Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sintofahamu ya UONGOZI TOC yatia neno

TOC Pict

Muktasari:

  • Kauli ya Nasra imekuja siku mbili baada ya Leonard Thadeo Katunzi, aliyetangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo, kutangaza kujiuzulu nafasi hiyo kwa madai kuwa uchaguzi ulifanyika kinyume na Ibara ya 9 ya Katiba ya TOC ya mwaka 2026.

BAADA ya sintofahamu ya zaidi ya mwezi mmoja kuhusu nani anastahili kuwa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Makamu wa Rais wa kamati hiyo, Nasra Juma Mohammed, amesema Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) imemtambua Anthony Mtaka kuwa ndiye rais aliyechaguliwa kihalali.

Kauli ya Nasra imekuja siku mbili baada ya Leonard Thadeo Katunzi, aliyetangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo, kutangaza kujiuzulu nafasi hiyo kwa madai kuwa uchaguzi ulifanyika kinyume na Ibara ya 9 ya Katiba ya TOC ya mwaka 2026.

Thadeo alikuwa miongoni mwa wagombea watatu wa nafasi ya urais katika uchaguzi uliofanyika Julai 5, 2026 jijini Dar es Salaam, ambao uliibua mvutano baada ya Kamisheni ya Uchaguzi kumtangaza kuwa mshindi, huku baadhi ya wajumbe wakipinga matokeo na kudai kuwa Mtaka ndiye aliyeshinda.

Akizungumza na Mwanaspoti Agosti 16, 2026, Nasra amesema suala la uchaguzi wa uongozi wa TOC limekamilika na kwamba IOC inamtambua Mtaka kama rais wa kamati hiyo na tayari imeanza kufanya naye kazi, hivyo hakuna sababu ya Thadeo kuendelea kuibua sintofahamu kuhusu uongozi uliopo.

Amesema taratibu zote za uchaguzi zilifuatwa na tayari TOC imeanza majukumu yake chini ya rais Mtaka ambaye ndiye anayetambuliwa na IOC Kauli hiyo imekuja wakati Thadeo akieleza kujiuzulu nafasi ya rais na kudai kuwa uamuzi wake wa kujiuzulu umetokana na msimamo wake kwamba uchaguzi huo haukufuata matakwa ya Ibara ya 9 ya Katiba ya TOC.

Thadeo amesema kwa mtazamo wake, dosari hiyo inafanya viongozi wote waliochaguliwa katika mkutano huo kutokuwa halali akidai alipochaguliwa aliapa kuitetea na kuilinda Katiba ya TOC, hivyo hawezi kuendelea kushikilia nafasi ambayo anaamini alipatikana kwa mchakato usiofuata Katiba.

Alidai utambuzi wa viongozi hao kwa mamlaka za ndani au taasisi za kimataifa hauwezi kuufanya mchakato huo kuwa halali ikiwa chanzo chake kilikuwa na dosari.

Hata hivyo, Nasra amesema uongozi wa TOC ni halali na Thadeo hakushinda kihalali kwenye mchakato huo akibainisha kwamba walioshinda wanatambulika na uongozi wao umekabidhiwa ofisi na uongozi uliopita kuendelea na majukumu ya kuendesha gurudumu hilo.

Kwa upande wake, aliyekuwa katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi, amesema katika uchaguzi kulikuwa na mwangalizi wa kimataifa aliyeshuhudia zoezi zima na ambaye alipaswa kuwasilisha ripoti yake kuhusu mwenendo wa mchakato huo.

“Ndiyo sababu hata kwenye utaratibu wa makabidhiano ya madaraka na namna viongozi wapya walivyotakiwa kutambuliwa baada ya uchaguzi sisi tulikabidhi kwa makamu (Nasra), kuhusu uhalali wa Mtaka kuwa rais hilo lipo chini ya BMT (Baraza la Michezo la Taifa) na uongozi mpya ambao mawasiliano yao ndiyo yapo IOC,” amesema Bayi.

Katibu Mkuu wa BMT, Neema Msitha, alipoulizwa kuhusiana na hilo, aliomba atumiwe ujumbe mfupi (SMS), alipotumiwa hakujibu hadi habari hii inachapishwa.

Uchaguzi wa TOC uliofanyika Julai 5, 2026 jijini Dar es Salaam.