Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kariakoo Derby ‘video sapoti’ ndani, sumu kupimwa

Muktasari:

  • TFF imewatangaza waamuzi wa mchezo huo, ambapo Ahmed Arajiga wa Manyara atakuwa mwamuzi wa kati, akisaidiwa na Mohammed Mkono kutoka Tanga, atakayekuwa msaidizi wa kwanza, wakati Leonard Mkumbo akiwa msaidizi wa pili, naye akitokea Manyara.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limethibitisha kwamba katika mchezo wa kesho wa Dabi ya Kariakoo kati ya Yanga dhidi ya Simba, waamuzi wa mchezo huo watakuwa na msaada wa video kuamua matukio ya utata.

TFF imewatangaza waamuzi wa mchezo huo, ambapo Ahmed Arajiga wa Manyara atakuwa mwamuzi wa kati, akisaidiwa na Mohammed Mkono kutoka Tanga, atakayekuwa msaidizi wa kwanza, wakati Leonard Mkumbo akiwa msaidizi wa pili, naye akitokea Manyara.

Taarifa iliyotolewa na TFF ni kwamba waamuzi hao wote watasaidiwa na teknolojia maalum ya Football Video Support (FVS), kuwasaidia kuamua matukio ya utata kwenye mchezo huo utakaopigwa kesho katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Bosi mmoja wa juu wa TFF ameongeza kuwa waamuzi wote watakaochezesha mchezo huo wamefanya vizuri kwenye mafunzo ya kutumia teknolojia hiyo.

Bosi huyo ameongeza kuwa waamuzi hao watakuwa wanafuatiliwa na wakufunzi waliowafundisha mafunzo hayo, kupima uwezo wao kabla ya teknolojia hiyo kuanza kutumika kwenye mechi zingine za Ligi kwa msimu ujao.

“Ndiyo, FVS itakuwepo na hawa waamuzi, nikwambie, ni kati ya wale waliofanya vizuri kwenye mafunzo haya ambayo yamekuwa yakiendeshwa na wakufunzi kutoka nje,” amesema bosi huyo.

“Hata wale wakufunzi waliokuwa wanawafundisha nao watakuwa wanafuatilia kila kitu juu ya kitakachoamuliwa na waamuzi hawa. Tunataka kuona mechi kubwa kama hii inaamuliwa kwa haki kwa kiwango kikubwa.”

Mbali na teknolojia hiyo, ambayo haitofautiana sana na VAR, pia klabu hizo za Simba na Yanga zimeletewa vifaa maalum ambavyo vitatumika kupima hewa yenye sumu vyumbani.

Bosi huyo amesema kuwa vifaa hivyo vimetwa nchini na kukabidhiwa na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), ambapo vitaanza kutumika kwenye mchezo huo endapo timu moja itahofia usalama wa vyumbani.

“Sio tu kuhusu FVS, pia yale mambo ya kukimbia vyumba hayatatokea kwenye mchezo kuanzia huu wa kesho. Tumeshanunua vifaa vya kisasa vitakavyotupa majibu ya haraka kwenye zile tuhuma za kupuliziana dawa vyumbani.

“Hivi vifaa vimeshakuja nchini na hapa Zanzibar pia vimeshafika. Kesho timu yoyote ikisema kuna hewa hawaielewi, tutapima. Tukikuta ni kweli tutachukua hatua, tukiona hakuna tutawajibu hakuna. Wakikaidi, tutatumia kanuni.”

TFF imeweka kanuni ambapo timu itakayokimbia kutumia vyumba maalumu vya kubadilishia nguo  itakatwa pointi tano kwenye ligi.