Aisha Masaka kurejea Brighton
Muktasari:
- Kwa Masaka kinachofuata ni kurejea katika hali nzuri na kupata nafasi ya kuonyesha uwezo uliomfanya Brighton imsajili kutoka Häcken.
UONGOZI wa mshambuliaji wa Tanzania, Aisha Masaka anayekipiga Brighton & Hove Albion Women unaamini bado nyota huyo ana uwezo wa kuendelea kucheza kikosini hapo licha ya changamoto za majeraha yaliyompata.
Masaka, ambaye aliandika historia mwaka 2024 kuwa Mtanzania wa kwanza wa kike kucheza Ligi Kuu England, amekuwa akikumbana na kipindi kigumu tangu alipojiunga Brighton akitokea BK Häcken ya Sweden.
Msimu wake wa kwanza England haukuwa mzuri akikubwa na majeraha kiasi yaliyomfanya apate muda mchache wa kucheza kikosini hapo.
Masaka aliumia kwenye mechi dhidi ya Arsenal Novemba 2024, alipoingia kipindi cha pili lakini muda mfupi baadaye akapata jeraha kubwa la bega. Jeraha hilo lilimuweka nje kwa takribani miezi mitano na kumfanya atumie muda mwingi nje ya uwanja wakati wenzake wakiendelea na mashindano ya WSL.
Baada ya kurejea Masaka kuanza kujenga kasi yake yalikwazwa tena na jeraha la goti alilolipata akiwa kwenye maandalizi ya Twiga Stars kwa WAFCON. Hilo lilimfanya akose nafasi ya kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano hayo, huku Brighton pia ikiendelea kumfuatilia kwa karibu kupitia timu yake ya kitabibu.
“Sioni sababu kwa nini Aisha aondoke sasa. Nafikiri ana hamu ya kurejea kucheza haraka iwezekanavyo. Amekuwa hana bahati na majeraha,” amesema kiongozi huyo;
"Tunapambana kuhakikisha anarejea uwanjani timu imeshampa taarifa kuwa haitaendelea naye hivyo tulikuwa tunaangalia timu itakayokwenda kucheza."
Kwa Masaka kinachofuata ni kurejea katika hali nzuri na kupata nafasi ya kuonyesha uwezo uliomfanya Brighton imsajili kutoka Häcken.