Vyoo Uwanja wa Mkapa hatari tupu

UWANJA wa Benjamini Mkapa una uwezo wa kuingiza mashabiki 60,000 una eneo zuri la kuchezea ‘pitch’, una vyumba vizuri vya kubadilishia nguo wachezaji na waamuzi kwa ufupi huduma zingine ni nzuri na ni miongoni mwa viwanja bora kabisa Afrika.

Lakini tatizo kubwa kwenye uwanja huo ni miundombinu upande wa vyoo vya mashabiki ambavyo kwasasa haviko salama tena, havifai kwa matumizi ya binadamu kutokana na kuharibiwa.

Meneja Uwanja huo uliopo Temeke, Dar es Salaam, Gordon Nsajigwa anasema kuna haja ya wananchi na mashabiki wa michezo wanaotumia vyoo hivyo kupewa elimu juu ya matumizi sahihi ya vyoo .

Kauli ya meneja huyo imekuja baada ya gazeti hili kufanya uchunguzi kwenye vyoo hivyo wakati wa mechi na kukuta vikiwa katika hali isiyoridhisha ikiwa uwanja huo unatajwa kuwa ni moja ya viwanja bora Afrika Mashariki na Kati.

“Changamoto ya vyoo ni kweli tumeiona na sisi kwa kushirikiana na wizara tunajitahidi kuifanyia kazi japo kuwa sehemu kubwa inayohitajika ni wananchi kupewa elimu juu ya matumizi sahihi ya vyoo kwani wengi wamekuwa waharibifu wa miundombinu jambo ambalo limekuwa sugu hususani upande wa vyoo vya wanaume.

“Mashabiki wanang’oa koki za maji mfano uwanja mzima koki zaidi ya 180 zimeibwa katika vyoo na watu wanaofanya matukio hayo wengi ni wanaume kwani muda mwingine wanaingia hadi vyoo vya wanawake na kuiba koki hizo kama wasimamizi tumekuwa tukisikitishwa na vitendo hivyo kwani tunaingia gharama kila mara kufanya matengenezo,” anasema Nsajigwa

Meneja huyo aliongeza mbali na koki kuna ‘footflash’ nazo zimeibiwa katika vyoo hivyo ambazo upatikanaji wake ni adimu ikapelekea wao kupeleka mapipa ya maji ili watu waweze kuchota na kutumia chooni na wengi wanayamwaga ovyo na kupelekea vyoo kuziba.

“Vyoo vinaziba kila inapochezwa mechi kubwa kwani watu wanamwaga maji na takataka nyingine chooni, aidha mashabiki hao wamekuwa wakiwafukuza wafanya usafi wa vyoo hivyo wanapoenda kufanya usafi wakati wa mechi.

Tunatamani tungeweza kuweka mazingira rafiki ya usafi kwa mfano nilienda viwanja vingi vikubwa chooni kuna hadi ‘dryer’za kukaushia nywele na sehemu ya kujipodolea huku kwetu watu wasio waaminifu wanaturudisha nyuma,”

Wakati wa mechi ya Ngao ya Jamii iliyowakutanisha watani wa jadi Simba na Yanga gazeti hili lilishuhudia vyoo vya uwanja huo vikiwa vimejaa uchafu na maji yamejaa jambo linalohatarisha usalama wa afya za watumiaji.

Mbali na uchafu kwenye vyoo hivyo lakini hata milango yake ilikuwa mibovu, maji yalikuwa yamejaa huku takataka nyingine kama vile maganda ya pipi na chupa za maji zikiwa zimetupwa na vinyesi vikiwa juu, jambo linaloweza kusababisha magojwa ya mlipuko.

Mmoja wa watumiaji wa vyoo hivyo, Lilian Mosha anaelezea mazingira hayo: “Ndugu yangu hali ni mbaya afadhali umeona na kuchukua picha maana uchafu umejaa na maji pia yamemwagwa hapa mtu anaweza kuteleza na kuanguka ovyo akaumia, tunaomba mamlaka zichukue hatua za haraka kunusuru hali hii kwani ni mbaya sana”

Kwa wa upande wa vyoo vya wanaume nako hali si salama kwani sehemu za kukojolea mkojo huwa zinajaa mikojo, huenda bomba zinazotiririsha mikojo zinaziba au ndogo kuliko mahitaji.

Sio sehemu za kukojolea tu, bali hata kwenye ‘masinki’ ya kujisaidia hali si shwari kwani yanakuwa yamejaa uchafu muda wote.

Mmoja wa watumiaji wa vyoo hivyo, Juma Ismail anasema kuwa; “Watanzania tuna uwanja mzuri ila hauna miundombinu rafiki ndugu mwandishi angalia vyoo vilivyojaa na pia hakuna koki za maji ni aibu kubwa kwani watazamaji wengine wanakuja kutoka nchi mbalimbali wakiona hali ya vyoo wanajisikia kinyaa kwani wanaweza kupata magojwa ya kuambukizwa”.