Super 8 kwa faida ya nani?

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania ,Jamal Malinzi.
Muktasari:
- Historia inajitosheleza, Ligi ya Muungano ilianzishwa ili kupata wawakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
NIMEWASOMA kwa umakini sana wachambuzi wa soka nchini na baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakichagiza na kushadadia kurudishwa kwa Ligi ya Muungano, wenyewe wanataka iitwe ‘Super 8’. Maana yake timu nne za Bara na Zanzibar zichuane.
Historia inajitosheleza, Ligi ya Muungano ilianzishwa ili kupata wawakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Miongoni mwa hao wanaopigia debe kurudishwa michuano hiyo kuwa tangu mwaka 2004 Zanzibar ilipopewa uanachama wa Caf na kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho (zamani Kombe la Washindi), Ligi ya Muungano ilipoteza uhalali.
Miaka 12 baadaye wanakuja watetezi wa Super 8 na hoja dhaifu kuwa ni wakati mwafaka kurudisha michuano hiyo! Bila kupepesa macho wala kope, nasema wazi michuano hiyo haina hata chembe ya uhalisia na ulazima kwani sababu zilizofanya iwepo hazipo tena.
Nani kati ya wapenzi wa soka au viongozi wa Bara na Zanzibar wanaokosa usingizi kwa kutokuwepo michuano hiyo? Imekosekana kwa miaka 12, kuna mwenye tatizo? Kinyume chake, Zanzibar imejipatia nafasi iliyokuwa ikiipigania kama inayoendelea kuipigania ya kuwa kuwa mwanachama wa Fifa.
Mtindo huu wa kubuni miradi ya mashindano kwa mgongo wa ‘kuutaka kuimarisha Muungano’ si ueledi na wala hauna tija katika soka la karne ya 21, soka la biashara.
Soka biashara
Kwa siku hizi soka ni biashara kubwa kuliko nyingine, labda zinashindana na faida na biashara kama za wagunduzi na wenye biashara ya mitandao kama Facebook, Google na wengine akiwemo Bwana Microsoft, Bill Gates. Mishahara ya kina Paul Pogba, Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Gareth Bale na wengine ni kufuru mbaya kukilinganisha na wanaolipwa wataalam wa nchi za Afrika na hata Ulaya kwenyewe.
Sokani biashara na hakuna nafasi ya kufanya siasa kama zamani. Yapo mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambayo kama kawaida lazima Yanga, Simba na Azam zishiriki.
Ukijiuliza nini madhumuni ya michuano hiyo utajibiwa ni kudumisha Muungano. Kama ni hoja ya Muungano, mbona hazichukuliwi timu zilizoshika nafasi ya saba hadi 12 katika Ligi ya Bara na huko Zanzibar? Kwa nini lazima iwe Yanga, Simba, Azam, Mtibwa na geresha ya klabu kutoka Kenya au Uganda?
Haihitaji uchunguzi kubaini kuwa kiini cha kubuni miradi hii yenye mtazamo wa kisiasa ni dili tu za watu wachache wenye lengo la kutafuta pesa baada ya kuona upepo wa kupiga dili umebadilika.
Kama si kutafuta pesa tu na si Muungano, kwa nini wanaopigia debe michuano hii ambayo kama wanavyokiri wote kuwa haina mtazamo uliokuwepo awali wa kumpata mwakilishi wa Jamhuri, wasipange timu za vijana wa miaka 14, 17 na chini ya 21 kutoka pande zote mbili kuchuana ili, kwanza kuandaa vijana wa timu mahiri za taifa Bara na Visiwani na pili kudumisha Muungano.
Mbona kuna kigugumizi cha kuwa na michuano bila ulazima wa Yanga, Simba na Azam. Kwa nini? Tena hazitakiwi kupeleka timu za vijana ama vikosi vya pili. Ajabu!
Kama ni Muungano, watetezi wa kurudi kwa michuano hii wanaweza kusema timu za kushiriki ni zile zilizoshika nafasi nne za mwisho kwenye ligi zote mbili ili kuziandaa na kuzipa nafasi ya kudumisha Muungano.
Hii itatoa morali kwa timu zinazoshika mkia ambazo hazipati pesa yoyote ya ligi kuu angalau kwenda Unguja, Pemba na za kule kucheza Bara, huku ndiko kudumisha Muungano.
Tanzania pekee tu
Soka si suala la Muungano na wala si kero ya Muungano kiasi cha kutafuta tiba yake kupitia mashindano maalumu yasiyo na shabaha yoyote ile isipokuwa pesa tu. Ulaya, Amerika na Asia hakuna michuano ambayo eti imeanzishwa bila kuwa na malengo mahususi.
Umewahi kusikia Dola au Uingereza ina michuano inayoshirikisha Scotland, Ireland, Wales na England ili kudumisha muungano wao? Au nchi za iliyokuwa Soviet Union kabla ya kuvunjika kulikuwa na michuano kama hiyo.
Kama ni bonanza, ieleweke hivyo lakini ni klabu gani yenye muda wa kupoteza kucheza bonanza lisilo na tija huku likiwagharimia wachezaji wake kwa mbinde.
Yanga inasemekana inatumia hadi Sh1.2 bilioni kwa mwaka kuihudumia timu, imesajili wachezaji kwa zaidi ya Sh 450-500 milioni. Ni busara kweli kuwaingiza wachezaji wake katika mashindano ambayo hayana malengo katika ulimwengu huu wasoka ni biashara na gharama kubwa?
Zipo timu nyingi-Simba, Azam, Mtibwa na karibu zote zilizoshika nafasi nne za juu Bara na Visiwani ambazo hazina hata uwezo wa kuhudumia wachezaji wake, leo mtu anasema zicheze Ligi ya Muungano ambayo hata kama kuna ufadhili hakuna manufaa yoyote.
Kama mdhamini wa Ligi ya Vodacom anatoa zawadi kiduchu ya Sh80 milioni kwa bingwa (tofauti na Afrika ya Kusini ambapo Vodacom ilikuwa ikitoa hadi bilioni 3 kwa bingwa wa PSL). Badala ya kupigania ufadhili uongezeke, wanajadili ligi ambayo haina nafasi miaka hii. Ni Tanzania pekee ambapo watu wanaweza kubuni michuano kila kukicha na inakufa kila uchao kwa sababu tu ni madili ya pesa na yakishatimia, mashindano husika hufifia.
Soka bila malengo ni hatari
Ulipata kusikia Muungano wa Ulaya (EU) umeandaa michuano ya klabu isiyo na malengo yoyote? Msomaji bila shaka unajua zawadi zinazoenda kwa washindi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya au Europa Ligi, ni sawa na bajeti za idara kadhaa za serikali yetu kwa mwaka. Isitoshe, bingwa wa Ligi ya Mabingwa anawakilisha bara hilo kwenye michuano ya klabu bingwa ya dunia.
Ndiyo maana nasema kila mashindano yana malengo yake kibiashara na kisoka. Haya ya Muungano yanayopigiwa debe hayana chembe ya uhalisia wa kuwa itasaidia kukua kwa kiwango cha soka kwa Zanzibar na Bara.
Hakuna asiyejua kiini cha kuporomoka kwa soka Zanzibar, soka ni udhamini, udhamini ukikosekana huwezi kupata ligi ya kufaa.
Tushike wapi, Vijana au Muungano?
Wakati wadau wengi wakisema kila uchao kuwa kiini cha kudorora kwa soka letu ni kukosa mipango madhubuti ya soka kwa watoto na vijana, wengine wanarudia kule kule kulikodhoofisha soka letu kwa kuzikumbatia klabu zile zile ambazo wengine huwa wanadai eti zinavuruga soka la Tanzania.
Huu si wakati wa kuwa na michuano ambayo lengo lake ni kujiburudisha na kutunisha mifuko ya watu fulani tu na siyo klabu. Kama nchi imeishiwa mawazo ya kuukuza mchezo huu Bara na Visiwani ni heri kukaa pembeni miaka mitano ili kutafakari upya tunapojikwaa.
Ni heri kuanzisha michuano ya Tanzania Bara na Zanzibar ili timu ya taifa inayoshinda iwakilishe nchi kwenye michuano ya mataifa ya Fifa na CAF kama tunaona njia hii itadumisha Muungano.
Nguvu zote zinazotumika sasa na wadau na TFF kufanikisha kurudi kwa michuano hii isiyo na hata chembe ya tija, itumike kuweka mfumo wa michuano kwa watoto na vijana wa pande mbili za Muungano kama wanaona kuwa michuano ya Pasaka iliyodumu kwa zaidi ya miongo minne haitoshi kudumisha udugu huo isipokuwa mpaka ziwepo Yanga, Simba na sasa Azam.
Timu za Serengeti Boys na Vijana za Zanzibar zishiriki michuano maalum itakayozikutanisha timu za vijana za klabu za Zanzibar na Bara kwa lengo la kuinua kiwango cha soka la vijana hao na timu hizo ili Zanzibar ipate wawakilishi mahiri zaidi kuliko ilivyo sasa.
Kutolewa kwa klabu za Zanzibar kwenye michuano ya Afrika hakutokani na kutokuwepo Ligi ya Super 8. Tusitafute mchawi wakati sote tunajua kinachomaliza soka la Zanzibar kama ambavyo tunajua kiini cha Taifa Stats kutokwenda AFCON 2017.
Ushauri
Nimalizie kwa kuwataka wenye mapenzi mema na soka kupinga kwa hoja zaidi nia isiyo na maana isipokuwa kupiga pesa tu ili kurudisha Ligi ya Muungano ambayo wala haistahili kuitwa Ligi ya Muungano kwa kuwa neno ligi lina maana yake katika soka yaani kugombea kitu chenye thamani.
Ningekuwa kiongozi wa klabu nne zilizoshika nafasi nne za juu Zanzibar na Bara nisingeruhusu timu itie mguu kwenye michuano hii kwa kuwa haiongezi kipato wala tija kwa klabu inayoshinda badala yake ningeruhusu ishiriki pale tu panapokuwa na tija ya fedha kwanza kwa kutwaa taji la nyumbani kisha likakupa tiketi kupata pesa zaidi Afrika kama Yanga inavyotarajia kupata Shilingi 300 milioni baada ya kushika nafasi ya nne katika kundi lake Kombe la Shirikisho- Hiyo ndiyo michuano yenye tija siku hizi ambapo ni gharama sana kuwahudumia wachezaji.
Kama imeshindikana kudumisha Muungano kupitia Kombe la Mapinduzi ambalo nalo kila wakati lazima Yanga, Simba na Azam ziwepo na ole wao timu hizi zipeleke timu zao za vijana! Linageuka kuwa suala la kisiasa kuwa timu imedharau Mapinduzi matukufu wakati huo huo nchi hizi zikilalama kuwa ni kichwa cha mwenda wazimu.
Wazungu wana msemo kuwa “For everything there is a reason”, yaani kila jambo lina sababu zake.” Nami nasema sababu za kurudishwa Super 8 nimeshaziweka wazi. Ni pesa kwa kwenda mbele si Muungano.
Sylvester Hanga ni mwandishi veteran wa michezo na ameandika na kuchapisha kitabu cha A-Z ya Kandanda Tanzania. [email protected]