Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CECAFA yavunja ukimya madai ya Singida fedha za zawadi

Muktasari:

  • Kauli hiyo imetolewa jijini Kigali ambapo Andemariam amezungumzia changamoto zinazoikabili CECAFA na dira ya uongozi wake wa kuirejesha hadhi ya michuano hiyo ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa ikikumbwa na malalamiko ya klabu kuhusu malipo ya zawadi, maandalizi na ubora wa mashindano.

WAKATI Singida Black Stars ikiendelea kusubiri fedha za zawadi ya ubingwa wa Kombe la CECAFA Kagame 2025, Rais wa CECAFA, Paulos Weldehaimanot Andemariam, amekiri suala la kuchelewa kwa malipo limekuwa doa kwa mashindano hayo, akiahidi uongozi mpya hautaruhusu jambo hilo kujirudia.

Kauli hiyo imetolewa jijini Kigali ambapo Andemariam amezungumzia changamoto zinazoikabili CECAFA na dira ya uongozi wake wa kuirejesha hadhi ya michuano hiyo ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa ikikumbwa na malalamiko ya klabu kuhusu malipo ya zawadi, maandalizi na ubora wa mashindano.

Msimu uliopita, Singida Black Stars ilitwaa ubingwa wa Kagame 2025 ikiwa chini ya kocha Miguel Gamondi ambaye kwa sasa ni kocha wa Taifa Stars, lakini hadi sasa hawajapewa malipo ya fedha za zawadi ambapo ni dola 30,000 (Sh79.3 milioni).

TATIZO LILIPO

Bila kuficha, Andemariam anasema uongozi mpya umeikuta CECAFA ikiwa imepoteza sehemu ya imani ya klabu kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo kuchelewa kulipa fedha za zawadi.

Anasema baadhi ya timu bado zinaendelea kulalamikia kutopokea fedha zao na kwamba jambo hilo halipaswi kuendelea ikiwa CECAFA inataka kujenga mashindano yenye hadhi ya kimataifa.

“Kutakuwa na mabadiliko, bado kuna timu zinazolalamika kwa sababu hazijapokea fedha zao za zawadi. Hatuwezi kuruhusu hali hiyo iendelee kutokea,” anasema Andemariam.

Ingawa Andemariam hakuitaja Singida Black Stars moja kwa moja, kauli yake imekuja wakati mabingwa hao wa mwaka 2025 wakiwa miongoni mwa timu zenyemadai ya kucheleweshewa fedha za zawadi.

Hali hiyo imekuwa ikiibua maswali kuhusu uendeshaji wa michuano hiyo, hasa wakati CECAFA ikijaribu kuwashawishi wadhamini wapya na kuongeza ushiriki wa klabu kubwa kutoka ukanda huo.


HAKUNA NAMNA

Kwa mujibu wa Andemariam, jambo la kwanza analotaka kulifanya ni kurejesha imani ya klabu wanachama.

Anasema CECAFA haiwezi kuwa na mashindano yenye hadhi kama klabu zinaendelea kuingia mashindanoni zikiwa na wasiwasi kuhusu haki zao.

“Hatutaki tena kuona hali ya kutokuaminiana kati ya CECAFA na klabu, tunataka kila timu ijue kuwa ikishinda, itapata haki yake kwa wakati,” anasema.

Mbali na kuhakikisha malipo yanafanyika kwa wakati, Andemariam amesema pia ana mpango wa kuongeza kiwango cha fedha za zawadi katika miaka ijayo.

Anakiri kuwa mwaka huu haikuwezekana kufanya hivyo kutokana na muda mfupi wa maandalizi na changamoto za kifedha zilizokuwepo kabla ya uongozi mpya kuingia madarakani.

“Tayari kuna wadhamini wanaonyesha nia ya kufanya kazi nasi, hatukupata muda wa kukamilisha mazungumzo kabla ya mashindano ya mwaka huu, lakini katika siku zijazo fedha za zawadi zitaongezeka,” anasema.


RWANDA KUWA MFANO

Katika mkakati wa kuibadilisha CECAFA, Andemariam ameipa Rwanda nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha mageuzi hayo.

Anasema si bahati mbaya kwamba Rwanda imepewa kuandaa mashindano kadhaa ya CECAFA mfululizo, kwani nchi hiyo imeonyesha uwezo mkubwa wa kuandaa matukio ya kimataifa.

Kwa mujibu wake, viwanja vya kisasa, huduma bora kwa timu, usafiri na maandalizi ndiyo msingi wa kujenga mashindano yanayoweza kuvutia wadhamini zaidi.

Andemariam anasema ndoto yake ni kuona Kagame Cup ikifikia kiwango cha kuvutia klabu hata kutoka kanda nyingine za CAF.

Anakiri kuwa hapo awali baadhi ya klabu kutoka COSAFA, UNAF na maeneo mengine zilionyesha nia ya kushiriki, lakini kutokana na ratiba na changamoto za fedha, CECAFA ililazimika kubaki na timu za ukanda wake. Hata hivyo alisema hilo ni jambo la muda mfupi.

“Lengo letu ni kuifanya Kagame iwe miongoni mwa mashindano bora ya klabu Afrika. Tunataka hata klabu kutoka kanda nyingine ziwe zinatamani kushiriki,” anasema.

Andemariam anasema uongozi wake ulipata ridhaa ya kuongoza kwa ahadi ya kufanya mabadiliko makubwa ndani ya ukanda huo.

Anasema wanatambua kuwa CECAFA ni moja ya kanda kongwe ndani ya CAF, lakini kwa miaka mingi imekuwa ikibaki nyuma ukilinganisha na kanda nyingine.

“Tunahitaji mabadiliko, tunataka CECAFA ambayo klabu zitajivunia kushiriki, mashabiki watafurahia na wadhamini wataamini,” anasema.