moja, huku msimu wa 2023-2024 akiongeza kiwango chake baada ya kufunga mabao 12 katika mechi 17 akiwa na timu hiyo.
Katika msimu wa 2024-2025 akiwa Dodoma Jiji, Junior alifunga bao moja, kabla ya kuongeza mabao matatu msimu wa 2025-2026, ikiwa ni msimu wake wa mwisho kabla ya kujiunga na Mombasa United ya Kenya.