Wakongomani waibeba Yanga ikianza msimu na ushindi
Muktasari:
- Yanga imelazimika kusubiri mpaka dakika ya 68 kupata bao lake la kwanza msimu huu, likifungwa na beki Mkongomani, Chadrack Boka kwa kichwa akipokea krosi ya Housseine Zakouani baada ya kuanziana kona fupi na Albert Kangwanda.
YANGA imeanza vizuri Ligi Kuu Bara msimu wa 2026-2027, baada ya kuichapa Namungo nyumbani kwao mabao 3-1, huku mabao yake mawili kati ya matatu yakifungwa na Wakongomani.
Yanga imelazimika kusubiri mpaka dakika ya 68 kupata bao lake la kwanza msimu huu, likifungwa na beki Mkongomani, Chadrack Boka kwa kichwa akipokea krosi ya Housseine Zakouani baada ya kuanziana kona fupi na Albert Kangwanda.
Hiyo inakuwa asisti ya kwanza kwa Zakouani kwenye mchezo wake wa kwanza wa ligi akiwa ni mmoja wa wachezaji wapya walioongezwa msimu huu.
Dakika mbili baadaye, Yanga ikapata bao la pili dakika ya 71 likifungwa kwa shuti kali na kiungo Mkongomani, Maxi Nzengeli, baada ya kuunasa mpira uliokuwa unaokolewa na Alex Masawe.
Kabla ya kujaa wavuni, kipa wa Namungo, Suleiman Said atajilaumu mwenyewe kwa kushindwa kuokoa shuti hilo kali la chinichini likijaa wavuni.
Namungo ikafanikiwa kupata bao lao pekee dakika ya 76 likifungwa na mshambuliaji Hubert Lukindo kwa shuti kali, akiirudisha timu yake mchezoni akifunga dakika saba tangu aingie uwanjani.
Wakati Namungo ikitafuta bao la kusawazisha, ikajikuta inaruhusu la tatu likifungwa na mshambuliaji raia wa Namibia, Peter Shalulile akinufaika na makosa ya beki wa wenyeji, Frank Magingi akishindwa kuzuia pasi ya kurudishiwa na mwenzake, Khamis Nyenye.
Huo unakuwa ushindi wa kwanza kwa Yanga msimu huu katika mechi yake ya kwanza ikiendeleza ubabe wake kwa Namungo ambayo haijawahi kushinda mbele ya mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara.
Ushindi huo unaifanya Yanga kuanza vizuri harakati zake za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara iliouchukua jumla mara 32, huku tano ikiwa mfululizo kuanzia 2021-2022.