Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

BADO MBILI LIGI KUU!

Muktasari:

Kumalizika kwa mechi hiyo ambayo siku zote zinapokutana timu kongwe za soka hapa nchini haijawahi kuwa rahisi, kunaashiria kipute cha mashindano ya Ligi Kuu Bara yanaanza rasmi ambapo Ijumaa hii zitapigwa mechi tatu.

BILA shaka ulishuhudia ushindani wa Yanga na Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii, iliyoashiria kufunguliwa kwa msimu wa mashindano yanayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) 2026-2027.

Kumalizika kwa mechi hiyo ambayo siku zote zinapokutana timu kongwe za soka hapa nchini haijawahi kuwa rahisi, kunaashiria kipute cha mashindano ya Ligi Kuu Bara yanaanza rasmi ambapo Ijumaa hii zitapigwa mechi tatu.

Lakini dabi hiyo ni ya kwanza kwa vigogo hao kwa msimu wa 2026-2027, kuna zingine mbili zipo zinawasubiri kwenye Ligi Kuu ambapo itachezwa Oktoba 10, 2026 Simba ikiwa mwenyeji, kisha Yanga itakuwa mwenyeji Februari 6, 2027.

Mbali na dabi hizo mbili zinazosubiriwa kuona nani ataibuka na kicheko baada ya hapo jana, pia timu hizo zinakabiliwa na ratiba ngumu ya mechi 13 kila moja kuelekea safari yao ya kuisaka hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2026-2027 ambapo msimu uliopita hapo kilikuwa kituo chao baada ya zote kushindwa kufuzu robo fainali.

Si Simba na Yanga pekee, bali Azam na Singida Black Stars zinazoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika, nazo zipo katika mitihani miwili, kukusanya pointi za kuwaweka sehemu nzuri kwenye msimamo wa ligi, pia hesabu za kucheza tena makundi CAF baada ya msimu uliopita zote kuweka historia.

Kuanzia Agosti 14 hadi Oktoba 25 ambapo ni kipindi cha takribani siku 72 sawa na miezi miwili na siku 11 au wiki 10 na siku mbili, ratiba za wawakilishi hao wa Tanzania kimataifa inaonyesha kila timu ina mtego wake, lakini pia kuna timu yenye unafuu mkubwa kuliko nyingine.

Kwa idadi ya mechi, Simba, Yanga na Singida zitacheza mechi 13 katika kipindi hicho, wakati Azam itakuwa na mechi 11 kutokana na kutoshiriki raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Huu ni mtihani wa makocha wote kwani atakayezingua, kuna uwezekano wa kibarua chake kusitishwa kwani imekuwa ni kama kawaida kwa klabu kushindwa kufikia malengo, inavunja benchi la ufundi.

Makocha wa timu hizo, Steve Barker (Simba), Manqoba Mngqithi (Yanga), Florent Ibenge (Azam) na Papy Kimoto (Singida Black Stars), kazi kwao.


SIMBA

Simba ndiyo moja ya timu zinazokabiliwa na ratiba yenye msongamano mkubwa.

Wekundu wa Msimbazi wataanza msimu kwa kucheza mechi tatu mfululizo ugenini.

Agosti 16 watakuwa Kaitaba dhidi ya Kagera Sugar, Agosti 19 wataelekea Mwanza kucheza na Pamba Jiji, kabla ya Agosti 22 kwenda Singida kukabiliana na Singida Black Stars.

Huo ni mwanzo unaoweza kuwalazimisha makocha kutumia nguvu nyingi za kikosi mapema.

Baada ya hapo Simba itapata nafuu kidogo kwa kucheza mechi mbili nyumbani dhidi ya Coastal Union (Agosti 27) na Geita Gold (Agosti 31). Lakini Septemba ndiyo changamoto kubwa inaanza.

Kati ya Septemba 4-6, Simba itakuwa Malawi kucheza na Mighty Wanderers katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza.

Septemba 9, siku chache baadaye, itarudi Tanzania kucheza na Azam FC kwenye Azam Complex. Kisha Septemba 11-13 itakuwa tena uwanjani kwa mchezo wa marudiano dhidi ya Mighty Wanderers.

Hapa Simba inakabiliwa na mechi tatu ndani ya siku chache, huku mbili zikiwa za kimataifa na moja ikiwa dhidi ya mpinzani mkubwa wa ligi. Mtego mwingine unakuja Oktoba.

Oktoba 10, Simba itakutana na Yanga katika Dabi ya Kariakoo, kabla ya kucheza na Mashujaa Oktoba 13.

Kisha kati ya Oktoba 16-18 kama itakuwa imevuka hatua ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, basi itasafiri kwenda kukutana na mshindi kati ya 15 de Agosto na Fomboni katika hatua ya pili ya CAF.

Kwa Simba, ratiba hii inaonekana kuwa ya ugumu mkubwa, hasa kutokana na safari ya kutoka kituo kimoja kwenda kingine, mechi za CAF na Dabi ya Kariakoo.

Faida yake kubwa ni kwamba, mechi mbili za mwisho za hatua hiyo zitachezwa nyumbani, jambo linaloweza kupunguza mzigo wa safari kwani kabla ya mchezo wa marudiano wa CAF, ina ratiba ya kuikaribisha Mbeya City.


YANGA

Yanga imepata mwanzo unaoonekana kuwa rafiki zaidi kwenye ligi kwani baada ya safari ya Lindi Agosti 15 kucheza na Namungo, Wananchi watacheza mechi tatu mfululizo nyumbani dhidi ya Coastal Union, JKT Tanzania na Pamba Jiji.

Hii ni nafasi nzuri ya kukusanya pointi kabla ya kuanza msururu wa safari za kimataifa.

Lakini Septemba Mosi, Yanga itasafiri kwenda Arusha kucheza na Fountain Gate. Siku chache baadaye, kati ya Septemba 4-6, itakuwa Botswana dhidi ya Gaborone United.

Baada ya kurudi Tanzania, Yanga itaikaribisha Geita Gold Septemba 8, kabla ya kukutana tena na Gaborone United katika marudiano kati ya Septemba 11-13. Hii ndiyo sehemu ambayo ratiba yake inaanza kuwa ngumu.

Katika kipindi kifupi, Yanga itakuwa imesafiri Arusha, Botswana na kurejea Tanzania huku ikiendelea kucheza mechi za ligi na CAF.

Kisha Oktoba 10 kuna dabi dhidi ya Simba. Siku tatu baadaye, Yanga itakuwa ugenini dhidi ya TRA United, kabla ya kuanza hatua ya pili ya CAF kati ya Oktoba 16-18 endapo itakuwa imefuzu.


AZAM

Kwenye karatasi, Azam ndiyo timu yenye ratiba yenye unafuu mkubwa zaidi. Sababu kubwa ni moja, timu hiyo haina ratiba ya kucheza mechi ya CAF mwezi Septemba kufuatia kuanzia hatua ya pili.

Wakati Simba, Yanga na Singida zitakuwa zikizunguka Afrika, Azam itakuwa ikicheza ligi pekee. Mchezo wake wa kwanza ni Agosti 15 dhidi ya Polisi Tanzania jijini Arusha.

Baada ya hapo itacheza nyumbani dhidi ya TRA United na Pamba Jiji nyumbani, kabla ya kusafiri Geita na Kagera Sugar.

Hadi Agosti 31, Azam itakuwa imecheza mechi tano. Mbili nyumbani na tatu ugenini.

Kisha Septemba 9 itacheza mchezo mkubwa dhidi ya Simba. Baada ya hapo, Azam haitakuwa na mechi ya CAF hadi Oktoba.

Hii inaipa Azam nafasi ya kutumia Septemba kuvuna pointi za ligi na kujiandaa kwa hatua ya kimataifa. Lakini Oktoba, ina mtego.

Ratiba inaonyesha Oktoba 8, Azam itacheza na Coastal Union mkoani Tanga, Oktoba 12 itaikaribisha Namungo, kisha Oktoba 16-18 itaingia kwenye hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Iwapo mpinzani wao atakuwa ZED FC ya Misri, safari hiyo inaweza kuwa ndefu na yenye changamoto, lakini kama ikiwa dhidi ya ASAS, inaweza kuwa nafuu kidogo kukabiliana na vijana hao kutoka Djibouti.

Pamoja na hayo, kwa kulinganisha na wapinzani wake watatu, Azam ndiyo yenye ratiba inayoweza kutajwa kuwa nyepesi zaidi katika kipindi cha mwanzo.


SINGIDA

Singida Black Stars ndiyo timu inayokabiliwa na changamoto kubwa zaidi katika suala la uzoefu. Msimu huu inashiriki mashindano ya CAF kwa msimu wa pili mfululizo, jambo ambalo ni hatua kubwa kwa klabu hiyo, lakini ratiba yake inaonyesha haitakuwa safari rahisi.

Singida inaanza ligi Agosti 14 kwa mchezo wa nyumbani dhidi ya Fountain Gate.

Agosti 19 itakwenda Kagera, kabla ya kurejea nyumbani kucheza na Simba Agosti 22. Baada ya hapo, itacheza na Polisi Tanzania na Namungo nyumbani.

Hapo inaonekana kuwa na faida kubwa kwa sababu ya idadi ya mechi za nyumbani. Lakini Septemba ndiyo inabadilisha kila kitu.

Septemba Mosi itacheza na Namungo nyumbani, kisha kati ya Septemba 4-6 itasafiri kwenda Sudan Kusini kucheza na Al-Ghazala Wau.

Septemba 8, siku chache baadaye, itakuwa Kigoma dhidi ya Mashujaa FC. Kisha Septemba 11-13 itarejea Singida kwa mchezo wa marudiano wa CAF.

Huo ni msururu unaohitaji kikosi kipana na maandalizi makubwa. Oktoba nayo haina nafuu. Mwezi huo unaanza kwa safari za ligi, itakwenda Dodoma Oktoba 9 na Tanga Oktoba 12, kabla ya kuanza hatua ya pili ya CAF nyumbani, Oktoba 16-18 endapo itakuwa imefuzu.


NANI ANA RATIBA NGUMU ZAIDI?

Kwa kuangalia mambo matatu ambayo ni idadi ya mechi, safari na ukaribu wa mechi za ligi na CAF, Simba na Singida zinaonekana kuwa kwenye upande mgumu zaidi.

Simba ina mechi 13 na inakabiliwa na safari za Kanda ya Ziwa, Malawi, dabi dhidi ya Yanga na Azam, pamoja na safari ya hatua ya pili ya CAF. Yanga pia ina mechi 13, lakini imeanza kwa faida ya kucheza mechi nyingi nyumbani.

Singida nayo ina mechi 13, huku ikiwa na changamoto kubwa ya kuzoea ushindani wa CAF.

Azam, kwa upande mwingine, ina mechi 11 pekee katika kipindi hicho na ina nafasi ya kupumua zaidi kabla ya kuanza kampeni yake ya CAF Oktoba.


MECHI ZA NYUMBANI NANI ANA FAIDA?

Katika mechi za mwanzo, Yanga na Singida zinaonekana kuwa na faida kubwa nyumbani.

Yanga itacheza Coastal Union, JKT Tanzania na Pamba Jiji mfululizo nyumbani baada ya mchezo wake wa kwanza dhidi ya Namungo ugenini.

Singida nayo ina mechi nyingi za mwanzo kwenye Uwanja wa Airtel, ikiwamo dhidi ya Fountain Gate, Simba, Polisi Tanzania na Namungo.

Azam pia ina faida ya kucheza TRA United, Pamba Jiji, Simba na Namungo nyumbani.

Simba, tofauti na wenzake, inaanza kwa safari tatu mfululizo ugenini. Hivyo, kwa mwanzo wa ligi, Simba ndiyo yenye ratiba inayohitaji nguvu zaidi.


MTEGO WA OKTOBA

Oktoba ndiyo mwezi ambao makocha wa timu zote nne wanaweza kuanza kuonyesha uwezo wao wa kupanga vikosi.

Simba na Yanga zitakutana Oktoba 10 katika Dabi ya Kariakoo.

Siku tatu baadaye, Simba itacheza na Mashujaa, huku Yanga ikicheza na TRA United.

Azam nayo itacheza na Namungo Oktoba 12. Singida itakuwa imecheza na Dodoma Jiji Oktoba 9 na Coastal Union Oktoba 12.

Kisha kuna mechi za CAF zitaingia kati ya Oktoba 16-18 zikihusisha timu zote.

Kwa hiyo, timu zote nne zitakuwa zinakabiliwa na mbio za ligi na CAF kwa wakati mmoja. Kumbuka baada ya zote msimu uliopita kukwama hatua ya makundi, safari hii zinatazama mbali zaidi.


NANI ANAWEZA KUCHOMOKA SALAMA?

Kwa mtazamo wa ratiba pekee, Azam inaonekana kuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuanza msimu bila mzigo mkubwa, kutokana na kutocheza raundi ya kwanza ya CAF.

Yanga ina nafasi ya pili kwa upande wa unafuu kutokana na idadi ya mechi za nyumbani mwanzoni, ingawa safari za Botswana na Dabi ya Kariakoo vinaweza kubadili picha.

Simba iko kwenye mazingira magumu zaidi kutokana na kuanza kwa safari tatu mfululizo, mechi ya CAF nchini Malawi, dabi mbili dhidi ya Azam na Yanga. Singida nayo ina mtihani mkubwa wa kuzikabili mechi za ligi na CAF kwa wakati mmoja, huku ikiwa na safari za Kagera, Sudan Kusini, Kigoma, Dodoma na Tanga. Lakini ratiba si matokeo.

Timu yenye ratiba ngumu inaweza kufanya vizuri ikiwa ina kikosi kipana, wakati timu yenye ratiba nyepesi inaweza kujikwaa ikiwa itashindwa kutumia nafasi zake.