Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kangwanda afichua siri ya bao la ushindi dhidi ya Simba

Muktasari:

  • Mzaliwa huyo wa Luanshya nchini Zambia, amefunga bao hilo dakika ya 31 kwa kichwa baada ya Boka kupiga krosi kutokea upande wa kushoto na kumfanya kipa Mahamadou Kassali akibaki hawezi kuokoa.

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga SC, Albert Kangwanda, amefichua siri ya bao lake lililoipa timu hiyo ushindi wa 1-0 dhidi ya Simba katika mchezo wa Ngao ya Jamii, akisema maagizo ya kocha ndiyo yaliyomsaidia kufika eneo sahihi na kuunganisha krosi ya Chadrack Boka.

Mzaliwa huyo wa Luanshya nchini Zambia, amefunga bao hilo dakika ya 31 kwa kichwa baada ya Boka kupiga krosi kutokea upande wa kushoto na kumfanya kipa Mahamadou Kassali akibaki hawezi kuokoa.

Ushindi huo umeipatia Yanga Ngao ya Jamii kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kuibuka na ushindi wa bao hilo katika mchezo uliochezwa leo Jumatano Agosti 12, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Azam TV baada ya mchezo, Kangwanda amesema kabla ya kuingia uwanjani alifahamu angekabiliwa na mchezo mgumu kutokana na ukubwa wa dabi hiyo, lakini kufunga mbele ya mashabiki wengi kumempa morali kubwa.

“Unajua, kabla ya mchezo nilijua kwamba hautakuwa mchezo rahisi. Kwa hiyo, kufunga katika mchezo wa dabi na mbele ya mashabiki wenye hamasa kubwa kiasi hiki, ni jambo linalonipa moyo na kunitia hamasa zaidi. Sasa ninaangalia mbele kwenye michezo ijayo,” amesema Kangwanda.

Mzambia huyo amesema, bao hilo limeongeza kujiamini kwake katika safari yake mpya ndani ya Yanga, huku akisisitiza kuwa furaha yake kubwa ni kuona amesaidia timu kupata ushindi.

“(Bao) linaongeza morali kubwa sana. Ninafurahi mno kwamba nimeweza kuisaidia timu kupata ushindi. Lakini zaidi ya yote, huu ni ushindi wa timu. Kwa hiyo, nawapongeza na kuwashukuru pia wachezaji wenzangu,” amesema.

Kangwanda ameeleza kuwa, hakukuwa na bahati pekee katika nafasi aliyopata hadi kufunga bao, bali ilikuwa ni utekelezaji wa maelekezo ambayo wamekuwa wakipewa na kocha Manqoba Mngqithi kuhusu namna mawinga wanavyopaswa kushambulia lango.

Amesema, kocha aliwaambia kila mpira unapokuwa katika eneo la pembeni, wachezaji wa pembeni wanatakiwa kukimbilia eneo la hatari ili kuwa tayari kupokea krosi.

“Kocha amekuwa akituambia sisi mawinga kwamba tunapaswa muda wote kushambulia lango. Kila mpira unapokuwa upande wa pembeni, unatakiwa kuelekea langoni na kutafuta nafasi ya kufunga,” amesema.

Kangwanda amesema baada ya Boka kupiga krosi, mpira ulimkuta katika eneo sahihi na kazi iliyobaki kwake ilikuwa kuhakikisha anaupeleka langoni kwa kichwa.

“Kwa bahati nzuri, mpira ulifika kwangu na nilichohitaji kufanya ni kuuelekeza langoni. Pia, pongezi nyingi kwa Boka kwa kazi nzuri aliyofanya,” amesema.

Bao hilo limekuwa mwanzo mzuri kwa Kangwanda katika safari yake mpya ndani ya Yanga baada ya kutua dirisha kubwa la usajili akitokea Red Arrows ya kwao Zambia, huku ushindi huo wa 1-0 dhidi ya Simba ukitoa ishara ya ushindani mkali unaotarajiwa katika msimu mpya wa soka 2026-2027.