Gor Mahia yatinga fainali kwa matuta
GOR Mahia ya Kenya imekuwa timu ya kwanza kutinga fainali ya Kombe la CECAFA Kagame 2026 baada ya kuiondoa Al Hilal ya Sudan kwa ushindi wa mikwaju ya penalti 8-7 kufuatia sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 120 za mchezo wa nusu fainali uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Kigali Pele.
Gor Mahia ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 37 baada ya beki wa Al Hilal, Steven Ebuela kujifunga alipokuwa akijaribu kumrudishia kwa kichwa kipa wake, Soufiane Ouedraogo.
Al Hilal ilirejea mchezoni na kusawazisha dakika ya 44 kupitia mshambuliaji wake Mgambia, Ansumana Samura, aliyehitimisha vizuri shambulizi lililoiacha Gor Mahia ikiwa haina jibu kabla ya mapumziko.
Kipindi cha pili kilikuwa na ushindani mkubwa huku kila timu ikitengeneza nafasi za kufunga, lakini uimara wa safu za ulinzi na makipa ulifanya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Gor Mahia ilipata pigo baada ya beki wake Dwang kuonyeshwa kadi nyekundu na kuilazimu timu hiyo kucheza pungufu.
Hata hivyo, Al Hilal ilishindwa kutumia faida ya kuwa na mchezaji mmoja zaidi uwanjani huku Gor Mahia ikionyesha nidhamu kubwa ya ulinzi na kupeleka mchezo huo kwenye mikwaju ya penalti.
Katika mikwaju ya penalti timu hizo zilikwenda hatua kwa hatua kabla ya Gor Mahia kuibuka na ushindi wa penalti 8-7 na kutinga fainali ya mashindano hayo.
Ushindi huo unaifanya Gor Mahia kusubiri mshindi wa nusu fainali nyingine kati ya Rayon Sports ya Rwanda na Jamus SC ya Sudan Kusini ili kujua mpinzani wake katika fainali ya CECAFA Kagame 2026 itakayochezwa Agosti 7 kwenye Uwanja wa Amahoro, Kigali.