Koyi, Kishamba wanaitaka nafasi ya ujumbe Yanga
Muktasari:
- Tuanze na Koyi ambaye ni mwanachama wa muda mrefu. Huyu kitaaluma ni mshauri wa masuala ya kikodi, elimu yake ya juu ni shahada ya uzamili ya sheria za kodi akihitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pia akiwa mfanyabiashara.
TUNAENDELEA kuwamulika wagombea wa nafasi ya ujumbe kwenye uchaguzi wa klabu ya Yanga utakaofanyika Agosti 2, 2026, jijini Dar es Salaam na leo tutakuwa na Julius Koyi na mgombea pekee wa kike, Prisca Kishamba.
Tuanze na Koyi ambaye ni mwanachama wa muda mrefu. Huyu kitaaluma ni mshauri wa masuala ya kikodi, elimu yake ya juu ni shahada ya uzamili ya sheria za kodi akihitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pia akiwa mfanyabiashara.
Koyi sio jina geni sana kwenye soka hasa utawala, kwani alikuwa mmiliki wa Mbeya Kwanza kabla ya timu hiyo kuuzwa kule Tabora ikinunuliwa na Yusuf Kitumbo, akiianzisha kutoka chini na baadaye kuja juu kushiriki Ligi Kuu Bara kabla ya baadaye kushuka daraja.
Kigogo huyo amekuwa kwa karibu sana na baadhi ya viongozi wa kamati ya mashindano akiwa mmoja wa wajumbe ambao wamekuwa wakitoa mchango wake kufanikisha majukumu mbalimbali ya kuitafutia Yanga ushindi.
Kama ulisafiri na Yanga msimu uliopita kwenda safari yoyote nje ya nchi utakuwa umeiona sura yake, kwani amekuwa akionekana kwenye misafara mingi ya timu hiyo.
Koyi anautaka ujumbe na amejipanga kwenda kutoa akili yake na utumishi wake wa wazi kwa kuyatekeleza maono ya Rais atakayechaguliwa, Injinia Hersi Said ambaye anagombea kutetea kiti chake.
“Kwanza niwapongeze sana viongozi wetu ambao walikuwa kwenye madaraka katika awamu inayomalizika, wamefanya kazi kubwa sana, lakini uwepo wa uchaguzi ni kutoa fursa ya sisi wengine kupata nafasi ya kuitumikia klabu yetu ya Yanga,” anasema Koyi.
“Mimi sina ilani lakini nipo tayari kwenda kuungana na wenzangu tutakaochaguliwa kwenda kuwatumikia wanachama na mashabiki wetu, kutekeleza maono ya rais wetu Hersi Said ambaye amekuwa mtu aliyeliongoza jahazi vyema.
“Natamani kuona katika uongozi wetu kukuza thamani ya wanachama, kwa sasa shabiki na mwanachama ni kama wanapata haki sawa, hii siyo sawa, tunatakiwa kubadilisha mambo ili mashabiki wengi waone umuhimu wa kuwa wanachama.”
PRISCA KISHAMBA HUYU HAPA
Mgombea pekee wa kike kwenye uchaguzi wa Yanga mwaka huu ni mwanadada Prisca Kishamba, ambaye alishtua kwa kujitosa kuutaka ujumbe wa kamati ya utendaji wa klabu hiyo na kuleta mvuto wa aina yake mara tu baada ya kuchukua fomu.
Kishamba ni jina maarufu miongoni mwa watu wa vyombo vya habari akiwahi kuwa mtumishi wa Clouds Media kabla ya baadaye kuanzisha kituo chake cha Kishamba Media ambacho kipo hadi sasa.
Kishamba ni mtaalamu wa mawasiliano, mwandishi wa habari kwa miaka 10 akiwa na Clouds Media na mjasiriamali mwenye uzoefu katika sekta ya habari, mawasiliano na usimamizi wa matukio kupitia kampuni yake ya Kishamba Media na Kishamba Tents and Events.
Kwa miaka ya utumishi wake, amejijengea sifa kwa uwezo wake wa kuwasiliana kwa ufasaha, kujenga mahusiano na wadau mbalimbali, pamoja na kushiriki katika shughuli zinazochangia maendeleo ya jamii na michezo nchini.
Katika sekta ya michezo, Prisca ni mdau anayejitolea kuimarisha utawala bora, uwazi na ushirikishwaji. Amewahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Motisha ya Timu za Taifa na kwa sasa ni mjumbe wa Kamati ya Tuzo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Aidha, amejitokeza kugombea nafasi ya uongozi ndani ya klabu ya Yanga akiwa na dhamira ya kuchangia maendeleo ya klabu kupitia uongozi wenye uwajibikaji, mawasiliano madhubuti na ushirikishwaji wa wanachama.
Mbali na shughuli zake za kitaaluma, Prisca anaamini katika uwezeshaji wa vijana na wanawake, ujenzi wa taasisi imara na matumizi ya mawasiliano kama nyenzo ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Anatambulika kwa uadilifu, bidii, ubunifu na uwezo wa kuunganisha watu ili kufikia malengo ya pamoja.
“Sitaki wanachama wenzangu wa Yanga wanichague kama mwanamke bali kama mgombea ambaye nina shauku kubwa ya kwenda kuwa sauti ya wanachama wenzangu wengine wa kike na wa kiume,” alisema Kishamba.
“Nataka kuwa sehemu ya mabadiliko ya timu yetu ya wasichana Yanga Princess, kuna mabadiliko inayapitia lakini nimepanga kwenda kuweka nguvu zaidi nikishirikiana na wenzagu kuipa mafanikio makubwa.”