IOC, ANOCA zamthibitisha Anthony Mtaka kuwa Rais wa TOC
Muktasari:
- Katika barua rasmi iliyoandikwa Julai 9, 2026, kutoka Lausanne, Uswisi, IOC na ANOCA zimethibitisha kuwa Anthony Mtaka amechaguliwa kuwa Rais mpya wa TOC baada ya kupata ushindi wa kishindo wa kura 29 kati ya 36 zilizopigwa. Uchaguzi huo uliofanyika Julai 5, 2026, katika hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam, ulishuhudiwa na mwangalizi huru kutoka IOC na ANOCA.
Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) na Chama cha Kamati za Kitaifa za Olimpiki Afrika (ANOCA), zimeidhinisha rasmi matokeo ya Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) uliofanyika hivi karibuni, huku zikitoa onyo kali dhidi ya vitendo vya udanganyifu vilivyojitokeza wakati wa mchakato huo.
Katika barua rasmi iliyoandikwa Julai 9, 2026, kutoka Lausanne, Uswisi, IOC na ANOCA zimethibitisha kuwa Anthony Mtaka amechaguliwa kuwa Rais mpya wa TOC baada ya kupata ushindi wa kishindo wa kura 29 kati ya 36 zilizopigwa. Uchaguzi huo uliofanyika Julai 5, 2026, katika hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam, ulishuhudiwa na mwangalizi huru kutoka IOC na ANOCA.
Pamoja na Rais Mtaka, safu mpya ya uongozi iliyothibitishwa inamjumuisha Nassra Juma Muhammed kama Makamu wa Rais. Wajumbe waliochaguliwa kuunda Kamati ya Utendaji ni Abdulrahman Said Simai, Makame Ally Machano, Thuwaiba Aboud Muhiddin, Mwatima Bakari Abdi, Noorain Gulam Hussein Shariff, Amina Mohamed Mfaume, Khalid Yahya Rushaka, Suma Steven Mwaitenda, Abdulkheir Ahmed Mohammed na Said Mohamed Abdullah.
Licha ya kuwapongeza viongozi hao wapya, IOC na ANOCA zimeonyesha kushtushwa na ripoti za jaribio la dakika za mwisho la Kamati ya Uchaguzi ya TOC kutaka kuchafua matokeo ya urais.
Taarifa hiyo imeeleza kulikuwa na njama za kutaka kumtangaza mgombea ambaye hakuwa ameshinda, kitendo ambacho kimetajwa kama ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya Olimpiki na kanuni za kimaadili.
"Tunalaani vikali vitendo hivi vya kitapeli ambavyo vinaenda kinyume na makubaliano yaliyofikiwa kati ya IOC, TOC, na mamlaka za serikali ili kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki," imeeleza barua hiyo iliyotiwa saini na James Macleod ambaye ni Mkurugenzi wa Mahusiano ya NOC na Rais wa ANOCA, Mustapha Berraf.
IOC imeagiza uongozi mpya chini ya Anthony Mtaka kufanya uchunguzi wa kina kuhusu jaribio hilo la udanganyifu na kuchukua hatua stahiki, ikiwa ni pamoja na kutoa adhabu kwa watu waliohusika ili kulinda heshima ya michezo nchini Tanzania.
Aidha, uongozi uliopita wa TOC umetakiwa kukabidhi mali na rasilimali zote za kamati mara moja, ikiwa ni pamoja na ofisi, akaunti za benki, tovuti, barua pepe rasmi na kurasa za mitandao ya kijamii. Makabidhiano hayo yametakiwa kufanyika bila ucheleweshaji ili kuruhusu timu mpya kuanza maandalizi ya michezo na matukio muhimu yanayokuja.
Mamlaka hizo za kimataifa zimesisitiza umuhimu wa umoja na maelewano ndani ya TOC kwa ajili ya maslahi ya wanamichezo wa Kitanzania na harakati za Olimpiki kwa ujumla.
Ikumbukwe kuwa, uchaguzi huo uliokumbwa na utata mwingi, Leonard Thadeo alitangazwa kuwa mshindi, matokeo ambayo wajumbe waliyagomea huku mawakala wa wagombea wakidai Thadeo alipata kura moja, huku Henry Tandau akiambulia kura saba na Mtaka kura 29.