Simba Queens kuweka kambi Kenya
Muktasari:
- Simba itakaa takriban siku saba Kenya na mbali na kufanya mazoezi, kikosi hicho kinatarajiwa kupata michezo ya kirafiki kwa ajili ya kujiweka tayari kabla ya kuanza kwa mashindano ya CECAFA.
KESHO Agosti 11 mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Wanawake Bara, Simba Queens inatarajia kwenda Kenya kwa ajili ya kuweka kambi ya maandalizi ya mashindano ya Kombe la Afrika Mashariki kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba itakaa takriban siku saba Kenya na mbali na kufanya mazoezi, kikosi hicho kinatarajiwa kupata michezo ya kirafiki kwa ajili ya kujiweka tayari kabla ya kuanza kwa mashindano ya CECAFA.
Ikumbukwe bingwa mtetezi wa mashindano ya CECAFA ni JKT Queens ya Tanzania na mwaka huu michuano hiyo itafanyika Rwanda kuanzia Agosti 21 na hadi Agosti 29.
Simba imepangwa Kundi C pamoja na Kenya Police Bullets ya Kenya na Top Girls ya Burundi, hivyo inahitaji maandalizi ya kutosha kabla ya kuanza safari yao ya kusaka taji la pili.
Akizungumzia safari hiyo, beki wa kushoto, Hellen Kutsanedzi amesema kambi hiyo itawasaidia wachezaji kujiandaa vizuri kabla ya kuanza michuano hiyo.
"Nafikiri ni kitu kizuri sana kwa sababu michuano mikubwa kama hiyo inahitaji maandalizi ya kutosha ili kujiweka sawa, tunaamini tutakuwa na mashindano mazuri," amesema Kutsanedzi.
Beki huyo aliyesajiliwa hivi karibuni akitokea Epiphany Warriors ameongeza ni fahari kwake kucheza michuano ya CECAFA kwa mara ya kwanza kwani ni fursa kwa wachezaji kuonekana kimataifa.
"Zinakutana timu nyingi lakini kuna mawakala, viongozi wa timu tofauti hivyo unapofanya vizuri ni fursa naahidi kutoa mchango mkubwa kwa ajili ya timu ili ifanye vizuri."