Washindi Nane wa kampeni ya Tembocard kushuhudia AFCON 2023
Dar es Salaam. Benki ya CRDB imezindua kampeni ya Tisha na Tembocard Tutakiwashe Afcon ambapo jumla ya washindi nane watahudhuria fainali hizo zilizopangwa kuanza Januari 13 mpaka February 11 mwakani nchini Ivory Coast.
Kampeni hiyo ilizinduliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Majjid Nsekela, ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa michezo pamoja na wachezaji wa zamani wa timu ya Taifa, Abdallah Kibadeni, Edibili Lunyamila na Athuman Idd”Chuji”.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Msigwa aliipongeza benki ya CRDB kwa kazi kubwa ya kuhamasisha maendeleo ya michezo nchini na kupitia kampeni hiyo itawawezesha Watanzania kwenda kuishangilia timu yao ya Taifa ambayo imefuzu katika mashindano hayo.
“Kampeni hii imekuja wakati muafaka ambapo wateja wa benki ya CRDB watapata fursa ya kuishuhudhia na kuishangalia Taifa Stars ambayo imefuzu kushiriki katika mashindano hayo. Naipongeza Benki ya CRDB na Visa kwa mpango huu, ambao utatoa fursa ya kipekee kwa washindi kwenda kushuhudia fainali hizo,” alisema Msigwa.
"Uchumi wa kidijitali unahitaji njia za kisasa za malipo ambazo hazihitaji watu binafsi kubeba pesa taslimu, kama TemboCard, ili kuwezesha malipo rahisi na ya haraka," alisisitiza.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Biashara wa benki ya CRDB, Boma Raballa alisema Ili kushinda nafasi ya kuhudhuria fainali za Afcon, mteja wa benki hiyo anatakiwa kufanya malipo kwa njia ya mtandao kwa kutumia TemboCard .
Raballa alisema kuwa mteja anaweza kufanya malipo pia kwa ni kulipa kupitia vifaa vya manunuzi (POS) kwenye maduka mbalimbali, supermarkets, migahawa, hoteli na vituo vya kuuzia mafuta na kuingia kwenye droo ya kutafuta washindi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Majjid Nsekela alisema kuwa wataendelea kuchochea maendeleo ya michezo nchini ambapo kwa sasa yameshika kasi.
Nsekela alisema kuwa benki yao ipo mstari wa mbele katika maendeleo ya michezo ikiwa pamoja na kuwaandaa wanamichezo.
Alisema kuwa kila mwaka Benki ya CRDB inaandaa mbio za CRDB Bank Marathon huku ikidhamini CRDB Bank Taifa Cup, kufadhili jezi za Zanzibar Heroes, Mashindano ya CRDB Bank Ngalawa Race, Timu ya Namungo pamoja na ligi za mikoa.
Katika kuwaleta mashabiki pamoja, Benki ya CRDB hushiriki matukio muhimu ya klabu kubwa nchini ya wiki ya Mwananchi ambayo inaandaliwa na klabu ya Yanga na Simba Day.