Omar Bakari kuinoa Uhamiaji kwa muda
Muktasari:
- Katika michezo mitano iliyosalia kumaliza mzunguko wa kwanza, Uhamiaji itakutana na Black Sailors, Muembe Makumbi, Mlandege, Kipanga na Zimamoto. Uhamiaji inashika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 16 baada ya kushinda mechi tano, sare moja na kupoteza nne.
WAKATI Uhamiaji ikiendelea na mchakato wa kutafuta kocha mpya baada ya kuvunja benchi lote la ufundi, timu hiyo imesema kwa sasa itaongozwa na kocha wa muda, Omar Bakari Mohammed.
Kauli hiyo ilitolewa na Ofisa Habari wa timu hiyo, Mwinyi Hamad, wakati akizungumza na Mwanaspoti katika Uwanja wa Mao Zedong, Unguja.
“Mchakato wa kumtafuta kocha unaendelea na katika kipindi hiki, kocha wa muda atakuwa Omar Bakari Mohammed ambaye atamalizia michezo mitano iliyobaki hadi dirisha dogo la usajili,” amesema. Ofisa huyo amesema Omar alianza majukumu yake katika mchezo wa Novemba 4, 2026, dhidi ya KVZ, uliomalizika kwa sare ya bila kufungana.
Amesema wakati mchakato wa kumpata kocha mpya ukiendelea, timu hiyo pia inaendelea kujipanga na kuimarisha maeneo ambayo bado hayajakaa vizuri kwa lengo la kurejea katika ubora wake. Mwinyi aliwaomba mashabiki na wadau wa timu hiyo kuendelea kuwa na imani na kikosi hicho kwa kukiunga mkono, akisisitiza kuwa bado hakijatoka katika malengo yake.
Katika michezo mitano iliyosalia kumaliza mzunguko wa kwanza, Uhamiaji itakutana na Black Sailors, Muembe Makumbi, Mlandege, Kipanga na Zimamoto. Uhamiaji inashika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 16 baada ya kushinda mechi tano, sare moja na kupoteza nne.