Twiga Stars mechi ya kufa na kupona WAFCON
Muktasari:
- Tanzania imejikuta kwenye presha kubwa baada ya kupoteza mchezo wake wa pili dhidi ya Burkina Faso kwa mabao 2-1, matokeo yaliyovuruga nafasi ya kufuzu mapema na kuifanya mechi dhidi ya Ivory Coast kuwa ya lazima kupata matokeo chanya.
HATMA ya Timu ya Taifa,Twiga Stars katika fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 itafahamika usiku wa Agosti 4, itakaposhuka kwenye Uwanja wa Larbi Zaouli mjini Casablanca kuivaa Ivory Coast katika mchezo wa mwisho wa Kundi B wa kuamua timu zitakazofuzu hatua ya robo fainali.
Tanzania imejikuta kwenye presha kubwa baada ya kupoteza mchezo wake wa pili dhidi ya Burkina Faso kwa mabao 2-1, matokeo yaliyovuruga nafasi ya kufuzu mapema na kuifanya mechi dhidi ya Ivory Coast kuwa ya lazima kupata matokeo chanya.
Katika mchezo huo, Burkina Faso ilipata mabao kupitia Naomi Kabré na Balkissa Sawadogo, huku Aisha Mnunka akiifungia Tanzania bao pekee.
Hadi sasa Ivory Coast inaongoza ikiwa na pointi nne baada ya kuifunga Burkina Faso mabao 4-1 katika mchezo wa kwanza na kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Afrika Kusini.
Twiga Stars iko nafasi ya tatu na pointi tatu baada ya kushinda mechi moja dhidi ya Afrika Kusini kwa mabao 2-1 na kupoteza mechi moja dhidi ya Burkina Faso.
Kutokana na msimamo huo, hakuna timu ambayo tayari imekata tiketi ya robo fainali. Hilo linaifanya michezo yote miwili ya mwisho ya kundi hilo iwe na uzito wa mkubwa kwani kila matokeo yanaweza kubadilisha nafasi za timu.
Kwa Tanzania, ushindi dhidi ya Ivory Coast ndiyo njia salama zaidi ya kufuzu. Ikishinda itaifikisha pointi sita na itakuwa na nafasi kubwa ya kumaliza katika nafasi mbili za juu kulingana na matokeo ya mchezo mwingine kati ya Burkina Faso na Afrika Kusini.
Iwapo Twiga Stars itatoa sare dhidi ya Ivory Coast, itafikisha pointi nne na italazimika kusubiri matokeo ya Burkina Faso dhidi ya Afrika Kusini.
Endapo mchezo huo pia utamalizika kwa sare au matokeo yatakayoiweka Tanzania mbele kwa tofauti ya mabao, bado inaweza kujikuta ikisonga mbele ama kama mshindi wa pili au kutegemea kanuni za washindi bora wa nafasi ya tatu.
Hata hivyo, endapo Tanzania itapoteza dhidi ya Ivory Coast, itabaki na pointi tatu na nafasi yake ya kufuzu itakuwa ndogo sana, ikitegemea matokeo pamoja na tofauti ya mabao. Hivyo, kikosi cha Kocha Bakari Shime kinaingia uwanjani kikijua kuwa hakina nafasi ya kufanya makosa.
Kwa upande wa Ivory Coast, sare pekee inaweza kuifanya ifikishe pointi tano na kubaki kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele. Ushindi utaifanya ifikishe pointi saba na kumaliza kileleni mwa kundi bila kuangalia matokeo ya mchezo mwingine.
Burkina Faso nayo inaingia kwenye mchezo dhidi ya Afrika Kusini ikiwa na morali kubwa baada ya ushindi dhidi ya Tanzania. Ikiifunga Afrika Kusini itafikisha pointi sita na kufuzu moja kwa moja. Sare inaweza pia kuipa nafasi nzuri, lakini italazimika kusubiri matokeo ya Tanzania dhidi ya Ivory Coast.
Afrika Kusini nayo bado iko kwenye mbio za kufuzu. Ushindi dhidi ya Burkina Faso unaweza kuifikisha pointi nne na kuipa nafasi ya kutinga robo fainali, hasa iwapo Tanzania haitashinda dhidi ya Ivory Coast.
Kwa Twiga Stars, changamoto kubwa itakuwa namna ya kuhimili safu ya ushambuliaji ya Ivory Coast iliyoonyesha makali tangu mwanzo wa mashindano. Katika mechi mbili zilizopita, timu hiyo imefunga mabao sita, jambo ambalo litahitaji Tanzania kucheza kwa umakini mkubwa kuanzia filimbi ya mwamuzi hadi dakika za mwisho.
Lakini Tanzania nayo imeonyesha kuwa inaweza kupambana. Katika ushindi wake wa kwanza ilionesha nidhamu ya mchezo, hata dhidi ya Burkina Faso ikirejea mchezoni kupitia bao la Aisha Mnunka kabla ya kuruhusu bao la ushindi dakika za mwisho. Makosa hayo ndiyo ambayo benchi la ufundi litahitaji kuyarekebisha kabla ya kuvaana na Ivory Coast.
Dakika 90 za mchezo huo zitakuwa na thamani kubwa kwa Stars, kwani ushindi utaifanya Tanzania kuandika historia mpya kwenye fainali hizo.