Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uhamisho wa Neymar barca umedunda hapa

Muktasari:

Mwandishi wa kituo cha Sky Sports News cha Uingereza, Bryan Swanson anachambua kwa nini.

LONDON, ENGLAND.KATIKA dirisha hili la uhamisho lililofungwa Jumatatu, staa wa kimataifa wa Brazil wa PSG, Neymar alionekana yupo njiani kurudi Hispania, hasa katika klabu yake ya zamani Barcelona lakini ghafla uhamisho huo ukaota mbawa.

Mwandishi wa kituo cha Sky Sports News cha Uingereza, Bryan Swanson anachambua kwa nini.

Inakuwaje PSG?

Mtu mmoja wa ndani anadai ‘Kulikuwa na mnunuzi ambaye hakutaka kununua na kulikuwa na muuzaji ambaye hakupania sana kuuza’. PSG walipanga kumuuza Neymara kwa dau ambalo hawakutaka kupunguza.

PSG walipuuza kelele na maombi ya Neymar mwenyewe. Walikaa kibiashara zaidi. Walilipa Pauni 198 milioni na kuvunja rekodi ya uhamisho Agosti 2017 na walitangaza wazi wangemuuza kama ofa ingekuwa nzuri.

PSG walikuwa tayari kukubali pesa na kupewa wachezaji kama uhamisho wa dili hilo lakini haikuwezekana.

Aliitaka Barcelona?

Hili halina ubishi. Alitaka kurudi Nou Camp na alikuwa tayari hata kutoa Pauni 18 milioni kutoka katika mfuko wake kwa ajili ya kusaidia uhamisho huo kufanyika. Neymar mwenyewe aliandika barua kwa Mtendaji mkuu wa PSG, Jean-Claude Blanc Agosti 30, akitoa wazo hilo. Neymar aliahidi kutoa Euro 20 milioni kwa mafungu matano lakini PSG walikataa wazo hilo kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la soka la Ufaransa. Baadaye Neymar aliiambia familia yake ameamua kubakia Ufaransa na akapanda ndege kwenda Marekani jijini Miami kwa ajili ya kujiunga na kikosi cha Brazil Septemba Mosi.

Alituma picha yake Instagram akiwa restaurant ufukwe wa Miami na wafuasi wake 125 milioni wa Instagram walijua atarudi Ufaransa.

Kwa nini alitaka kuondoka PSG?

Kuna sababu nyingi. Neymar aliamini waamuzi wa Ufaransa walikuwa hawamlindi, aliamini baadhi ya wachezaji wenzake wanamwonea wivu, lakini pia anaamini mashabiki wanashindwa kukikubali vyema kipaji chake.

Neymar pia anaamini vyombo vya habari vya Ufaransa havimtendi haki. Inadaiwa Kocha wa PSG, Thomas Tuchel alitaka kumchezesha katika pambano la ufunguzi la Ligi dhidi ya Nimes Agosti 11. Neymar alikuwa tayari kucheza lakini hakukubali sharti alilopewa la kutoa kauli angebakia klabuni hapo. Akaamua kutocheza.

Barcelona walipania kumrudisha?

Inawezekana ni kweli Barcelona walipania kumrudisha lakini sio kwa njia ambayo ingewapendeza PSG. Kipesa ni tayari walishatumia pesa nyingi mwanzoni mwa dirisha la uhamisho baada ya kumnasa Antoine Griezmann kutoka Atletico Madrid. Barcelona walikuwa wamejiandaa na dili la mkopo kisha kumnunua msimu ujao. Hata hivyo walipata wakati mgumu wa kuongeza mchezaji katika dili hilo. Philippe Coutinho alijiunga na Bayern Munich.

Ousmane Dembele aliweka wazi hakutaka kuondoka. Barcelona waliishiwa maarifa.

Lionel Messi alitaka sana dili litokee lakini halikutokea. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa ufundi wa PSG, Leonardo, ofa pekee ya Barcelona ya maandishi ilikuja wakati mabosi wa timu hizo walipoongea uso kwa uso jijini Paris Agosti 27.

Haikuwa nzuri kwa PSG na walikataa. Kulivuja habari klabu hizo zilifikia makubaliano Agosti 29 lakini baadae ikagundulika kwamba hazikuwa habari za kweli.

Real Madrid walikuwa na nafasi yoyote?

Inadaiwa ni kweli Real Madrid walivutiwa na mpango wa kumchukua Neymar mpaka dakika za mwisho za kufungwa kwa dirisha hilo, hawakufikia makubaliano na PSG.

Kukwama kwa dili hakushangazi?

Ndio na hapana. Neymara, baba yake na wawakilishi wake wa karibu walifanya kikao Jumamosi Agosti 21 na kuamua ingekuwa ni kupoteza muda kuendelea kushikilia uhamisho huo ufanyike.

Walikubaliana na ukweli Neymar inabidi abakie tu Paris. Walikubaliana mawazo yake yote ayaelekeze katika mpira na uvumi mwingi kuhusu hali yake ya baadaye ulikuwa unaharibu sifa yake.

Baadaye Barcelona na Real Madrid waliambiwa ukweli Neymar alikuwa ameamua kubakia PSG.

Neymar ana furaha kubaki, mashabiki je?

Mtu mmoja wa karibu na Neymar anasema “Amejikita na PSG sasa. atatoa asilimia 100 ya uwezo wake. anapenda soka, ni mshindi, na atafanya kila anachoweza kushinda mataji.

Ni kitu cha kawaida wakati mwingine kujisikia kwenda kwingine. Katika moyo wake na akili yake anabakia kuwa mchezaji wa PSG. Ataonyesha hilo uwanjani.”

Uhusiano wake na PSG umeimarika tangu aliporudi katika mazoezi ya msimu mpya Julai. Akirudi klabuni baada ya wikiendi hii ya mechi za kimataifa anatazamiwa kutimiza majukumu yake klabuni.

Haieleweki mashabiki watampokea vipi. Baadhi ya mashabiki bado wana hasira kwa alichofanya.

Inabidi arudishe uhusiano upya na hilo litategemea jinsi atakavyoonyesha kiwango.

Neymar amesimamishwa katika mechi tatu za mwanzo za Ligi ya mabingwa baada ya kuikosoa Uefa msimu uliopita kupitia mtandao wake wa Instagram baada ya PSG kuondolewa na Manchester United nyumbani.

Lakini kama akicheza vema katika mechi dhidi ya Real Madrid, Galatasaray na Club Brugge, na kufurahia mafanikio ya mataji ya ndani, basi anaweza kusamehewa vilivyo na mashabiki wenye chuki wa PSG.