Prime
Wawili mezani Yanga
YANGA inaendelea kukamilisha maboresho ya kikosi chake kwa ajili ya msimu mpya, huku viongozi wa klabu hiyo wakibakiwa na majina mawili ya mwisho katika harakati za kusajili kiungo wa kati (namba 6). Wachezaji wanaotajwa ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Mohamed Zoungrana.
Mohamed Zoungrana (anayefahamika pia kama Zagrana) kwa sasa ndiye anayehusishwa kwa kiwango kikubwa na tetesi za kujiunga na Yanga msimu wa 2026/2027.
Kwa sasa, nyota huyo anakipiga katika klabu ya MC Alger ya Algeria, ambako bado ana mkataba wa mwaka mmoja.
Taarifa za ndani zimeliambia Mwanaspoti Yanga inaendelea kufanya hesabu za kupata saini ya mchezaji huyo ili kuimarisha eneo la kiungo mkabaji, baada ya Mkenya Duke Abuya kushindwa kuziba ipasavyo pengo lililoachwa na Mganda Khalid Aucho, licha ya kuonyesha kiwango kizuri katika baadhi ya mechi alizopata nafasi ya kucheza.
Zoungrana ametajwa mara kwa mara kuwa ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuvaa jezi namba sita katika kikosi hicho, ambacho tayari kimetambulisha nyota kadhaa wapya kwa ajili ya msimu ujao, akiwemo Peter Shalulile aliyesajiliwa kutoka Mamelodi Sundowns.
Mbali na Zoungrana, taarifa zinaeleza Yanga imeanzisha tena mazungumzo ya kumrejesha aliyekuwa kiungo wake, Feisal Salum ‘Fei Toto’, ambaye anatajwa kutaka kuondoka Azam FC.
Hata hivyo, Yanga inakabiliwa na ushindani kutoka kwa klabu mbalimbali, zikiwemo Simba, Orlando Pirates ya Afrika Kusini na Kaizer Chiefs.
Feisal amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake na Azam FC. Ingawa klabu hiyo imeanza mazungumzo ya kuongeza mkataba, inaelezwa mchezaji huyo amekataa kusaini mkataba mpya kutokana na nia yake ya kuondoka Chamazi.
Chanzo cha karibu na mchezaji huyo kilieleza Yanga tayari imeanza mazungumzo na wawakilishi wa Feisal, lakini hadi sasa hakuna makubaliano yaliyofikiwa wala mkataba uliosainiwa.
“Ni kweli Feisal anahitajika na Yanga, na viongozi wanaendelea kumshawishi ili wakae mezani kwa mazungumzo. Hata hivyo, bado hajatoa uamuzi wowote. Kuna timu nyingine pia zinazohitaji saini yake, huku Azam ikiendelea kupambana kuhakikisha anabaki. Mchezaji anaona kuna mambo ambayo hayajaenda sawa ndani ya timu hiyo na hata kama ataamua kubaki, hana mpango wa kusaini mkataba mpya,” kilisema chanzo hicho.
KINACHOENDELEA
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Yanga inaendelea kufanya tathmini ya mwisho kati ya Feisal na Zoungrana, ikizingatia mahitaji ya benchi la ufundi pamoja na malengo ya klabu katika mashindano ya ndani na kimataifa.
Mmoja wa viongozi wa Yanga amesema:
“Mpango uliopo ni kusajili kiungo mmoja kati ya Feisal na Zoungrana. Uamuzi wa mwisho bado haujafanyika, lakini mmoja wao ndiye anayetarajiwa kuvaa jezi ya Yanga msimu ujao. Wote ni wachezaji wenye mikataba na klabu zao, hivyo sio wachezaji huru.”
Iwapo mazungumzo na Feisal hayatakamilika, Yanga itaelekeza nguvu zake kwa Zoungrana ili kuhakikisha nafasi hiyo muhimu ya kiungo inazibwa kabla ya dirisha la usajili kufungwa. Endapo juhudi za kuwapata wote wawili zitashindikana, klabu hiyo ina orodha ya wachezaji wengine ambao inaweza kuwafuatilia.
Hata hivyo, hadi sasa Yanga haijatoa tamko rasmi kuhusu usajili wa mmoja wa wachezaji hao. Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amesema:
“Yanga tayari imepata kiungo namba sita. Kilichobaki ni suala la muda tu kabla ya kumtangaza rasmi, kwani uongozi umebakiza hatua chache kukamilisha dili hilo.”