Uwanja wa AFCON Zanzibar wafikia asilimia 81
Muktasari:
- Uwanja huo unaojengwa na kampuni ya Urkun kutoka Uturuki, ukikamilika unatarajia kubeba watu 35000.
Wakati uwanja utakotumika katika Fainali za Mataifa ya Africa (Afcon) ukifikia asilimia 81, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeeleza kuridhishwa na hatua zilizofikiwa katika ujenzi huo.
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah ameyasema hayo baada ya kufanya ziara kutembelea uwanja huo leo Agosti 17, 2026 Fumba, Unguja.
Abdullah amesema hakuna sababu ya uwanja huo kutokamilika kwani tayari asilimia 95 ya vifaa vipo eneo la ujenzi jambo ambalo limempa faraja.
“Wapo watu wamekuwa na wasiwasi ikiwa uwanja huu upoje na kama utatumika. Lakini tayari uwanja umefikia asilimia 81. Niwahakikishie utaisha na kutumika kama ilivyopangwa.
"Tayari vifaa zaidi ya asilimia 95 vipo. Hili ni jambo ambalo limenipa faraja na wakandarasi wamenihakikishia ndani ya wiki mbili mpaka wiki tatu zinazokuja hapa kutakuwa na mabadiliko makubwa,” amesema Abdullah.
Abdullah amesema wanaridhika na hatua kubwa iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi wa huo na kuwaambia watanzania hasa wale wenye wasiwasi kuwa maendeleo ya mradi huo ni mazuri na kazi inaendelea.
Makamu huyo wa Rais Zanzibar amesema upo uwezekano uwanja huo ukatumika kwa mashindano ya Kombe la Mapinduzi.
“Tunaamini mwezi Desemba ama Januari utakuwa umeshakamilika na hata usichangae mechi ya Mapinduzi Cup ikachezwa hapa kwani kazi inaendelea vizuri,” amesema.
Amesema kila baada ya muda atautembelea mradi huo kuhakikisha wanahimizana ili kuona unakamilika kwa wakati.
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma amempongeza Abdullah kwa uamuzi wake wa kufanya ziara hiyo ambayo imelenga kuangalia maendeleo ya mradi huo lakini pia kufuata maelekezo wanayoyapokea kutoka kwa mkuu wa nchi.
Naye mratibu wa mradi huo kutoka kampuni ya Urkun, Ahmet Isler amesema kwa sasa vifaa vingi vimeshafika na wanaendelea na hatua ya kuviunganisha.
Uwanja huo unaojengwa na kampuni ya Urkun ya nchini Uturuki, utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kubeba watu 35000.