Vijue vigezo vya chini vya leseni za klabu
LESENI ya Klabu, kwa kimombo Club Licensing na mfumo wake ni zao la mkutano wa 57 wa Shirikisho la Soka duniani (Fifa) uliofanyika mwaka 2007 pale Munich, Ujerumani.
Ingawa kuna dhana pia kwamba, Shirikisho la Soka barani Ulaya (Uefa) walikuwa tayari wameanza kupiga hatua katika hili, Fifa ni kama waliurasimisha moja kwa moja mfumo huu.
Kwa mfano, Oktoba 29, 2007 Kamati ya Utendaji ya Fifa ilipitisha kanuni za leseni kwa klabu zilizoanza kufanya kazi Januari 1, 2008.
Kwa ujumla ni kwamba, kanuni hizi ni kama nyaraka kazi kwa ajili ya mashirikisho na vyama vya soka katika bara na nchi husika.
Ninapoisoma Ibara ya 1(1) ninaona malengo ya kuanzishwa kwa mfumo huu katika soka.
Moja ya malengo hayo ni kulinda uaminifu na uadilifu wa mashindano ya vilabu, kuongeza kiwango cha weledi katika familia ya mpira wa miguu.
Malengo mengine ni kukuza maadili ya mchezo kulingana na kanuni za haki na pia mazingira salama ya mechi.
Vilevile ni kukuza uwazi katika fedha za klabu, kukuza uwazi katika umiliki wa vilabu, na kukuza uwazi katika kudhibiti vilabu. Utekelezaji wa kanuni hizi unatakiwa kuanzia kwenye mashirikisho ya soka katika bara husika kabla ya kutumiwa katika vyama vya soka katika nchi wanachama.
Kwa mujibu wa kanuni hizi za Fifa, utekelezaji huu kwa mashirikisho ulitakiwa uwe umefanyika kwa kuwa na kanuni zake kwa msimu wa 2009/2010.
Hapa ni msimu mmoja kabla ya kuanza kutumiwa katika vyama vya soka mwanachama, ingawa kwa kuwa pia na kanuni zake zenye maudhui haya.
Hivi ndivyo ninavyoielewa Ibara za 2 (2) na 11 za kanuni hizo za Fifa.
Kwa taarifa yako ni kwamba, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) lilipitisha kanuni zake za leseni za klabu mnamo Januari 19, 2012 ambazo zilianza kufanya kazi Machi 1, 2012.
Pamoja na hayo ninavyoziona Ibara za 15(g) na 23(g) za Sheria ya Fifa (The Fifa Statutes) toleo la 2018, Ibara za 7(1)(f) na 53 ya Sheria ya Caf (The Caf Statutes) toleo la 2017 ninapata faraja kubwa.
Hivyohivyo kwa Ibara ya 66 ya Katiba ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) toleo la 2019 na kanuni ya 11 ya Kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara toleo la 2018, maana ni msingi bora kabisa wa kutekeleza misingi ya mfumo wa leseni za vilabu. Hoja kuu katika Makala hii ni je, vigezo vipi vya chini katika Mfumo wa Leseni ya Klabu (Club Licensing System) ili kukidhi hadhi za kimashindano ya ndani na yale ya kimataifa?
Mosi, ni kigezo cha mchezo
Katika kigezo hiki kinahitaji kila klabu mathalani zinazoshiriki ligi ya TFF na CAF kuwa na mpango bora wa maendeleo ya soka la vijana. Hapa ninamaanisha walau timu moja ya vijana kati ya miaka 15-21, na nyingine kati ya miaka 10-14.
Hapa klabu haitakiwi kusahau kuwekeza pia katika elimu ya mpira na isiyo ya mpira lakini halali kisheria, na katika afya zao. Moja ya faida ya kigezo hiki ni kupata wachezaji wa kuwapandisha timu ya wakubwa, na pia kupata fidia (compensation) ya kuwapa mafunzo wachezaji walio chini ya miaka 23 endapo watasajiliwa na timu ya kigeni.
Pili, kigezo cha miundombinu
Kigezo hiki huenda ni moja ya vigezo vigumu sana kutekelezeka kwa klabu nyingi hasa za Bara la Afrika. Timu zinatakiwa kuwa na kiwanja salama cha mazoezi na mechi za mashindano kwa mechi za nyumbani, bila kusahau vifaa bora vya mazoezi. Uzoefu katika hili ni kwamba, klabu nyingi hasa za ulimwengu wa tatu na chache kwenye nchi zilizoendelea hazimiliki viwanja. Maana yake ni kwamba huwa zinatakiwa tu walau kupeleka mkataba au kibali cha kutumia uwanja kutoka kwa wamiliki ili zipewe leseni.
Katika kiwanja hasa cha mechi, huwezi kuacha kuzungumzia ubora wa uzio, vyumba vya kubadilishia nguo, majukwaa kwa ajili ya mashabiki na pia miundombinu kwa ajili ya waandishi wa habari.
Zaidi ya hivyo, kunatakiwa kuwe na miundombinu bora ya vyoo, sehemu za kupaki magari yakiwemo yale ya huduma ya kwanza na dharula. Pia, kiwanja kinatakiwa kiwe sehemu rahisi kwa ajili ya kufika hospitali ikiwa itabidi kufanya hivyo.
Tatu, wafanyakazi na watawala
Ili klabu ziishi katika weledi, hakuna ubishi kwamba zinatakiwa kuwapa nafasi wasomi wa taaluma mbalimbali.
Uzuri ni kwamba hiki ni kigezo cha lazima katika sheria za FIFA, CAF na pia TFF, na kwamba siyo lazima kwamba mtu awe amewahi kucheza soka peke yake. Timu inahitaji kuajiri wataalamu wa benchi la ufundi, sheria, tiba, fedha, masoko, habari na mahusiano ya umma, burudani na kadhalika. Pia timu iwe na sehemu ya wao kufanyia kazi zao.
Ukishakuwa na wataalamu wa aina hii bila kuingilia majukumu yao, ni rahisi kuona matokeo chanya ndani na nje ya uwanja.
Hivi unafahamu kwamba klabu ni taasisi kubwa zinazoingiza fedha nyingi kupitia shughuli zake, kupitia wadhamini na pia matangazo ya runinga?
Ndiyo maana ya kuwa na watu wenye weledi mkubwa kufanikisha haya na kuzifanya klabu kukua kisoka na kiuchumi pia. Ngoja nikupe mfano hai. Unamkumbuka Peter Kenyon kwa kazi alizowahi kufanya Manchester United na baadaye Chelsea kama Mtendaji Mkuu wa Klabu?
Ni rahisi RB Leipzig kuuelewa mchango wa Ralf Rangnick katika nafasi ya Ukurugenzi wa Soka. Ndiyo maana licha ya kwamba aliondoka, wamefika nusu fainali ya Klabu Bingwa Ulaya ndani ya miaka 11 tu tokea kuanzishwa kwake
Hapa sijawataja kina Giuseppe Marotta wa Juventus, Txiki Begiristain wa Manchester City, au Michael Zorc wa Borussia Dortmund.
Nne, ni kigezo cha kisheria
Kigezo hiki ni nyeti sana maana kinadhibiti uadilifu na uaminifu katika soka.
Kila klabu inatakiwa kuwajibika kwenye sheria, kanuni na maamuzi mbalimbali ya FIFA, CAF, na vyama vya soka katika nchi husika. Hapa kigezo hiki kinaangalia vyema umikili na udhibiti wa vilabu.
Pia kinadhibiti mtu kati (third party) kuingilia mambo ya klabu, na kudhibiti mtu au taasisi moja kumiliki klabu zaidi ya moja na kushiriki katika shindano moja. Ni lazima kuwe na muundo wa wazi wa umiliki na udhibiti wa kila klabu chini ya kanuni hizi.
Tano, ni kigezo cha kifedha
Hiki ni moja ya kigezo nyeti sana maana fedha zimekuwa na ushawishi mkubwa sana katika soka.
Klabu inaweza kuwa inapata fedha zisizokuwa halali kutoka sehemu nyingine, au kujihusisha kashfa za kupanga matokeo kwa sababu ya kifedha. Kanuni zinataka vyama vya nchi wanachama kuweka utaratibu wa wazi kwa vilabu ikiwemo kuwa na taarifa za kifedha.
Lengo la kufanya hivi ni kuchochea uchumi wa klabu, kuleta uwazi na uaminifu na pia kulinda maslahi ya wadai na wadau.
Mwisho, vyama vya soka katika nchi husika na pia mashirikisho ya soka kama vile CAF vimepewa meno ya kutotoa leseni kwa klabu ambazo hazijatimiza vigezo hivyo. Maana yake ni kwamba klabu hizo hazitakuwa na sifa ya kushiriki mashindano yanayoratibiwa na vyama hivyo. Ikiwa itagundulika kwamba, chama cha soka kilitoa leseni bila kufuata vigezo kinaweza kupewa adhabu na Fifa hasa baada ya Shirikisho katika Bara husika kushindwa kutoa adhabu. Usikose kusoma namna mfumo wa leseni kwa klabu unavyofanya kazi Tanzania katika gazeti la Mwanaspoti kesho, Alhamisi.Nakutakia Tafakuri Njema.
Kasanda Mitungo ni wakili wa Mahakama Kuu na pia mwandishi wa masuala ya kisheria, kijamii na siasa za kimataifa. Anapatikana kwa simu: 0712 786 051; barua pepe: [email protected]