Kagera Sugar yalia na maproo wanne
Muktasari:
- Kagera ambayo imepanda daraja msimu huu, ilicheza mechi yake ya kwanza ya ligi dhidi ya Simba Jumapili iliyopita na kulala kwa mabao 2-0 nyumbani
BAADA ya kupokea kichapo cha mabao 2-0 ikiwa nyumbani kutoka kwa Simba timu ya Kagera Sugar imesema sababu kubwa ya kichapo hicho ni kukosekana kwa wachezaji wao mahiri kikosini.
Kagera ambayo imepanda daraja msimu huu, ilicheza mechi yake ya kwanza ya ligi dhidi ya Simba Jumapili iliyopita na kulala kwa mabao 2-0 nyumbani
Akizungumza baada ya mchezo huo Ofisa Habari wa timu hiyo Stephen Julius, amesema wamepoteza mchezo huo kutokana na kukosekana kwa wachezaji wao wanne wa kimataifa ambao bado hawajapata vibali na sasa wanapambana kwa nguvu kubwa kuhakikisha kuwa wanakamilisha hilo ili mchezo wa leo dhidi ya Singida waweze kuwatumia.
“Tupo kwenye mchakato wa kuhakikisha tunakamilisha hilo ni wachezaji wazuri ambao wataongeza nguvu kikosini na kuipa timu nafasi ya kufanya vizuri mechi zilizopo mbele yetu baada ya kupoteza dhidi ya Simba,” amesema.
Wachezaji wa kimataifa waliosajiliwa na Kagera Sugar ambao walikosekana mechi ya kwanza dhidi ya Simba ni Wakenya watatu, Collins Maina aliyetokea Fortune Sacco, Boniface Onyango kutoka Kakamega Homeboyz na Ally Salum aliyekuwa Kariobangi Sharks. Pia kuna Mrundi, Emmanuel Mvuyekule aliyetokea Vision FC ya kwao Burundi.
Tatizo la wachezaji wa kigeni kukosa vibali mwanzoni mwa msimu limekuwa likizisumbua timu kadhaa kwenye Ligi Kuu kwa misimu kadhaa sasa.