Twiga Stars matumaini kufuzu robo fainali yapo
Muktasari:
- Tanzania kwa sasa ina pointi tatu, sawa na Burkina Faso, wakati Ivory Coast inaongoza kwa pointi nne na Afrika Kusini ikiwa na pointi moja. Hivyo, kila timu bado inaweza kubadilisha nafasi yake katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi.
BAADA ya Tanzania kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Burkina Faso kwenye mechi ya pili ya kundi B ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake, matumaini ya Twiga Stars kufuzu hatua ya robo fainali bado yapo.
Tanzania kwa sasa ina pointi tatu, sawa na Burkina Faso, wakati Ivory Coast inaongoza kwa pointi nne na Afrika Kusini ikiwa na pointi moja. Hivyo, kila timu bado inaweza kubadilisha nafasi yake katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi.
Kwa Tanzania ili ifuzu itahitahi kushinda mechi ya mwisho dhidi ya Ivory Coast utakaochezwa Agosti 4.Wakati huohuo, Burkina Faso itakutana na Afrika Kusini katika mchezo mwingine wa Kundi B.
Twiga Stars ikishinda, itafikisha pointi sita na kujihakikishia nafasi nzuri sana ya kumaliza katika nafasi mbili za juu za kundi.
Hata hivyo, kundi hilo limekaa kimtego sana iwapo Burkina Faso itashinda dhidi ya Afrika Kusini pia inaweza kufikisha pointi sita na itaangaliwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Tanzania ikitoka sare, itafikisha pointi nne. Hapo mambo yatakuwa magumu zaidi kwa sababu Ivory Coast pia inaweza kubaki na pointi nne au kuongeza idadi hiyo, huku Burkina Faso ikiwa na nafasi ya kufikisha pointi sita iwapo itaifunga Afrika Kusini.
Kwa upande mwingine, Tanzania ikipoteza, itabaki na pointi tatu na hapo itahitaji kutegemea matokeo ya mchezo wa Burkina Faso na Afrika Kusini pamoja na hesabu za nafasi ya timu iliyomaliza nafasi ya tatu. Katika mfumo wa WAFCON 2026, timu mbili za juu kutoka kila kundi pamoja na timu mbili bora zilizomaliza nafasi ya tatu ndizo zinazofuzu robo fainali hivyo Twiga Stars ikifanya vizuri inaweza kutoboa hapo.