Wadau wa soka wamuaga Kifukwe, kuzikwa kesho Mbeya
Muktasari:
- Kifukwe alifariki dunia Agosti 15, 2026 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu ambapo leo Alhamisi klabu ya Yanga iliandaa tukio maalum la kumuaga, likifanyika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
WADAU wa soka wamekutana kumuaga aliyekuwa Rais wa Yanga, Injinia Francis Kifukwe, huku salamu mbalimbali zawasifu wake zikitamalaki.
Kifukwe alifariki dunia Agosti 15, 2026 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu ambapo leo Alhamisi klabu ya Yanga iliandaa tukio maalum la kumuaga, likifanyika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo, viongozi mbalimbali wa soka wakiongozwa na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, makamu wake Arafat Haji na wajumbe wa kamati ya utendaji, walihudhuria.
Mbali na viongozi hao, pia alikuwemo Mwenyekiti wa Simba SC, Murtaza Mangungu, huku Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likiwakilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Baraka Kizuguto.
Katika salamu zake, Hersi amesema Kifukwe alikuwa nguzo muhimu ya klabu hiyo ambapo wakati wa kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa kisasa, alishiriki kubadilisha nyaraka mbalimbali huku akiwa anaumwa.
"Unaweza kumuelezea kwa mengi Kifukwe alikuwa kiomgozi ambaye Yanga ilikuwa inatangulia kabla ya mengine, mimi binafsi mara ya mwisho hivi karibuni tulikutana na changamoto moja katika kubadilisha mfumo wa uendeshwaji," amesema Hersi.
"Tulikuta kuna nyaraka nyingi zilifunguliwa na kusajiliwa kisheria, ili tuweze kuendelea na mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshwaji ilibidi hizo nyaraka zote ziwe na taarifa zinazolingana na mtu sahihi aliyetakiwa kutusaidia hilo alikuwa Kifukwe.
"Nikapiga simu moja tu kwenda kwake akanipokea, akaniambia afya yake haipo sawa lakini nimtume kijana aende kwake atasaini, nikafanya hivyo baada ya muda mfupi tukafanikiwa, hili lilinipa funzo kubwa sana juu ya utayari wake."
Wakati Hersi akisema hivyo, Mangungu ambaye aliiwakilisha Simba, amesema Kifukwe alikuwa kiongozi wakweli ambapo alishiriki na kusimamia msiba wa aliyekuwa mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Dk Arnold Kashembe.
"Tukio ambalo sitalisahau ambalo lilinikutanisha na Kifukwe ni wakati Simba tulipopata msiba wa aliyekuwa afisa mtendaji mkuu, Dk Kashembe, Kifukwe alinipigia kunipa taarifa za msiba na akaniambia msiba utafanyika hapa kwangu.
"Tukashirikiana naye vizuri lakini kabla ya siku ya kwenda kuzika, tulikuwa na safari na timu yetu (Simba), nikamwambia kaka, timu ina safari na mimi natakiwa kuwa sehemu ya safari lakini sitakwenda.
"Nitakuwa hapa mpaka tukamilishe taratibu za mazishi, Kifukwe akanishtua sana akaniambia mwenyekiti, wewe tulikuwa sote kuanzia mwanzo, mimi nakuruhusu nenda kasimamie timu nayajua majukumu haya, mimi nitakamilisha hili.
"Hapa tunatakiwa kujifunza kwamba soka sio uadui kama ambavyo baadhi yetu wanafanya sasa, nje ya burudani hii sisi bado ni ndugu, nashukuru hapa wamesema wenyewe kwamba Kifukwe aliikuta hii timu inatembea kwa miguu," amesema Mangungu.
Mchezaji wa zamani wa Yanga, Ally Mayay 'Tembele' amesema wachezaji ambao walifanya kazi na Kifukwe hawakuwa wanamtambua kama rais bali walimuita jina la mwana kutokana na alivyokuwa anaishi nao karibu na kutatua shida zao.
Yanga kwenye msiba huo imetoa rambirambi ya Sh10 milioni huku pia ikigharamia taratibu mbalimbali za mazishi yatakayofanyia kesho Ijumaa, Kyela mkoani Mbeya.