Wazir Jr atua Mombasa United, Moallin afurahia
Muktasari:
- Mombasa United inayoshiriki Ligi Kuu Kenya baada ya kupanda daraja ikitokea National Super League, inafundishwa na Moallin anayekumbukwa kwa kuipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wuliopita.
ALIYEKUWA Kocha wa Yanga, Abdihamid Moallin, amefurahishwa na usajili wa mshambuliaji, Waziri Junior Shentembo katika kikosi cha Mombasa United baada ya nyota huyo kuachana na Dodoma Jiji.
Mombasa United inayoshiriki Ligi Kuu Kenya baada ya kupanda daraja ikitokea National Super League, inafundishwa na Moallin anayekumbukwa kwa kuipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wuliopita.
Akizungumzia usajili huo, Moallin alisema Shentembo ni mshambuliaji mzuri anayeamini atakuwa na mchango mkubwa katika safu ya ushambuliaji kutokana na uzoefu wake, jambo lililomvutia kumsajili ili kwenda kuongeza nguvu na nyota wengine.
“Usajili wake ni miongoni mwa mapendekezo yangu kwa ajili ya kuongezea nguvu eneo la ushambuliaji, kupata saini yake ni jambo nzuri kwetu kwa sababu kulikuwa na ofa mbalimbali kutoka timu nyingine zilizomuhitaji kumsajili,” alisema Moallin.
Moallin alisema usajili huo utaongeza chachu ya wachezaji wengine wa Kitanzania kuendelea kuonekana nje ya mipaka kwa sababu hata Ligi Kuu Bara wapo wengi wanaotokea Kenya na wanatua ili kujikuza zaidi.
Msimu uliopita, nyota huyo alirejea Dodoma Jiji baada ya kuondoka Februari 7, 2025 kwenda Al-Minaa ya Ligi Kuu ya Iraq kwa mkopo wa miezi sita, japo hakuitumikia baada ya Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kuchelewa kutoka.
Licha ya nyota huyo kujiunga na Dodoma Jiji tangu Agosti 15, 2025, akitokea Al-Minaa, alianza kuitumikia dirisha dogo la Januari 2026, baada ya ITC kutolewa.
Katika miezi sita aliyoichezea Dodoma Jiji alifunga mabao matatu Ligi Kuu Bara msimu uliopita huku ulio bora ni wa 2023-2024 akiichezea KMC aliposhika nafasi ya tatu kwa wafungaji bora na mabao 12.
Katika msimu huo, Waziri alizidiwa na kiungo mshambuliaji wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga 19 na kinara, Stephane Aziz KI wa Yanga aliyefunga 21 na kuibuka mfungaji bora kwa msimu wa 2023-2024.
Baada ya kuichezea Al-Minaa, mshambuliaji huyo alikuwa Mtanzania wa pili kucheza Ligi Kuu Iraq, akifuata nyayo za nyota wa zamani wa Yanga, Saimon Msuva anayeichezea sasa Newroz SC akitokea Al-Talaba.