Waamuzi 65 wafuzu mtihani utimamu wa mwili
Muktasari:
- Kati ya waamuzi 65 waliofuzu, wanawake ni wanane, hatua inayotarajiwa kutoa nafasi kwa waamuzi hao kuendelea na majukumu yao katika mashindano mbalimbali ya soka Zanzibar msimu wa 2026-2027.
WAAMUZI 73, wakiwemo wanawake 12, wamefanya mtihani wa utimamu wa mwili katika Uwanja wa Mao Zedong kisiwani Unguja, huku 65 wakifanikiwa kufuzu na 18 wakishindwa.
Kati ya waamuzi 65 waliofuzu, wanawake ni wanane, hatua inayotarajiwa kutoa nafasi kwa waamuzi hao kuendelea na majukumu yao katika mashindano mbalimbali ya soka Zanzibar msimu wa 2026-2027.
Mtihani huo ulikuwa sehemu ya mchakato wa kuwapima waamuzi uwezo wao wa kimwili kabla ya kuanza kwa msimu wa 2026-2027, huku waliofuzu wakipangwa katika madaraja mbalimbali kulingana na uwezo na viwango vyao. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Kamati ya Waamuzi Zanzibar, Issa Haji Vuai, baadhi ya waamuzi waliofuzu wataendelea kuchezesha mechi za Ligi Kuu ya Zanzibar, huku wengine wakipewa majukumu ya kuchezesha ligi za madaraja ya chini.
Amesema, baadhi ya waamuzi wanaofanya vizuri wanatarajiwa kupandishwa madaraja. Akizungumzia mtihani huo, Vuai, amesema zoezi hilo lilikuwa zuri na lilihusisha ushindani mkubwa miongoni mwa waamuzi.
“Waamuzi walijiandaa sana na hilo lilionekana katika ushiriki wao,” amesema Vuai. Amesema maandalizi mazuri ya waamuzi ni muhimu katika kuhakikisha wanakuwa katika hali bora ya kimwili kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao uwanjani kwa ufanisi.
Matokeo hayo pia yanaweka msisitizo kwa waamuzi ambao hawakufanikiwa kufuzu kuendelea kujiandaa kwa ajili ya kupata nafasi nyingine ya kuonesha uwezo wao, huku wale waliofuzu wakitakiwa kuendelea kudumisha kiwango chao cha utimamu wa mwili.
Mtihani huo uliofanyika Mao Zedong unatarajiwa kuwa sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha waamuzi wanaopewa majukumu ya kusimamia mashindano ya Zanzibar wanakuwa na viwango vinavyokidhi mahitaji ya ushindani.