Vijana hawakufuata maelekezo

Muktasari:

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20 'Ngorongoro Heroes', Jamhuri Kihwelu 'Julio' amesema kukosa kwao ubingwa kwenye fainali ya Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ni wachezaji wake kutofuata maelekezo yake.

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20 'Ngorongoro Heroes', Jamhuri Kihwelu 'Julio' amesema kukosa kwao ubingwa kwenye fainali ya Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ni wachezaji wake kutofuata maelekezo yake.

Wakati Julio akiyasema hayo nyota wawili wa Ngorongoro Herous, Abdul Hamis Suleiman  na Paschal Mshindo waliibuka vinara wa mashindano hayo.

Mshindo amekuwa Mchezaji Bora wakati Suleiman  ni Mfungaji Bora baada ya kufunga mabao matano sambamba na mshambuliaji wa Uganda, Ivan Bogere.

Julio aliyasema hayo mara baada ya fainali hiyo kumalizika ambapo Uganda walitwaa ubingwa huo baada ya kushinda bao 4-1, mechi hiyo imechezwa Uwanja wa Kituo cha Black Rhino wilayani Karatu mkoani Arusha.

"Kipindi cha kwanza vijana walicheza vizuri kwa kufuata maelekezo lakini kipindi cha pili haikua hivyo ndio maana tukafungwa bao nyingi.

"Haya ni mambo ya mpira lolote hutokea hivyo nimekubali matokeo na nina wapongeza Uganda kuchukua ubingwa kwetu kwani hata sisi msimu uliopita tulichukua tukiwa kwao," amesema Julio

Kocha wa Uganda, Byekwaso Mchama alizungumzia ubingwa huo na mchezo mzima kwa ujumla.

"Nashukuru kubeba ubingwa, mchezo ulikua mzuri na Tanzania walikua bora lakini nawapongeza vijana wangu wamecheza kwa kujituma na kufuata maelekezo na hatimaye tumepata ushindi uliotufanya kuwa mabingwa," amesema Mchama.

xxxxx