Okwi atundika daruga, atakuwepo Simba Day
Muktasari:
- Okwi (33), ametangaza uamuzi huo muda mfupi baada ya kushuhudia Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Al Merrikh ya Sudan katika mchezo wa kirafiki uliochezwa leo, Jumanne, kwenye Uwanja wa FERWAFA, Kigali, Rwanda.
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba na nahodha wa timu ya taifa ya Uganda, Emmanuel Okwi ametangaza kustaafu soka la ushindani, akihitimisha safari ya miaka 18 uwanjani.
Okwi (33), ametangaza uamuzi huo muda mfupi baada ya kushuhudia Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Al Merrikh ya Sudan katika mchezo wa kirafiki uliochezwa leo, Jumanne, kwenye Uwanja wa FERWAFA, Kigali, Rwanda.
Katika ujumbe aliouposti kwenye mitandao yake ya kijamii, Okwi amesema umefika wakati wa kuaga soka la kulipwa, akieleza kuwa mchezo huo ulimpa kila kitu kuanzia ndoto, heshima, marafiki na mafanikio ambayo atayathamini kwa maisha yake yote.
Nyota huyo aliyewahi kuiongoza Uganda Cranes kama nahodha amesema kuvaa jezi ya timu ya taifa ilikuwa heshima kubwa kwake huku akizishukuru klabu zote alizozichezea, makocha, wachezaji wenzake na mashabiki waliomuunga mkono katika kipindi chote cha maisha yake ya soka.
Akizungumza na Mwanaspoti jijini Kigali, Okwi amesema licha ya kutundika daruga, atakuwa sehemu ya familia ya Simba kwa kuhudhuria tamasha la Simba Day litakalofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
"Nitasafiri kesho pamoja na kikosi cha Simba kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya Simba Day. Nimealikwa kwenye tamasha hilo na nitakuwepo kushiriki pamoja na familia ya Simba," amesema Okwi.
Okwi aliichezea Simba kwa mafanikio makubwa na kuwa mmoja wa wachezaji waliopendwa na mashabiki wa klabu hiyo kutokana na kiwango bora na mchango wake katika mafanikio ya timu hiyo.
Mbali na Simba, mshambuliaji huyo pia aliwahi kucheza katika klabu mbalimbali barani Afrika na Ulaya huku timu yake ya mwisho ikiwa Polisi ya Rwanda.