Simba Queens yatoa mwelekeo CECAFA
Muktasari:
- Michuano ya Cecafa inatarajiwa kuanza Agosti 21,2026 nchini Rwanda huku bingwa wa akiwa na nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
KOCHA msaidizi wa Simba Queens, Mohamed Mrishona ‘Xavi’ amesema timu yake inaendelea kujifua kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Cecafa ambayo itawapa nafasi ya kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Michuano ya Cecafa inatarajiwa kuanza Agosti 21,2026 nchini Rwanda huku bingwa wa akiwa na nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania kwa msimu uliopita imekuwa kwenye maandalizi kabambe kwa kipindi cha wiki mbili sasa ikiwa imepania kufanya mambo makubwa kwenye michuano hiyo msimu huu.
Akizungumzia maandalizi hayo Xavi ambaye ni mmoja wa makocha wa timu hiyo amesema hadi sasa yanaendelea vizuri na wachezaji wanaimarika siku hadi siku.
“Nimekuja huku ili kuongeza nguvu baada ya kuwa kwenye timu ya wanaume kwa msimu uliopita. Mbali na mazoezi tunayofanya, lakini tunacheza mechi za kirafiki ili kuwapa wachezaji kipimo sahihi kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Cecafa.
“Hivi karibuni tumecheza mchezo dhidi ya Mathare United ya Kenya na kutoka suluhu, mchezo huu umekuwa na msaada mkubwa kwetu na umezidi kutuonyesha kuwa nini tunatakiwa kufanya kwa siku hizi zilizobaki,” amesema kocha huyo mtaalamu wa viungo.
Akizungumzia mahudhurio ya wachezaji kambini, Xavi amesema kuwa bado siyo wachezaji wote wameweza kufika kwa kuwa wengine wapo na timu zao za taifa, lakini hili halizuii maandalizi yao.
“Siku chache zijazo tutaitengeneza timu vizuri kwenye upande wa utimamu wa mwili na mbinu, ili kuandaa timu itakayoiwakilisha vyema Tanzania kwenye michuano hiyo ya Cecafa,” amesema Xavi ambaye ni msaidizi wa Mussa Mgosi ambaye ndiye kocha mkuu wa timu hiyo.
Timu zitakazoshiriki michuano hiyo ni 10 ikiwamo Simba Queens ya Tanzania, Rayon Sports ya Rwanda, Kenya Police Bullets, CBE ya Ethiopia, pamoja na Kawempe Muslim Ladies FC, Top Girls Academy FC ya Burundi, Djibouti FC Ujeco, Eritrea ni Denden FC, Sudan Kusini itawakilishwa na Yei Joint Stars FC na Zanzibar ni Mafunzo SC.