Mastaa wampokea Jonas Mkude
Muktasari:
- Mkude msimu uliopita wa 2025/26 alikaa nje baada ya kuachana na Yanga aliyoitumikia kwa misimu miwili akitokea Simba ambako alicheza kwa zaidi ya miaka kumi.
BAADA ya Mashujaa kumtambulisha kiungo mkabaji Jonas Mkude waliyemsajili kwa mkataba wa mwaka mmoja wanasoka mbalimbali wameonekana kufurahishwa na hatua yake huku wakimtakia mafanikio katika majukumu yake mapya.
Mkude msimu uliopita wa 2025/26 alikaa nje baada ya kuachana na Yanga aliyoitumikia kwa misimu miwili akitokea Simba ambako alicheza kwa zaidi ya miaka kumi.
Kitendo cha kutangazwa na Mashujaa kimeonekana kuwagusa wachezaji wenzake baada ya kuuvamia ukurasa wa Mashujaa kwa kumpongeza mchezaji huyo, huku wengi wakiamini kuwa anaweza kufanya mambo makubwa msimu huu wa Ligi Kuu.
Miongoni mwa wachezaji waliofurahishwa na hilo ni mshambuliaji wa Newroz ya Iraq Mtanzania Simon Msuva aliyesema:”Kila lenye heri kwako”.
Ukiachana na komenti yake hiyo, katika mtandao wa kijamii wa Instagram Msuva aliwahi kufanya mahojiano na Mwanaspoti alikiri kwamba Mkude ndiye kiungo mahiri zaidi nchini :”Mkude ni kiungo mkabaji bora wakati mwingine upepo unakuwa haujakaa vizuri kwa mchezaji ila haimaanishi kashuka, kwangu ni kati ya viungo bora sana.”
Mastaa kutoka Yanga ambao pia walimtakia kila la heri kiungo huyo ni Dickson Job, Kibwana Shomari, Denis Nkane kila mtu alitumia fursa yake kumpongeza mchezaji huyo.
Kwa upande wa Simba ni nahodha wa zamani wa timu hiyo John Bocco ambaye ni kocha wa kikosi B aliandika :”Nungunungu kila la heri kiungo bora.”
Ukiacha Bocco mwingine kutoka Simba aliyetumia ukurasa wake wa kumpongeza ni beki Nickson Kibabage aliandika:”Kila lenye heri mjomba”.
Mbali na wachezaji, makocha wazawa na mashabiki wenye wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii walionekana kumpongeza mchezaji huyo ambaye sasa anasubiriwa kwa hamu kuonyesha kiwango chake kwa mara ya kwanza nje ya Simba na Yanga.