Soka letu, wiki moja ujinga mara tatu
Muktasari:
Wiki ilianzia kwa Mwinyi Kazimoto kumpiga Mwandishi wa habari, Mwanahiba Richard pale Shinyanga. Mwinyi aliambiwa na washkaji zake kuwa Mwanahiba alikuwa amemwandika vibaya. Ilikuwa wakati ule Simba inafanya vibaya na Kazimoto akawa mmoja kati ya wachezaji walioohojiwa na viongozi wake kwa kucheza chini ya kiwango.
FIKIRIA maisha yangekuwaje bila ya soka la Ulaya. Ingekuwa vipi kama tungekuwa tunafuatilia upuuzi wa soka la Tanzania tu bila ya kutupia macho soka tamu la Ulaya. Tungehitaji Panadol kufuatilia upuuzi unaofanyika kila siku katika soka la Bongo.
Wiki ilianzia kwa Mwinyi Kazimoto kumpiga Mwandishi wa habari, Mwanahiba Richard pale Shinyanga. Mwinyi aliambiwa na washkaji zake kuwa Mwanahiba alikuwa amemwandika vibaya. Ilikuwa wakati ule Simba inafanya vibaya na Kazimoto akawa mmoja kati ya wachezaji walioohojiwa na viongozi wake kwa kucheza chini ya kiwango.
Huyu ni Mwinyi Kazimoto. Rafiki yangu asiyejitambua sana. Katika dunia ya leo mwanamke huwa hapigwi. Hata kama si mwandishi lakini mwanamke huwa hapigwi. Hilo ni jambo moja. Lakini jambo la pili ni kwamba katika soka kushuka kiwango ni kitu cha kawaida.
Kazimoto anadhani ameonewa kwa kuambiwa ameshuka kiwango. Ajiulize, kwa nini hayupo katika kikosi cha timu ya taifa na mashabiki wala hawapigi debe? Miezi 24 iliyopita alikuwa mchezaji wa kudumu katika kikosi cha Taifa Stars kwa nini leo hayupo?
Hata hivyo, ni Mwanahiba huyu huyu na waandishi wengine ndio waliokuwa wakipiga debe Kazimoto aitwe na kocha Marcio Maximo baada ya kuonyesha kiwango murua katika michuano ya Kombe la Taifa akiwa na timu ya Mkoa wa Pwani mwaka 2008. Wakati huo mbona hakupiga mwandishi?
Pamoja na yote, Mwinyi anawakilisha tu upuuzi wa wanasoka wetu kutotambua kuwa soka ni maisha yao. Wanasoka wetu wanaamini kuwa soka ni burudani tu ndio maana wanaweza kufanya mambo mazito kwa wepesi mkubwa.
Kwa Ulaya, mchezaji kama Kazimoto anafungiwa miaka miwili, anapoteza wadhamini wake binafsi, anafukuzwa katika timu. Anaharibu maisha. Ndio maana pamoja na hasira zao, hawa kina Wayne Rooney hawawezi kurusha ngumi. Soka ni maisha.
Ndani ya wiki hii hii iliyopita, Yanga imechelewa kwenda Mauritius kucheza pambano lao la michuano ya Caf. Wameingia Mauritius usiku wa manane kwa ajili ya pambano hilo na wakacheza mechi ndani ya saa chache kisha wakageuza kwao.
Ni kwa vile inaonekana wapinzani wao hawakuwa katika ubavu wa kushindana na Yanga ndio maana wakashinda. Lakini kama Yanga ingekuwa inacheza na timu yenye ushindani mkubwa kisoka, ni wazi kwamba maandalizi yao yalikuwa ya ovyo kuelekea katika mechi hii na wangeweza kupoteza kirahisi.
Wachezaji wa Yanga walisota Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam. Wakasafiri usiku na kukosa usingizi mzuri, wakalazimika kuzoea hali ya hewa ya Mauritius kwa muda mfupi kabla ya mechi. Haya siyo maandalizi sahihi kwa timu inayoshiriki mechi ya Ligi ya Maingwa ya Afrika.
Ratiba ya mechi hii imejulikana miezi miwili iliyopita na Yanga ilipaswa kujua mapema kuhusu maandalizi ya safari yake. Napata mashaka kuamini kuwa Yanga ingejiandaa hivi kama ingekuwa inacheza na Zamalek, Etoile du Sahel, TP Mazembe au wengineo.
Wakati Donald Ngoma akiipatia Yanga bao pekee la ushindi dakika ya 17 ya pambano hilo, kule Kigoma na Tabora timu za Daraja la Kwanza zilikuwa zinashindana kupanga matokeo uwanjani. Geita Gold ilikuwa inaishindilia JKT Kanembwa mabao 8-0 huku Polisi Tabora ikiishindilia JKT Oljoro mabao 7-0.
Ilitakiwa timu moja yenye mabao zaidi na hiki ndicho kilichotokea. Imetokea aibu kwa taifa na wala hatuhitaji darubini kujua kuwa mechi zina dalili ya kupangwa. Na aibu zaidi ni kwamba timu tatu zilizohusika ni za majeshi yetu.
Aibu hii inaliangukia taifa wakati huu Rais Mpya, John Magufuli akijaribu kulitengeneza taifa linalojali. Kinachoonekana ni kwamba bado kuna taasisi nyingi nchini hazielewi kile ambacho Magufuli anajaribu kukifanya na ndio maana bado mambo yanaenda ovyo ovyo.
Kwanza kabisa kuna ukweli kwamba kuna mabosi wa TFF walikuwa na timu zao ambazo walitaka zipande. Hili la matokeo ya mwisho ni umaliziaji tu wa upuuzi mwingi ambao umefanyika katika mechi za Daraja la Kwanza msimu huu na msimu uliopita.
Wajumbe wa Kamati za Utendaji walikuwa na timu za kutoka mikoa yao ambazo walitaka zipande. Vurugu nyingi zipo huko kwa sababu watu hawafuatilii sana Daraja la Kwanza. TFF nayo imekaa kimya kwa sababu haipati presha kubwa kama inavyopata katika upuuzi ambao huwa unafanyika Ligi Kuu. Matokeo haya ya mwisho yanakupa swali dogo tu. Timu hizi zimepata wapi ujasiri wa huo na kusababisha aibu kama hayo? Kuna wakati mwanadamu anaweza kupata ujasiri wa kupanga matokeo ya 3-0, lakini katika zama hizi unapata wapi ujasiri wa (kinachoonekana) kupanga matokeo ya 8-0 au 7-0 . Ilikuwa wiki moja lakini ambayo imejaa ujinga mwingi.