Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vijue Vifungu vya Mkataba Bora kwa Mchezaji

MKATABA ni makubaliano huru, yenye masilahi baina ya watu wenye uwezo kisheria na yanatekelezeka kisheria.

Mikataba baina ya wachezaji na klabu inatakiwa kuwa ya maandishi na siyo vinginevyo.

Hapa ndipo suala la kusajiliwa kwenye shirikisho la soka katika nchi husika linapokuja.

Hivi ndivyo ninavyokumbuka mathalani kanuni ya 70(8) ya Kanuni za Ligi Kuu ya Tanzania Bara toleo la 2018.

Hivi ndivyo ninaelewa mahitaji ya mfumo wa mtandao yaani FIFA Transfer Matching System (TMS) hasa kwa wachezaji wa kimataifa kwa mujibu wa Kanuni za Uhamisho na Hali za Wachezaji Toleo la Juni, 2020.

Mkataba mzuri unatakiwa kuwa na vifungu (clauses) vifuatavyo kwa ajili ya kulinda masilahi ya pande zote mbili:

Mosi, kifungu tafsiri.

Faida ya kuwa na kifungu hiki ni kuondoa utata wa tafsiri ya misamiati baina ya pande mbili kwenye mkataba. Moja ya misamiati muhimu, ni Wakala, Klabu, Shirikisho la Mpira wa nchi, FIFA, Maadili ya Klabu, Makosa ya kinidhamu, Likizo, Ligi, Majeraha, Picha za mchezaji na kadhalika.

Pili, Muda wa Mkataba.

Hiki ni kifungu muhimu kuonyesha lini mkataba umesainiwa, umeanza kutekelezwa na lini utafikia mwisho.

Tatu, wajibu na Majukumu ya mchezaji.

Hapa ni pamoja na kuhudhuria mazoezi ya timu kwa wakati mwafaka, kuhudhuria mechi na kucheza pale ambapo amepangwa na kuwa na nidhamu ndani na nje ya mchezo wakati wote.

Majukumu kama haya anatakiwa ayafanye kwa kiwango kinachokubalika na timu yake labda tu pale amethibitishwa kuumwa au ana majeraha kwa mujibu wa daktari wa timu.

Nne, kushiriki shughuli za klabu katika mahusiano ya Umma na masoko.

Lazima itambulike mchezaji ni mali halali ya klabu, hivyo ni muhimu zaidi kushiriki kwenye shughuli zake zingine, zinazoitangaza klabu kupitia wadhamini wake.

Mchezaji hasa wa kulipwa anapokuwa kwenye shughuli za klabu yake hatakiwi kuvaa nguo au kutumia vifaa vya kampuni nyingine ambazo siyo wadhamini wa klabu ili kulinda masilahi ya klabu kibiashara.

Tano, ni kifungu cha malipo na gharama.

Katika kifungu hiki ni lazima tuonyeshwe kiwango kinachokubalika cha mshahara na malipo mengine ya ziada (bonus) kulingana na sera ya klabu.

Vilevile, tunategemea kuona gharama za kambi au mechi zikilipwa na klabu na endapo mchezaji ametumia gharama zake kuwe na utaratibu wa kumfidia.

Endapo mchezaji ametiwa hatiani kwa utovu wa nidhamu au kuisababishia hasara klabu, faini ni muhimu zikawepo katika kifungu hiki ili kulinda hadhi ya klabu.

Sita, kwa kuwa mkataba una pande mbili, ni muhimu kuwepo kwa majukumu ya klabu kwa mchezaji.

Katika kifungu hiki, klabu lazima impatie sera na kanuni mchezaji mara kwa mara, pia mkataba.

Pia, klabu inatakiwa kuwatibu wachezaji wake wanapopata majeraha, au kuumwa. Ni muhimu kila klabu kuwa na sera ya afya na bima inayotekelezeka kwa manufaa ya wachezaji.

Klabu ina wajibu wa kuwa na mazingira salama ya wachezaji kucheza soka, siyo hatarishi.

Klabu haitakiwi kumnyima fursa mchezaji ikiwa anataka kujiendeleza kielimu. Hapa ni lazima kuwe na mazingira rafiki ya kimkataba ya kutekeleza hilo.

Ni lazima ifahamike pia, klabu haitakiwi kumkataza mchezaji kuitumikia timu yake ya Taifa pale anapoitwa.

Ikumbukwe zaidi, klabu haitakiwi kutumia picha za mchezaji kinyume na shughuli za kawaida za klabu na mdhamini.

Pia, klabu haitakiwi kutoa siri za vipimo vya afya vya mchezaji kwa Umma bila ridhaa yake, isipokuwa taarifa za utimamu wa mwili wake baada ya kupata majeraha.

Saba, ni kifungu cha Majeraha na Ugonjwa.

Katika kifungu hiki ni lazima mkataba ueleze ni namna gani mchezaji atatoa taarifa za ugonjwa wake kwa klabu.

Vilevile, ni lazima kifungu hiki kitueleze ni namna gani malipo yatakuwa yanafanyika kwa mchezaji ambaye ana majeraha au yule ambaye hawezi tena kucheza kutokana na maumivu ya kimwili na kiakili baada ya kuitumikia klabu.

Nane, lazima mkataba huu uwe na kifungu kinachoonyesha mchezaji kushindwa kabisa kucheza kutokana na majeraha ya kudumu.

Hapa ni lazima tuone Ilani ya kuachana naye ndani ya mkataba na kwa namna gani, na pia lazima kuwe na muda maalumu wa Ilani hiyo.

Tisa, kifungu cha utaratibu wa kinidhamu.

Mchezaji anapotuhumiwa kukiuka maadili, atapata muda mzuri zaidi wa kujiandaa kujibu mashtaka yake na pengine kutafuta Wakili wake.

Kumi, kifungu cha kumuacha mchezaji kimkataba.

Hapa endapo kuna hoja ya kinidhamu, au masuala mengine ya kimkataba, na kifungu hiki lazima kiweke muda maalumu wa Ilani kutolewa kwa mchezaji.

Kumi na moja, kifungu cha mchezaji kuvunja mkataba na klabu yake.

Mchezaji ana haki ya kuvunja mkataba na klabu yake ikiwa imeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa mchezaji ikiwemo kulipa mshahara na stahiki zake zingine zilizopo kwenye mkataba.

Kitu kinachotakiwa kufanyika ni kutoa Ilani ya kufanya hivyo na kama ilivyo kwa utamaduni wa nchi nyingi Ilani ya namna hii na ile ya timu kwa mchezaji huwa ni kuanzia siku 14.

Kumi na mbili, ni kifungu cha utaratibu wa kulalamika.

Mkataba unatakiwa umpe utaratibu mchezaji kulalamika ndani ya klabu yake kuhusu mkataba pengine kabla ya kwenda kwenye vyombo vya nje.

Kumi na tatu, kifungu cha uwakilishi wa mchezaji.

Katika kifungu hiki, mchezaji lazima apewe haki ya kuwa kilishwa katika mambo yake ya kimkataba ndani na nje ya klabu.

Hapa anaweza kuwakilishwa na nahodha wa timu, chama cha wachezaji wa kulipwa, au mwanasheria wake.

Kumi na nne, kifungu cha likizo kwa mchezaji.

Mchezaji ni sawa na wafanyakazi wengine, wanahitaji kupumzika.

Kwa utamaduni wa nchi nyingi katika soka, inashauriwa walau wiki tano za malipo kwa mwaka na wiki tatu ni mfululizo.

Kumi na tano, kifungu cha uhai wa mkataba.

Hiki ni muhimu maana upande ambao utakuwa hautekelezi majukumu yake, utaupa faida upande unaotekeleza.

Kumi na sita, kifungu cha usiri.

Hiki ni moja ya vifungu nyeti kwenye mkataba wowote ukiwemo wa soka.

Baada ya kufanyika kwa mkataba kila upande utalazimika kutunza siri za mkataba na kutovujisha kwa upande wa tatu usiohusika bila ridhaa ya mwingine, au bila matakwa ya sheria.

Kumi na saba ni kifungu cha Usuluhishi.

Hiki ni muhimu pale ambapo kunatokea mgogoro baina ya mchezaji na klabu yake. Hapa ni kulingana na makubaliano baina ya mchezaji na klabu, pia kwa mujibu wa Kanuni za Ligi husika.

Kumi na nane, kifungu kinachoonesha mkataba huo ni kwa ajili ya ajira ya kucheza soka.

Umuhimu wa kifungu hiki ni, unarahisisha kulinda haki za klabu na mchezaji katika mamlaka ya soka na siyo za kiraia, licha ya kuwepo kwa kifungu cha mamlaka.

Kumi na tisa, ni kifungu cha malipo ya kumaliza au kusitishwa kwa mkataba.

Malipo haya ni katika mazingira ambayo klabu imevunja mkataba bila utaratibu na mchezaji hajapeleka malalamiko yoyote katika vyombo vinavyohusika au amenyimwa mkataba mpya.

Ishirini, ni kifungu kinachokiri kufanyika kwa mkataba huo na kufuta yote ikiwa imefanyika awali na idadi ya nyaraka za mkataba huo.

Mwisho, ni kifungu kinachohusu Mamlaka na Sheria.

Hiki kinaonyesha mamlaka na sheria zipi zitatumika kutafsiri mkataba ulioingiwa na pande zote mbili, endapo kutakuwa na mgogoro.

Ninakutakia Tafakuri Njema.

Kasanda Mitungo, ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, pia Mwandishi wa masuala ya Kisheria, Kijamii, na Siasa za Kimataifa, anapatikana kupitia:

Simu: +255 712 786 051; Barua pepe: [email protected]