Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Stumai Abdallah: Sina mimba, napambana na jeraha!

STUMAI Pict

Muktasari:

  • Stumai aliandika ujumbe huo kwenye mitandao yake ya kijamii, akisimulia namna jeraha hilo lilivyomuweka mbali na wenzake, mashabiki na furaha ya kuvaa jezi ya timu yake. Alieleza kuwa kipindi hicho kimeambatana na maumivu, changamoto na nyakati ngumu ambazo si rahisi kuzisimulia.

“SINA MIMBA,” ni ujumbe aliouandika mshambuliaji wa JKT Queens, Stumai Abdallah, katika kueleza changamoto anazopitia kwa takribani misimu miwili akiwa nje ya uwanja kutokana na jeraha linalomzuia kufanya kitu anachokipenda zaidi, kucheza soka.

Stumai aliandika ujumbe huo kwenye mitandao yake ya kijamii, akisimulia namna jeraha hilo lilivyomuweka mbali na wenzake, mashabiki na furaha ya kuvaa jezi ya timu yake. Alieleza kuwa kipindi hicho kimeambatana na maumivu, changamoto na nyakati ngumu ambazo si rahisi kuzisimulia.

Mshambuliaji huyo alisema pamoja na changamoto hizo, upendo wake kwa soka haujabadilika na bado ana ndoto ya kurejea uwanjani, licha ya kutokuwa na uhakika wa lini atakuwa tayari kuungana tena na wenzake.

STUMA 01

“Nyuma ya ukimya wangu kumekuwa na maumivu, changamoto, kujitoa mhanga na nyakati nyingi ambazo si rahisi kuzisimulia. Kuna siku zimekuwa ngumu sana, lakini pamoja na yote, jambo moja halijawahi kubadilika; upendo wangu kwenye mpira na ndoto yangu ya kurejea tena uwanjani,” aliandika Stumai.

Katika ujumbe huo, Stumai pia alieleza namna alivyoguswa na kitendo cha JKT Queens kuweka jezi yake uwanjani kama ishara ya kumkumbuka na kutambua mchango wake ndani ya timu. Alisema kitendo hicho kimemkumbusha miaka aliyoitumikia klabu hiyo, jasho alilomwaga na kumbukumbu walizotengeneza pamoja.

“Nimeumia, nimepitia mengi, nimekuwa na nyakati za kukata tamaa, lakini bado nina ndoto, bado nina imani na bado nina sababu ya kupigana,” aliandika Stumai, akieleza matumaini yake ya siku moja kuivaa tena jezi ya JKT Queens.


STUMA 02

WANASOKA WAMUUNGA MKONO

Ujumbe wa Stumai umegusa wachezaji na wadau mbalimbali wa soka, ambao wamemtumia salamu za kumtia moyo na kumtakia apone ili arejee uwanjani.

Kiungo wa zamani wa Yanga Princess, Simba Queens na JKT Queens, ambaye kwa sasa anakipiga Mashujaa Queens, Maimuna Hamis ‘Mynaco’, aliandika ujumbe mrefu wa kumfariji mshambuliaji huyo.

“Wala sijamalizia kusoma ujumbe wako umenitoa machozi. Allah hakupi mtihani ambao huwezi kuumudu. Naamini kuna kila sababu ya hili unalopitia kwa sasa ili upokee kilicho bora zaidi ya jana, na utarejea ukiwa imara kuliko siku zote.

“Wewe ni mchezaji unayejituma sana, unayecheza kwa uchungu na mpambanaji sana. Mpaka umefika hapo si kwa kubebwa, huna hata mia ya urithi, vyote ni vyako na umetafuta kwa jasho lako mwenyewe! Najivunia wewe sana Stumai. Nakupenda sana pia, utarejea ukiwa imara,” aliandika Mynaco.

Aliyekuwa kocha wa Yanga Princess, Edna Lema, naye alimpa moyo kwa kuandika: “Utarudi ukiwa imara mwanangu, hiyo ndiyo nimeipenda.”

Mshambuliaji wa Brighton & Hove Albion, Aisha Masaka, aliandika: “Pona haraka, dada. Nakutumia kumbatio kubwa kutoka kwangu.”

Naye nyota wa JKT Queens, Asha Mwalala, aliandika: “Na hiyo mimba siyo ugonjwa, ni baraka kubwa sana kutoka kwa Allah. Watu walijue hilo.”


STUMA 03

REKODI ZAKE

Katika misimu aliyoiitumikia JKT Queens, Stumai amekuwa miongoni mwa washambuliaji waliokuwa na uwezo mkubwa wa kufunga mabao, akionyesha kiwango kizuri katika misimu kadhaa kabla ya kukabiliwa na majeraha.

Msimu wa 2019/20 alicheza mechi 18 na kufunga mabao 22, kabla ya msimu uliofuata kucheza mechi tatu na kufunga mabao saba.

Msimu wa 2021/22 alikaa nje ya uwanja akiuguza jeraha la goti. Alirejea msimu wa 2022/23 na kufunga mabao 14 katika mechi tisa, wakati Jentrix Shikangwa wa Simba Queens akitwaa kiatu cha dhahabu.

Msimu wa 2023/24, Stumai alicheza mechi 18 na kufunga mabao 19, kabla ya kufanya vizuri zaidi msimu wa 2024/25 alipofunga mabao 27 katika mechi 18 na kuwa mfungaji bora.

Hata hivyo, msimu wa 2025/26 alicheza mechi 10 pekee na kufunga bao moja.

Rekodi ya Stumai Abdallah

2019-2020 - mechi 18, mabao 22

2020-2021 - mechi 3, mabao 7

2021-2022 - hakucheza alikuwa majeruhi

2022-2023 - mechi 9, mabao 14

2023-2024 - mechi 18 mabao 19

2024-2025 - mechi 18 mabao 27

2025-2026 - mechi 10, bao 1