Alliance inazitaka pointi 12 nyumbani
KOCHA wa Alliance Girls, Sultan Juma amesema ushindi katika mechi nne za nyumbani zilizosalia kwenye mzunguko wa kwanza unaweza kuiweka timu hiyo katika nafasi nzuri ya kujiondoa kwenye presha ya vita ya kusaka kubaki Ligi Kuu ya Wanawake (WPL).
Sultan amesema anaamini Alliance inaweza kuepuka presha katika hatua za mwisho za ligi ikiwa itatumia vizuri michezo yake ya nyumbani, akisisitiza kuwa matokeo mazuri katika mechi hizo yatakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha nafasi yao kwenye msimamo.
Kocha huyo amesema ushindi wa mechi mbili mfululizo walioupata hivi karibuni ni hatua muhimu kwa kikosi hicho, hasa ikizingatiwa kuwa kimekuwa katika kipindi cha kujijenga upya msimu huu baada ya kuondokewa na baadhi ya wachezaji muhimu.
“Unajua kwenye soka la wanawake ni mahesabu na mipango. Tumekuwa na wakati mzuri mechi mbili za mwanzo, lakini ukipiga hesabu tukishinda mechi nne zote nyumbani, tunakwenda kupambana raundi ya pili tu.”