Tshabalala awaachia msala wazawa Simba

Muktasari:

  • Wazawa pekee unaoweza kusema wanatamba kikosini hapo ni beki wa kulia Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr.’, aliyetua kikosini miaka 10 iliyopita akitokea Kagera Sugar.

SIMBA bado kunafukuta. Timu hiyo inapitia kipindi kigumu cha mpito ambacho mambo mengi yametokea na yatatokea lakini wakijipanga vizuri yatapita na wakali hao wa Msimbazi watarejea kwenye ubora na uimara wao kama taasisi imara ya soka.

Wakati upepo huo ukiendelea kupita Simba, Mwanaspoti inakudokeza sababu nyingine ambayo imeifanya timu hiyo kukosa uimara. Si nyingine ni wachezaji wazawa.

Simba kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa eneo gumu sana kwa wachezaji wazawa wanaosajiliwa kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza na kuonyesha ubora. Wengi husajiliwa kisha baadaye kuondoka baada ya kushindwa kupata nafasi kutokana na sababu mbalimbali.

Ukikiangalia kikosi cha Simba cha sasa mchezaji mzawa anayepata nafasi muda mwingi na amesajiliwa katika minne ya hivi karibuni ni Kibu Denis, wengine wote hali ni tete na wengi wamesepa zao.

Wazawa pekee unaoweza kusema wanatamba kikosini hapo ni beki wa kulia Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr.’, aliyetua kikosini miaka 10 iliyopita akitokea Kagera Sugar.

Shomari Kapombe na Aishi Manula waliosajiliwa mwaka 2017 kwa pamoja wakitokea Azam FC, na kwa mbali Mzamiru Yassin aliyesajiliwa mwaka 2016 akitokea Mtibwa Sugar labda na Kennedy Juma aliyetua msimbazi 2019 akitokea Singida United.

Kwa maana hiyo nguzo ya Simba kwa wazawa ipo katika wachezaji wanne hadi watano tu kwani tungemuweka John Bocco lakini tayari straika huyo amejiengua kwenye timu na anafanya kazi ya ukocha kwa sasa akikinoa kikosi cha vijana cha Simba.

Mwandishi na mchambuzi wa soka wa Mwanaspoti, Oscar Oscar alisema Simba inashindwa kuwa imara uwanjani kutokana na kukosa nguvu ya wachezaji wazawa.

“Tatizo kubwa la Simba sio wachezaji wa nje, ni kushuka kiwango na majeraha kwa wachezaji wazawa. Pamoja na ubora wa wageni, Simba iliyotisha hivi karibuni ilikuwa na wachezaji wengi bora wazawa. Manula, Erasto Nyoni, Kapombe, Zimbwe Jr, Boccco, Jonas Mkude na Muzamiru Yassin,” alisema Oscar na kuongeza;

Simba inahitaji wachezaji watano hadi sita wazawa kwenye kikosi cha kwanza. Msingi wa Simba bora unajengwa na wazawa bora,” alisema Oscar aliyetoa mfano wa Yanga ilivyoimara kwa sasa kutokana na kuwa na wazawa wengi walio kwenye kiwango bora akiwataja Mudathir Yahya, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Jonas Mkude na Clement Mzize.

Pamoja na kwamba usajili ni kubahatisha lakini Simba imekuwa sehemu chungu zaidi kwa Wazawa kwani mara nyingi husajili wazawa wenye viwango bora kulingana na rekodi zao kwenye timu walizotoka lakini wakitua Msimbazi mambo hupwaya.

Utawakumbuka Gadiel Michael aliyetua Simba akiwa moto akitokea Yanga lakini pale alifeli, Ibrahim Amme aliyekuwa kitasa pale Coastal Union akizima na Mwamnyeto lakini Simba pakawa pagumu kwake, hivyo hivyo kwa Ibrahim Ajibu aliyetoka Yanga akiwa bora sana lakini Simba akawa wa kawaida.

Miraji Athuman alitoka Lipuli akiwa hashikiki, Simba akawa mchezaji wa benchi hivyo hivyo kwa Charles Ilamfya aliyekuwa KMC moto lakini Simba kukawa kuchungu kwake. Hao wote kwa sasa wameondoka Simba baada ya mambo kuwa magumu.

Wapo wengi, wamekimbia Msimbazi kutokana na mambo kuwa magumu kwa wazawa kwa miaka ya hivi karibuni, Unamkumbuka Abdulswamad Kassim aliyesajiliwa Simba akitokea Kagera? Vipi kuhusu Yusuph Mhilu na Jimmyson Mwanuke? Wote hao walitua Simba wakiwa wakali lakini sasa hawapo Msimbazi baada ya maisha ya pale kuwawia ugumu kisoka.

Msimu uliopita pia walisajiliwa Nassoro Kapama akiwa moto kutokea Kagera, kipa Jeremiah Kisubi, Habib Kyombo na bwana mdogo Mohamed Mussa kutokea Zanzibar. Wote hao benchi la Simba lilikuwa eneo lao la kukaa zaidi ya kucheza na baadaye wakaondoka.

Msimu huu Simba iliwasajili wazawa kipa Hussein Abel, mabeki Hussein Kazi na David Kameta ‘Duchu’, viungo Abdallah Hamis, Edwin Balua, Ladack Chasambi na Salehe Karabaka lakini wote bado hawajafanya maajabu ndani ya kikosi hicho.

Chilunda tayari amejiondoa na kutimkia KMC lakini hata huko anaanzia benchi, Duchu, Hamis, Kazi, Abel, Chasambi na Salehe wao ni kama wasindikizaji tu, kuna muda benchi la ufundi linaamua kutoa nafasi kidogo kwao na wakati mwingi huishia benchi na kwenye majukwaa.


WASIKIE HAPA

Kocha wa zamani wa Simba, aliyekuwa akiwapa zaidi nafasi wazawa, Mbeligiji Patrick Aussems ‘Uchebe’, alisema wachezaji wengi wa Kitanzania (wazawa) wana vipaji vikubwa lakini Simba inakuwa changamoto kwao kutokana na ushindani wa namba na matarajio.

“Nilijaribu kutoa nafasi kwa kila mchezaji lakini ushindani wa namba ulikuwa mkubwa zaidi. Kuna muda nilikuwa naongea na mchezaji mmoja mmoja (mzawa) na kumueleza malengo ya timu na nini anatakiwa kufanya. Wakati mwingine niliwabadilisha hadi maeneo ya kucheza ili wapate nafasi na kuzoea ushindani lakini mwishowe baadhi yao waliniangusha na kushindwa kufikia malengo,” alisema Aussems anayeinoa AFC Leopards ya Kenya na kuongeza;

“Nadhani tatizo lao kubwa ni maisha ya Simba. Pale kuna presha kubwa hivyo mchezaji akishindwa kuhimili na kuimudu basi itakuwa ngumu kwake kuonyesha kiwango bora.”

Uchebe aliinoa Simba kuanzia Julai 2018 hadi Novemba 2019.

Kiungo Abdulswamad aliyesajiliwa Simba na baadaye kuondoka alisema kilichomkwamisha ni kukosa mwanga baada ya aliyemsajili (Zakaria Hans Pope) kufariki lakini pia kocha hakumwamini.

“Simba nilishindwa kwakuwa aliyenisajili alifariki halafu nikawa sina mwanga. Ujue yule mzee muda mwingi alikuwa akinipa nguvu kuwa naweza na nipambane yupo atanisimamia lakini alivyofariki kila kitu kikabadilika kwani nilikuwa sina msimamizi hivyo nilijawa na hofu na kushindwa kufanya vizuri kutokana na presha ya timu ile,” alisema Abdulswamad na kuongeza;

“Jambo jingine sikupewa muda wa kutosha kucheza. Hauwezi kuonyesha ubora wako bila kucheza hivyo hilo lilikuwa changamoto kutokana na eneo langu nililokuwa nacheza (kiungo), kuwa gumu lakini pia kuwepo na watu waliokuwa maalumu kucheza pale,” alisema Abdulswamad aliyetua Simba mwaka 2021 na kukaa miezi sita tu kisha kuondoka na kujiunga na Ruvu Shooting. Msimu huu Abdulswamad alianza na Coastal Union lakini aliachwa na sasa hana timu.

Nahodha msaidizi wa Simba aliyedumu kikosini hapo kwa miaka 10 na kumudu kupata nafasi katika kikosi cha kwanza licha ya ushindani uliopo, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ alisema siri ya kukaa muda mrefu kwenye timu hiyo ni nidhamu na kujitambua.

“Nidhamu ndio kitu cha msingi lakini pia kujitambua. Kufanya mazoezi sana na kufuata maelekezo ya makocha ndio siri ya mafanikio,” alisema Zimbwe Jr maarufu kama Tshabalala jina la kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini.

Kocha Juma Mgunda alisema Simba ni sehemu ngumu kucheza kwa mchezaji ambaye hajajiandaa kisawa sawa kisaikolojia kwani kuna presha kubwa.

“Sio kwamba wachezaji wazawa hawana uwezo wa kucheza Simba lakini wanakumbana na changamoto nyingi ambazo wanashindwa kuzitatua. Simba ni timu kubwa, kuna presha ambayo mchezaji asipoihimili basi anakwenda na maji na hilo linawatokea sana wazawa. Kingine ni ushindani wa namba. Siku zote makocha hutoa nafasi kwa mchezaji aliyetayari na aliyefanya vizuri mazoezini,” alisema Mgunda ambaye kwa sasa ni kocha mkuu wa Simba Queens.

Mwanasaikolojia na Mshauri Nasihi, Godfrey Jumbe alisema tatizo kwa wachezaji wengi wazawa kushindwa kucheza soka kwenye klabu kubwa hususani Simba ni kutokana na mambo mengi yanayowazunguka ikiwemo kupata maisha mazuri.

"Hili jambo linasababishwa na mambo mengi. Sitazungumzia mambo ya kiufundi bali saikolojia zaidi.

Wachezaji wengi wazawa wana shida ya kupokea maisha mapya. Timu hizi kubwa zina utamaduni wa kuwapa mishahara na posho kubwa wachezaji tofauti na ilivyo kwa timu nyingine na hapa wengi wao wanajisahau na kusahau kilichowaleta kwenye hizo timu.

“Jambo jingine linalowakumba ni matokeo baada ya kupata hayo maisha makubwa, wengi hujiingiza kwenye matanuzi zaidi na tunajua matanuzi na soka haviendani na huo huwa mwanzo wao kushindwa," alisema Jumbe aliyeshauri wachezaji wazawa wanaosajiliwa kwenye timu kubwa ikiwemo Simba na Yanga kutafutiwa waangalizi na wasimamizi (mentors) wa ndani ya timu na maisha ya nje ya timu.