Mo Dewji atenga Sh30 bilioni Simba akiahidi kujenga uwanja
Muktasari:
- Mo Dewji ametoa kauli hiyo leo Agosti 8, 2026 kwenye kilele cha Simba Day, akieleza kuwa mpango huo unalenga kuifanya Simba kuwa na miundombinu ya kisasa itakayosaidia klabu hiyo katika maendeleo ya timu zake na programu za vijana.
MWEKEZAJI wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’, ameweka wazi mpango wa uwekezaji wa takribani Sh30 bilioni klabuni hapo, akiahidi kujenga uwanja wa mechi pamoja na viwanja sita vya mazoezi kwa ajili ya timu za Simba, Simba Queens, vijana na kuboresha miundombinu ya klabu.
Mo Dewji ametoa kauli hiyo leo Agosti 8, 2026 kwenye kilele cha Simba Day, akieleza kuwa mpango huo unalenga kuifanya Simba kuwa na miundombinu ya kisasa itakayosaidia klabu hiyo katika maendeleo ya timu zake na programu za vijana.
“Ninaahidi kuwa nitajenga uwanja na viwanja sita vya mazoezi kwa ajili ya Simba, Simba Queens, Simba vijana na vituo vya mazoezi ya ndani vya kisasa, yaani gym, vituo vya kupatia nafuu kama recovery, kambi ya malazi, ofisi za kisasa na uendeshaji na usimamizi,” amesema Mo Dewji.
Mo amesema uwekezaji huo unalenga pia kuweka msingi imara wa programu ya vijana ndani ya Simba, huku akisisitiza umuhimu wa klabu kuwa na mfumo wa kulea vipaji.
Mwekezaji huyo amesema tayari amepeleka pendekezo la uwekezaji huo kwenye Bodi ya Wadhamini ya Simba na sasa anasubiri majibu ili kuanza utekelezaji.
“Nimeweka mezani pendekezo la uwekezaji wa takribani bilioni 30, nimeifikisha kwa Bodi ya Wadhamini ya Simba na nasubiri majibu yao. Mimi niko tayari hata kesho kwa ajili ya ujenzi na wadhamini wenyewe wako hapa hapa,” amesema.
Mpango huo ukitekelezwa utakuwa miongoni mwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu katika historia ya Simba, ukiwa na lengo la kuipa klabu mazingira bora ya mazoezi, maandalizi ya timu, malezi ya vijana na maendeleo ya soka la wanawake.