Prime
Vita ya namba sita bado mbichi!
KUNA mikwara ambayo Simba na Yanga zinapigana juu ya jezi namba zita ambapo ndani yake kuna vita flani nzito inapigwa kwa klabu zote mbili, ikipimwa jeuri ya fedha lakini zaidi akitajwa kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC.
Simba wanatamani sana kuona siku moja Fei Toto anakuwa kiungo wao lakini hali kadhalika Yanga nao wana kiu ya kuona kiungo wao wa zamani anarudi kuwatumikia sasa mikwara imebaki kwa mashabiki na vigogo wa juu wa klabu hiyo.
Hivi karibuni taarifa zinasema kuwa Simba wameshamalizana na kiungo huyo na wamekubaliana kila kitu ukiwemo mshahara wake na kumpa jezi hiyo namba sita, huku pia ikielezwa kuwa Yanga nao wanapambana kuhakikisha kiungo huyo fundi haendi kwa wapinzani wao na kuhakikisha wanamrudisha Jangwani sehemu ambayo alitoka na kujiunga na Azam.
Vita hivyo imebakiza siku nne tu aidha kama timu hizo moja itaipata saini ya kiungo huyo aliyebakiza mwaka mmoja na Azam au atabaki kwenye viunga vya Chamazi hadi mwishoni mwa msimu.
JEZI NAMBA SITA WAZI
Ukienda Simba jezi namba sita hakuna mchezaji anaitumikia kwa sasa, mara ya mwisho ilitumiwa msimu wa juzi na kiungo Mkongomani Fabrice Ngoma ambapo tangu alipoondoka kuanzia mpaka sasa hakuna ambaye anaitumia na inaelezwa kuwa kwenye mazungumzo ya Fei hili ni moja ya jambo ambalo lipo kwenye mkataba wake.
Kwa upande wa Yanga, nako hali iko kama hivyo, jezi hiyo haina mtu kwasasa ikibaki wazi na aliposajiliwa kiungo mkabaji Freddy Ngoma ilielezwa kwamba angetumia jezi hiyo lakini ikazuiwa kisha akapewa namba nane, mchezaji wa mwisho kuivaa alikuwa Msauz Mahalatse Makudubela ‘Skudu’ ambaye aliichezea timu hiyo kwa msimu mmoja tu wa juzi, hali hii inaonyesha kuwa jezi hiyo ipo maalumu kwa ajili ya ingizo hilo jipya kwenye kikosi hicho.
PRESHA KWA MATAJIRI
Tajiri wa Yanga Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ inafahamika kwamba anataka kumrudisha kiungo huyo ambaye misimu miwili iliyopita alichukuliwa na Azam kwa mikiki na mivutano iliyomalizwa na busara za Serikali.
Yanga inaelezwa imempa ofa ya kufuru Fei Toto yenye thamani ya sh 3 Bilioni ambayo Mwanaspoti linafahamu kwamba kiungo huyo ameshawishika kabisa kukubali kurudi klabu yake hiyo ya zamani, lakini anakutana na ugumu kwa kuwa tayari pia alishazungumza na Simba ambao hawajafikia kiwango hicho cha fedha.
Taarifa kutoka ndani ya familia ya Fei Toto ni kwamba ukiacha dau hilo la usajili kiungo huyo pia atavuta mshahara mkubwa kushinda ule anaouchukua Azam FC.
Simba nao waanatamani kuwa na Fei Toto na presha kubwa haitoki kwa makocha wala viongozi bali kwa wanachama na mashabiki ambao wana kiu ya kuona kiungo huyo anajiunga na timu yao kwa kuiongezea nguvu.
Simba awali ilikuwa imefikia dau la sh 2 Bilioni lakini matajiri wa klabu hiyo walikuwa wanajipanga kuongeza mzigo huo ili kumpata kiungo huyo vita hiyo ikiendelea atakayepoteza Dabi ya kesho atatakiwa kupambania zaidi saini hii ili kushusha presha.
NAMBA SITA MITANDAONI
Yanga ndio ilianza na mkwara wa namba sita ikitengeneza machapisho kuhusu jezi hiyo na mashabiki wake wakauvaa upepo huo wakisubiri kuona nani atatambulishwa juzi kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi, ambapo hata hivyo hakuna mchezaji ambaye alitambulishwa au jezi hiyo kuzungumzwa.
Wakati Yanga wakichagiza hivyo, Simba nayo tajiri yao Mohammed Dewji ‘MO’ akanunua kesi hiyo kwa kuchapisha jezi hiyo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram ingawa baadaye alitoa chapisho hilo, lakini kauli kuwa fedha zipo benki ni ishara kuwa tayari wanamazungumzo mazuri na Fei na kukubaliana dau.
FEI NA AZAM
Uhalisia ni kwamba Fei Toto bado ni mchezaji halali wa Azam FC akibakiza mkataba wa mwaka mmoja ambapo akiitumikia msimu ujao atakuwa amemalizana na matajiri hao wa Chamazi huku pia hakuna timu ambayo imeufuata uongozi wa klabu hiyo kutaka huduma ya kiungo huyo.
“Sisi tunasikia tu taarifa hizo kwenye mitandao hakuna klabu ambayo imetufuata, Feisal ni mchezaji wetu na hivi tunavyozungumza anaendelea na maandalizi yake ya msimu ujao, tumeshazoea hizi taarifa kila wakati sasa hatuwezi kuwa watu wa kuendelea kujibu suala ambalo watu wanajua utaratibu wake,”amesema Rais wa Azam FC Nassoro Idrisa ‘Father’
MSIKIE KAMWE
Akizungumzia kuhusu chapisho la usajili wa namba sita Meneja wa Habari wa Yanga Ally Kamwe, amesema Yanga bado haijafunga usajili na kwamba kutozungumzia lolote juu ya namba sita kwenye siku ya Yanga bado kuna muda wa usajili.
“Nikweli hatujamtambulisha yoyote lakini angalia hizi siku hapa mpaka kufikia kufungwa dirisha la usajili lolote linaweza kutokea, msimalize maneno kwanza muda bado unatutosha kabisa,”amesema Kamwe.