Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi Tanzania yapata ushindi Ligi Kuu baada ya siku 1193

POLISI Pict

Muktasari:

  • Siku hizo ni sawa na miaka mitatu, miezi mitatu na siku tano tangu iliposhinda mara ya mwisho Mei 15, 2023 dhidi ya Mtibwa Sugar mabao 3-1.

POLISI Tanzania imepata ushindi katika Ligi Kuu Bara baada ya kupita siku 1193 kufuatia leo Alhamisi Agosti 20, 2026 kuitandika JKT Tanzania mabao 2-0, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Siku hizo ni sawa na miaka mitatu, miezi mitatu na siku tano tangu iliposhinda mara ya mwisho Mei 15, 2023 dhidi ya Mtibwa Sugar mabao 3-1. Hiyo ilikuwa ni msimu wa 2022-2023 ambapo ilishuhudiwa Polisi Tanzania ikishuka daraja, kisha imerejea Ligi Kuu 2026-2027, ikishiriki Ligi ya Championship misimu mitatu ambayo ni 2023-2024 na 2024-2025 na 2025-2026.

Polisi Tanzania ilishuka daraja msimu wa 2022-2023 baada ya kumaliza nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ikishinda mechi sita kati ya 30 na kukusanya pointi 25, wakati huo Ruvu Shooting ilimaliza mkiani na pointi 20.

Polisi Tanzania baada ya kurejea Ligi Kuu Bara, ilianza kampeni yake kwa kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC, kisha leo ikashinda 2-0.

Ushindi huo umeifanya Polisi Tanzania kufikisha pointi nne baada ya mechi mbili, huku pointi zote ikiwa imezikusanya kwenye uwanja wake wa nyumbani. Kikosi hicho kimeonyesha mwanzo wenye matumaini katika harakati zake za kuhakikisha inasalia Ligi Kuu.

Katika mchezo dhidi ya JKT Tanzania, Polisi ilipata bao dakika ya 45+1 kupitia kwa Kenny Ally Mwambungu, aliyeibuka nyota wa mchezo huo.

Mwambungu alipata nafasi hiyo baada ya kupokea pasi kutoka kwa Jamal Mtegeta, ambaye alifanya kazi kubwa ya kuwasumbua na kuwavuruga mabeki wa JKT Tanzania kabla ya mpira kumfikia mfungaji na kuipa Polisi Tanzania uongozi.

Baada ya mapumziko, Polisi Tanzania iliendelea kulisakama lango la JKT Tanzania na dakika ya 64 Habib Kyombo akaandika bao la pili, akimalizia pasi ya Anuary Jabir na kuipa timu hiyo nafasi nzuri ya kulinda ushindi huo hadi filimbi ya mwisho.

JKT Tanzania chini ya kocha Ahmad Ally, imeanza msimu kwa kusuasua baada ya kushindwa kupata ushindi katika mechi zake mbili za mwanzo. Kikosi hicho kilianza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya TRA United nyumbani, kabla ya leo kukutana na kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Polisi Tanzania.