Simba yanasa beki Zimbabwe
Muktasari:
KIKOSI cha Simba kilitua jioni ya jana nchini kutoka Zimbabwe, kilikoteza kwa bao 1-0 dhidi ya FC Platinum katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini hakijarudi patupu kwani mkononi wana jina la beki wa kati wa timu ya taifa ya Zimbabwe ili kuimarisha kikosi.
KIKOSI cha Simba kilitua jioni ya jana nchini kutoka Zimbabwe, kilikoteza kwa bao 1-0 dhidi ya FC Platinum katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini hakijarudi patupu kwani mkononi wana jina la beki wa kati wa timu ya taifa ya Zimbabwe ili kuimarisha kikosi.
Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti limezipata ni kuwa mabosi wa Simba wamefanya mazungumzo na beki huyo kwa ajili ya kumnasa kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo baada ya jina lake kupendekezwa na kocha Sven Vandenbroeck.
“Wakiwa Zimbabwe, viongozi walioambatana na timu akiwamo kocha walipata fursa ya kutazama mechi mbili za mazoezi za timu ya taifa ya Zimbabwe inayojiandaa na Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) na Sven akamuona beki huyo na kuvutiwa naye,” kilisema chanzo kutoka ndani ya Simba.
“Na katika kujiridhisha zaidi, waliwasiliana na kocha wa timu ya Taifa ya Zimbabwe, Zdravko Logarusic aliyewahi kuinoa Simba ambaye aliwahakikishia kuwa beki huyo ni mzuri na atakuwa msaada mkubwa kwao katika safu ya ulinzi kutokana na uzoefu na uwezo wake mkubwa.”
Inadaiwa mazungumzo baina ya Simba na beki huyo yamefikia pazuri yakichagizwa na ushawishi wa kiungo wa zamani wa Simba, raia wa Zimbabwe, Justice Majabvi ambaye wawakilishi hao wa Tanzania walipotua nchini humo alikuwa nao sambamba. Majabvi alipotafutwa na Mwanaspoti kuelezea juu ya dili la beki huyo alikataa kusema lolote, lakini licha ya usiri unaofanywa juu ya dili la beki huyo, Mwanaspoti linafahamu kikosi cha Zimbabwe kinachojiandaa na mashindano ya Chan kina mabeki wanne wa kati wanaochezea klabu tatu tofauti nchini humo.
Mabeki hao ni Patson Jaure (30) anayechezea Dynamos ya Zimbabwe ambaye ni nahodha wa timu ya taifa na Frank Makarati (26) ambaye ni nahodha wa Ngezi Platinum ya nchini humo.
Pia wapo mabeki wawili wa Highlanders ambao ni Peter Maduwa (27) na Andrew Mbeba (20).
Hata hivyo, kati ya majina hayo manne, Jaure huenda ndiye mlengwa kwani anayechezea Dynamos FC, timu ambayo Majabvi ana ukaribu nayo akiwa amewahi kuichezea mechi 84 na kuifungia mabao 14 kuanzia 2006 hadi 2008.
Simba imekuwa ikihaha kusaka beki wa kati mwenye nguvu na kasi kutokana na mabeki waliopo kushindwa kukabiliana na washambuliaji wenye nguvu na kasi, jambo ambalo limekuwa likisababisha timu kuruhusu mabao pindi wakutanapo na timu zenye washambuliaji wenye sifa hizo.
Katika mchezo wao waliopoteza mbele ya FC Platinum, Perfect Chikwende alifunga bao baada ya kumzidi ujanja Pascal Wawa kwa kumzidi mbio na kumpora mpira kabla ya kumtungua kipa Aishi Manula, jambo lililowatibua mashabiki wa Simba wakitaka aletwe beki mwingine mkali.
Mbali na Wawa, mabeki wengine wa kati ni Joash Onyango, Kennedy Juma na Ame Ibrahim aliyesajiliwa msimu huu kutokea Coastal Union.