Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanyama anafuata ratiba ya umri wa soka, sisi je?

Victor Wanyama

Muktasari:

Ukatae au ukubali, lakini hiyo ndio miaka yake. Kwa ukubwa wa klabu, Tottenham ni klabu kubwa kuliko Southampton ambayo amehama. Huwa inatokea Southampton kumaliza juu ya msimamo mbele ya Tottenham, lakini ukubwa wa Tottenham kwa Southampton upo wazi.

HATI ya kusafiria ya Victor Mugubi Wanyama inaonyesha alizaliwa Juni 25, 1991 jijini Nairobi. Siku kama ya juzi miaka 25 iliyopita. juzi hiyo hiyo ilikuwa siku yake ya pili kamili tangu awe mchezaji rasmi wa Tottenham. Furaha iliyoje?

Ukatae au ukubali, lakini hiyo ndio miaka yake. Kwa ukubwa wa klabu, Tottenham ni klabu kubwa kuliko Southampton ambayo amehama. Huwa inatokea Southampton kumaliza juu ya msimamo mbele ya Tottenham, lakini ukubwa wa Tottenham kwa Southampton upo wazi.

Spurs wapo mbele kwa ukubwa wa uwanja, mafanikio katika Ligi, FA, kushiriki Ligi ya Mabingwa na mengineyo.

Hata katika akaunti zao, Tottenham ni matajiri zaidi kwa Southampton. Mchezaji wao ghali aligharimu pesa nyingi kuliko wa Southampton.

Katika madaraja ya soka, Tottenham ipo daraja la chini kidogo kwa Arsenal, Manchester United, Liverpool, Chelsea na sasa Manchester City. Kwa Ulaya nyingine wapo chini ya Real Madrid, Barcelona, AC Milan, Inter Milan, Bayern Munich na hata Borussia Dortmund.

Katika hali halisi, inawezekana mchezaji akatokea Genk kwenda Real Madrid au Manchester United, lakini huwa inatokea nadra sana mchezaji anapaswa kwanza kuhama kutoka Genk kwenda Tottenham halafu baada ya hapo aende timu ya juu zaidi ambapo, anaweza kuangukia Real Madrid, Barcelona au Manchester United.

Christian Benteke alitoka Genk, akaenda Aston Villa, ambayo ni kama Tottenham, halafu akaenda Liverpool ambayo ni ya juu zaidi. Suala la msingi zaidi ni kujiuliza, unatafuta kucheza timu kubwa ukiwa na umri gani?

Wanyama ana miaka 25 na yupo Tottenham. Ina maana ndani ya miaka miwili akiwa na umri wa miaka 27 anaweza kwenda timu ya juu zaidi ya Tottenham kwa sababu umri utakuwa unamruhusu.

Mbwana Samatta ameingia Ulaya akiwa na umri wa miaka 23. Anaweza kuuzwa kwenda Southampton akiwa na miaka 25. Baada ya hapo kama aking’ara sana basi anaweza kuuzwa kwenda Tottenham akiwa na miaka 27. Itakuwa vigumu kwake kuuzwa kwenda timu kubwa akiwa na umri wa miaka 30.

Wazungu wanapenda kumnunua mchezaji ambaye atakuwa na thamani ya kuuzwa tena usoni (Resale value).

Ni vigumu sana kwa timu kubwa kumnunua mchezaji mwenye umri wa miaka 29 au 30 labda awe na kipaji kikubwa sana.

Hii inakuonyesha kuwa katika umri wa miaka 23 Samatta amechelewa kwenda Ulaya. Bahati nzuri kwake kinachoweza kumrusha kwenda mbali na juu kwa haraka zaidi ni kwa sababu washambuliaji wanauzika kwa urahisi zaidi wakifanya kazi zao kwa ufasaha kuliko wachezaji wa nafasi nyingine.

Katika umri wa miaka 25 ambao Wanyama anayo sasa, kwa mujibu wa hati yake ya kusafiria, tayari amecheza katika klabu za Helsingborg ya Sweden, Beerschot ya Ubelgiji, Celtic ya Scotaland, Southampton na sasa ameingia Tottenham. Katika umri wa miaka 23 ndiyo kwanza Samatta ameingia Ulaya.

Hii inamaanisha kuwa wachezaji wetu wasichelewe kwenda nje kama wanaamua kufunga safari. Hasa nyakati hizi ambazo Watanzania tunaendelea kuota ndoto ya kuona wachezaji wetu wanacheza katika timu kubwa kama Manchester United, Real Madrid, Barcelona na nyinginezo. Safari haiwi rahisi sana kama tunavyofikiri.

Inashangaza sana mchezaji anahojiwa na mwandishi wa habari akiwa na umri wa miaka 22 halafu anaudanganya umma kwamba, ndoto yake ni kuichezea Manchester United. Labda kama ni Manchester United ya Ukonga Madafu.

Utafika lini Manchester United ya Old Trafford? Kwa mzunguko upi ambao mpaka leo Wanyama hajafika halafu wewe unafika.

Iwe kwa udanganyifu wa miaka au kwa miaka halisi, mchezaji wa Tanzania mwenye ndoto za kufika mbali kisoka huku akicheza katika timu kubwa za juu lazima aondoke nchini huku hati yake ya kusafiria ikionyesha ana umri wa miaka 17 au 18.

Ni rahisi kwa mchezaji aliyezaliwa Ulaya kutoka katika timu ndogo kwenda katika timu kubwa moja kwa moja. Lakini kwa mchezaji aliyetoka Afrika lazima atachukua muda kuweza kufika juu kwa sababu ana mambo mengi ya kurekebishwa.

Nilipokuwa Genk Machi mwaka huu nilizungumza na Samatta kuhusu hili. Aliniambia wazi kwamba anajuta kupoteza muda mwingi akiwa TP Mazembe. Nilimkubalia kutokana na hali halisi niliyoiona katika soka la Ubelgiji.

Muda mwafaka wa Samatta kwenda Ulaya ungeweza kuwa ule ule alipochomoza Tanzania akiwa na Simba akitokea African Lyon. Kama moja kwa moja angeweza kwenda Sweden au Ubelgiji, leo Samatta angekuwa katika moja kati ya timu kubwa barani Ulaya kuliko Genk.

Hata hivyo, afadhali yeye ameanza kuliko hawa ambao wanatudanganya huku wakiwa na umri wa miaka 22 halafu anataka kwenda kucheza Manchester United. Wanyama ndiye amefuata vyema ratiba ya umri mpaka sasa.

Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwanaspoti au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz