Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

2026/27 Yanga inabebwa na mifumo mitatu

YANGA Pict


HADI kufikia sasa, Yanga imeonekana kuimarisha zaidi eneo lake la ushambuliaji ambalo linadhihirisha msimu ujao litakuwa hatari zaidi ya ilivyokuwa msimu uliopita 2025-2026.


Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya NBC baada ya msimu wa 2025-2026 kufunga mabao 71 katika ligi yakiwa machache kulinganisha na msimu wa nyuma yake 2024-2025 walipofunga 83, kuna maboresho yamefanyika yanayotoa taswira chanya ya kuamua nani aanze kulingana na mifumo ilivyo.


Kupitia usajili wa dirisha kubwa, Yanga imeshusha washambuliaji waliokuwa wakifanya vizuri walipotoka akiwemo mshambuliaji raia wa Namibia, Peter Shalulile.

Usajili wa Shalulile umeongeza uzito mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya Yanga na sasa umeiweka benchi la ufundi chini ya kocha Manqoba Mngqithi kwenye nafasi ya kufanya uamuzi mgumu kuhusu nani aanze na nani akae benchi, lakini pia upande mwingine ni hatari kwa wapinzani kutokana na nyota waliopo.

Yanga imejenga kikosi chenye ushindani mkubwa eneo la mbele baada ya kuwasajili wachezaji wenye uwezo tofauti, huku lengo likiwa ni kutetea ubingwa wa Ligi Kuu NBC kwa mara ya sita mfululizo na kufanya vizuri zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Shalulile ametambulishwa rasmi baada ya kujiunga na Yanga akitokea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

YANGA Pict

WASHAMBULIAJI WATANO

Yanga ina washambuliaji watano wa kati ambao kila mmoja ana uwezo wa kuanza kikosini.

Wapo Shalulile, Laurindo Aurelio ‘Depu’, Cheick Ibrahim Toure, Clement Mzize na kinda Hussein Mihambo aliyesajiliwa kutoka Mashujaa.

Depu ameendelea kubaki kikosini baada ya kuonyesha uwezo mzuri tangu aliposajiliwa dirisha dogo la msimu uliopita lakini pia kuna taarifa za kuwepo mazungumzo ya kumtoa iwe kwa mkopo au kumuuza kama wakikubalaina, huku Mzize akirejea mazoezini baada ya kupona jeraha la goti lililomuweka nje kwa muda mrefu. Hata hivyo, taarifa zinasema atarejea rasmi uwanjani Desemba 2026.

Toure naye amewasili akitokea Al Jabalain ya Saudi Arabia akiwa na sifa ya kufunga mabao 19 katika msimu wake wa mwisho, wakati Mihambo anatarajiwa kujifunza na kukua akiwa nyuma ya washambuliaji wakongwe zaidi.

Miongoni mwa washambuliaji hao, Shalulile ndiye mwenye uzoefu mkubwa zaidi.

Katika kipindi chake cha misimu sita akiwa Mamelodi Sundowns aliweka rekodi ya kuwa mmoja wa wafungaji bora wa Ligi ya Afrika Kusini, akifunga mabao 68, ingawa msimu wake wa mwisho haukuwa mzuri baada ya kumaliza akiwa na mabao matatu pekee.

Depu alifunga mabao tisa, huku Toure akiwasili akiwa katika kiwango kizuri baada ya kufunga mabao 19 nchini Saudi Arabia.

Kwa upande wa Mzize, kurejea kwake kunampa Mngqithi silaha nyingine muhimu kutokana na kasi, nguvu na uwezo wake wa kushambulia nafasi.

Mbali na washambuliaji wa kati, Yanga pia imeongeza ushindani kwenye nafasi za mawinga.

Kikosi hicho sasa kina Allan Okello, Maxi Nzengeli, Albert Kangwanda, Housseine Zakouani, Juma Abushiri “Chuga” na Erick Mwijage.

Hata hivyo, Pacome Zouzoua hataonekana msimu huu baada ya kupata jeraha kubwa lililohitaji upasuaji. Yanga imeamua kumtoa kwenye mfumo kwa msimu huu huku ikiendelea kugharamia matibabu yake hadi atakapokuwa tayari kurejea uwanjani.

Usajili huo eneo la mbele, unampa kocha Mngqithi kuwa na machaguo mengi ya mifumo ndani ya kikosi chake.

YANGA Pict

MFUMO WA 4-4-2

Iwapo Mngqithi ataamua kutumia mfumo wa 4-4-2, atakuwa na nafasi ya kuwachezesha washambuliaji wawili wa asili kwa pamoja.

Katika mfumo huu, Allan Okello anaweza kucheza winga wa kulia huku Maxi Nzengeli akitokea kushoto, Mudathir Yahya akisimama nyuma ya washambuliaji wawili.

Mbele, Mzize na Depu wanaweza kuunda pacha wa ushambuliaji unaochanganya kasi ya Mzize na uwezo wa Depu wa kushikilia mpira na kumalizia mashambulizi.

Mfumo huu unaweza kuifanya Yanga iwe hatari zaidi ndani ya eneo la penalti kwa kuwa itakuwa na washambuliaji wawili wa asili wanaoshambulia kwa wakati mmoja.

MASHINE Pict

MFUMO WA 4-5-1

Katika mfumo wa 4-5-1, Yanga inaweza kuongeza idadi ya viungo huku ikitumia ubunifu wa mawinga.

Housseine Zakouani anaweza kuanzia upande wa kulia na Albert Kangwanda kushoto wakitengeneza nafasi nyingi kupitia pembeni.

Mbele kabisa anaweza kusimama Cheick Ibrahim Toure akiwa mshambuliaji wa mwisho, huku Peter Shalulile akicheza nyuma yake kama mshambuliaji wa pili anayezunguka kutafuta nafasi na kutumia uzoefu wake wa kusoma mchezo.

Mfumo huu unaweza kuifanya Yanga iwe na umiliki mkubwa wa mpira huku ikitengeneza mashambulizi kupitia viungo na mawinga.

SHALULILE Pict

MFUMO WA 4-3-3

Endapo Mngqithi atachagua mfumo wa 4-3-3, atakuwa na nafasi ya kutumia kasi ya mawinga wake vijana.

Abushiri anaweza kucheza upande wa kulia, Mwijage kushoto, huku Shalulile akiwa namba tisa wa kati.

Mzize anaweza kutumika kama mshambuliaji wa pembeni anayekata kuelekea katikati au kubadilishana nafasi na Shalulile kulingana na hali ya mchezo.

Mfumo huu unategemea mashambulizi ya kasi, presha kubwa kwa wapinzani na matumizi ya nafasi za pembeni, jambo ambalo linaweza kuwafanya mawinga wa Yanga kuwa silaha muhimu.

Kwa kikosi kilichopo sasa, ushindani wa nafasi ya ushambuliaji ni mkubwa kuliko misimu iliyopita.

Ni ushindani ambao unaifanya Yanga iwe na nguvu, pia unampa Mngqithi kazi ngumu ya kuchagua mfumo sahihi na wachezaji wanaoweza kuanza kila mechi.

Kwa kifupi, Yanga imejenga safu ya ushambuliaji yenye machaguo mengi, jukumu la kuamua nani aanze, nani akae benchi na mfumo upi utumike, limebaki kwa Manqoba.