Tamasha la Kizimkazi kuwaunganisha wananchi
Muktasari:
- Ameyasema hayo katika mchezo wa Fainali uliowakutanisha mashabiki wa Yanga na Simba wa Mkoa wa Kusini uliochezwa kwenye Uwanja wa Mpira wa Miguu Kitogani uliopo Mkoa wa Kusini Unguja.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema Tamasha la Kizimkazi (Kizimkazi Festival) linaendelea kuwaunganisha na kuwaweka pamoja wananchi kutokana na shughuli za maendeleo zinazofanyika kupitia tamasha hilo.
Ameyasema hayo katika mchezo wa Fainali uliowakutanisha mashabiki wa Yanga na Simba wa Mkoa wa Kusini uliochezwa kwenye Uwanja wa Mpira wa Miguu Kitogani uliopo Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika fainali hiyo, Hemed aliwataka wanamichezo kucheza mpira kwa nidhamu na kufuata kanuni na sheria za soka huku wakipaswa kutambua kuwa kupitia michezo fursa mbalimbali zinapatikana ikiwemo ajira.
Hemed aliwaasa wanamichezo hao kujiepusha na makundi maovu ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya na kutoshiriki katika matukio mabaya yanayoweza kutaharisha amani ya nchi.
Amesema amelipokea ombi la Mbunge wa Paje, Jaffar Ismail Sanya la kuangaliwa tena bei za kuvitumia viwanja vya Wilaya na kusema Serikali itaangalia namna ya kulifanyia kazi ili vijana waweze kufaidika na viwanja hivyo.
Mbunge wa Jimbo la Paje, Jaffar Ismail Sanya amesema lengo la kujengwa kwa viwanja vya michezo vya Wilaya na Mikoa ni kuimarisha michezo na kukuza vipaji vya vijana, hivyo ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguzwa gharama katika viwanja hivyo ili fursa za kuvitumia iwe kubwa.
Sanya alizipongeza timu zilizoshiriki katika Fainali ya Tamasha la Kizimkazi kwa kucheza kwa nidhamu na kufuata kanuni na sheria zinazoongoza mpira wa miguu.