Tamasha la Simba lilivyobadili burudani ya soka
Muktasari:
- Tamasha hilo ambalo ni la 17 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009, limekuwa likifanyika sambamba na burudani kwa wasanii hasa wale mashabiki wa timu hiyo kulipamba kwa kuimba nyimbo zao na zile za kuisifu timu yao.
SIMBA inatarajia kufanya Tamasha la Simba Day leo kwa lengo la kutambulisha wachezaji na benchi la ufundi, huku zoezi hilo likisindikizwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali.
Tamasha hilo ambalo ni la 17 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009, limekuwa likifanyika sambamba na burudani kwa wasanii hasa wale mashabiki wa timu hiyo kulipamba kwa kuimba nyimbo zao na zile za kuisifu timu yao.
Kadri miaka inavyokwenda tamasha hilo linazidi kukua na kuvutia si tu wapenda soka bali hata wasanii na mashabiki wao na wamekuwa wakiisubiri sana Agosti ili kushuhudia tamasha hilo.
Burudani katika tamasha hili imekuwa ikihusisha mfumo wa kisasa wa sauti, DJs, MCs, madansa na maonyesho ya moto (fireworks), huku majina makubwa ya wasanii wakinogesha na kwa miaka ya karibuni wameshuhudiwa wasanii kama Alikiba, Joh Makini, Chino Kidd, Oka Martin, Mbosso na Tunda Man yamewahi kuwasha jukwaa hilo, kila mmoja akiacha alama yake mbele ya maelfu ya mashabiki waliofurika uwanjani.
WASANII WANAVYOIPAMBA
Ukiambiwa ni zaidi ya burudani ndiyo hivi. Mashabiki wanaofika wanjani na wanaofuatilia tamasha hili wakiwa nyumbani, wanapata burudani kutoka kw wasanii wakubwa kama ilivyokuwa mwaka uliopita 2025 na Mbosso Khan ndiye aliyekinukisha kwa ubunifu wa aina yake.
Shoo ya msanii huyo ni moja ya zilizoacha kumbukumbu tamu hasa kutokana na ubunifu uliofanyika wa kuingia na kundi kubwa la watu waliomsindikiza kutoa burudani kwa staili ya 'mazombi' kama ilivyo katika filamu za Mad Max, wakiwa wamejichora kwa rangi nyeupe na magari waliyotumia yakifanana na ya kwenye filamu hiyo.
Mkali huyo wa kibao cha ‘Mr Dj’ aliimbia kwa dakika 62 ambazo kila shabiki aliyekuwa jukwaani aliinjoi shoo hiyo ambayo aliimba vibao vyake karibu tisa ikiwemo ‘Sele’, ‘Aviola’,’Pawa’ na ngoma nyinginezo.
Katika Simba Day ya mwaka 2024, Ali Kiba alikuwa kivutio kikuu akishirikiana na Joh Makini na Chino Kidd na wimbo wake 'Mnyama uliotoka kipindi hicho ulileta mzuka katika tamasha hilo.
Ubunifu mwingine ulionekana katika shoo ya Tunda Man na katika tamasha la Simba Day 2023 aliingia akiwa ndani ya jeneza na kuvutia umati uliojitokeza.
Shoo nyingine iliyotikisa ni ya Diamond Platnumz ambaye katika tamasha hilo la mwaka 2020 akiongozana na Haji Manara aliyekuwa msemaji wa klabu hiyo, walitinga na helikopta na kupiga shoo iliyovuta hisia za mashabiki waliofika Uwanja wa Benjamin Mkapa. Mwaka 2022, ilishuhudiwa ubunifu mwingine kutoka kwa Zuchu ambaye aliingia uwanjani akiwa anashuka na kamba na kushangiliwa na maelfu ya mashabiki waliofika uwanjani hapo.
Wasanii wengine waliopata shavu na kufanya makubwa ni Twanga Pepeta, Meja Kunta, Mwasiti.
USHEREHESHAJI wanaibua vaibu
Kabla ya kila shoo ya msanii huwa kuna madj's wanasherehesha katika kuwaweka sawa mashabiki na hii imekuwa ikiwapa vaibu la kuendelea kusubiri wakati wote wa tamasha.
Katika tamasha hili, madj's wamekuwa wakitumika kuleta vaibu wakiwamo DJ Sinyorita, DJ White na DJ Bike na wameongeza mvuto katika matamasha hayo kutokana na ufundi wao wa kucheza na muziki wakitumia vidole vyao vya mikono.
KUNAPENDEZA
Kila mwaka kumekuwa na mabadiliko makubwa kuanzia uandaaji wa tamasha kabla na limekuwa likiambatana shamrashamra za nje ya uwanja siku chache kabla ya kilele hicho na mashabiki na wanachama wanakutana na viongozi wa hamasa wa klabu kuhamasishana ikiwamo kuchangia damu na kufanya shughuli za kijamii.
Pia siku ya tamasha kumekuwa na mabadiliko ikiwamo jukwaa na aina ya utambulishaji na kila mwaka mashabiki wanasubiri kuona ni nini kitakuwa kipya huku pia washereheshaji wakija na ubunifu tofauti wakiongozwa na msemaji wa klabu hiyo Ahmed Ally.
Mwaka jana mtangazaji, Meena Ally ndiye aliyekuwa MC katika tamasha hilo na mvuto wake ulilifanya kuvutia na ndiyo maana hata mwaka huu amepewa tena nafasi hiyo akishirikiana na Richard Nyondo ‘Rich Msafi’, Adam Mchomvu na Samio Love.
Ni wa zi mwaka huu Simba inataka kuongeza ladha zaidi katika tamasha lao ambalo limekuwa likianza mapema asubuhi kwa mashabiki kuwahi uwanjani ili kupata nafasi kwani kutokana na idadi yao, wengi huishia getini kwa kushindwa kuingia na kujikuta wakilifuatilia kwenye runinga.
Pia mwaka huu linafanyia Uwanja wa Uhuru ambao hauingizi mashabiki wengi na wale watakaowahi tiketi ndio watakaoshuhudia moja kwa moja.
Alikiba ndiye msanii mkuu wa tamasha hilo, akirejea kwenye jukwaa ambalo amewahi kulitikisa huko nyuma. Hata hivyo, pamoja na uwepo wake, jambo kubwa litakalosubiriwa ni kuona kama Simba itaendelea kufanya kwa kiwango cha burudani kilichoifanya Simba Day kuwa moja ya matamasha makubwa zaidi yanayounganisha michezo na muziki nchini. Baada ya miaka 17, jambo moja linaonekana wazi Simba Day haijawahi kuwa sherehe ya mpira wa miguu, bali imekuwa tamasha linaloandika historia mpya ya burudani Tanzania.