Simba Queens kujipima kwa Mathare
Muktasari:
- Mechi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya Simba Queens kuelekea michuano ya kuwania kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, ambapo timu hiyo inaiwakilisha nchi katika hatua ya mchujo wa ukanda wa CECAFA.
MABINGWA wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, Simba Queens, leo Agosti 13, 2026 wanatarajiwa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mathare United Women katika Uwanja wa Dandora, Nairobi nchini Kenya, kuanzia saa 10:00 jioni.
Mechi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya Simba Queens kuelekea michuano ya kuwania kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, ambapo timu hiyo inaiwakilisha nchi katika hatua ya mchujo wa ukanda wa CECAFA.
Kwa upande wa Mathare, ni mechi ya kujipima nguvu kuelekea msimu mpya wa Ligi ya Wanawake nchini Kenya inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Kupitia taarifa iliyotolewa na timu hiyo, mechi hiyo ilipaswa kuchezwa jana Agosti 12, 2026 lakini iliahirishwa kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi.
“Mechi yetu iliyokuwa ichezwe leo dhidi ya Simba Queens ya Tanzania katika Uwanja wa Dandora, imeahirishwa na sasa itachezwa kesho (leo),” ilisema taarifa hiyo ya Mathare.
Simba imeweka kambi ya siku saba nchini Kenya kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya CECAFA ambayo inatarajiwa kuanza Agosti 21 hadi Agosti 29, 2026 nchini Rwanda.
Timu hiyo imepangwa kundi C pamoja na Kenya Police Bullets ya Kenya na Top Girls ya Burundi, huku kundi A likiwa na Rayon Sports ya Rwanda, Yei Joints ya Sudan Kusini, Mafunzo SC ya Zanzibar na Denden FC ya Eritrea. Kundi B lipo na CBE ya Ethiopia, Kawempe Ladies ya Uganda na FC Ujeco ya Djibouti.
Tangu mashindano ya CECAFA yaanzishwe mwaka 2021 huku Vihiga Queens ikibeba ubingwa huo kwa mara ya kwanza, Simba Queens imeshiriki mara mbili, mwaka 2022 na 2024. Kwenye ushiriki wake wa kwanza, Simba Queens iliandika rekodi ya kuwa bingwa wa kwanza CECAFA kutoka Tanzania na kufuzu Ligi ya Mabingwa.
Kwenye Ligi ya Mabingwa iliandika pia rekodi ya kucheza nusu fainali ya michunao hiyo mikubwa Afrika, rekodi ambayo haijavunjwa hadi sasa na timu kutoka ukanda wa CECAFA ambazo ni Vihiga Queens, JKT Queens, CBE zote zikiishia hatua ya makundi.