Safari ya soka la Okwi hadi Simba, sasa imefika mwisho
Muktasari:
- Pembeni ya eneo la mapokezi, Emmanuel Arnold Okwi anaketi kwa utulivu akiwa na tabasamu lilelile ambalo mashabiki wa Simba walilizoea kwa miaka mingi. Tofauti pekee ni safari hii hakuwa amevaa jezi ya mazoezi wala hakutarajia kuingia uwanjani tena.
ILIKUWA Jumatano ya Agosti 5, 2026 kwenye moja ya hoteli yenye hadhi kubwa jijini Kigali wakati wachezaji wa Simba walikuwa wakiendelea na maandalizi ya safari ya kurejea Tanzania, kwa ajili ya Tamasha la Simba Day baada ya kumaliza kambi yao ya maandalizi nchini Rwanda.
Pembeni ya eneo la mapokezi, Emmanuel Arnold Okwi anaketi kwa utulivu akiwa na tabasamu lilelile ambalo mashabiki wa Simba walilizoea kwa miaka mingi. Tofauti pekee ni safari hii hakuwa amevaa jezi ya mazoezi wala hakutarajia kuingia uwanjani tena.
Saa chache zilizopita alikuwa ametangaza rasmi kustaafu soka la kulipwa baada ya miaka 18 ya kuutumikia mchezo huo.
Lakini kabla ya kuondoka Kigali kwenda Dar es Salaam kushiriki Simba Day kwa dakika chache Mwanaspoti ilipata nafasi ya kuzungumza na fundi huyo kutokana na ugumu wa ratiba yake.
NDOTO ZILIZOANZA KAMPALA
Okwi alizaliwa Desemba 25, 1992, jijini Kampala, Uganda. Tangu akiwa mdogo alianza kuonyesha mapenzi makubwa kwa mpira wa miguu.
Akiwa mwanafunzi wa St. Henry’s College Kitovu, soka lilikuwa sehemu muhimu ya maisha yake. Wakati wengine waliona mpira kama mchezo wa kawaida, kwake ulikuwa njia ya kutimiza ndoto.
Akiwa kijana mdogo, alikuwa akivutiwa na mshambuliaji wa Arsenal, Thierry Henry, ambaye alijulikana kwa kasi, akili ya kucheza na uwezo wa kufunga. Sifa hizo zilianza kuonekana pia kwa Okwi. Alikuwa mchezaji aliyependa kushambulia nafasi zilizo wazi, kukimbia nyuma ya mabeki na kutumia kasi yake kama silaha kubwa.
Alikuwa na uwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa kati, pia angeweza kutokea pembeni kama winga wa kushoto, nafasi ambayo aliwatesa mabeki wengi.
SC VILLA: HATUA YA KWANZA
Kabla ya jina lake kusikika Afrika Mashariki, Okwi alianza kujijenga kuanzia SC Villa, moja ya klabu kubwa na zenye historia ndefu Uganda.
Akiwa SC Villa, kipaji chake kilianza kupata nafasi ya kuonekana kwa watu wengi. Alikuwa bado kijana, lakini alionyesha tabia ambazo baadaye zilimfanya kuwa mshambuliaji anayeheshimika.
Alikuwa na kasi, uwezo wa kupokea mipira katika mazingira magumu na utulivu akiwa mbele ya lango.
Katika kipindi chake cha kwanza akiwa na SC Villa kati ya mwaka 2008 na 2009, Okwi alicheza mechi 40 na kufunga mabao 13.
Takwimu hizo zilitosha kuzifanya baadhi ya klabu kubwa kuanza kufuatilia maendeleo yake. Haikuwa tena siri Uganda ilikuwa na kipaji maalumu kilichokuwa kikikua.
SIMBA SC: JINA LA OKWI LILIPOVUMA
Mwaka 2009 ukawa ukurasa muhimu katika maisha ya Okwi. Simba SC ya Tanzania iliamua kumleta mshambuliaji huyo kijana kutoka Uganda kwa ada iliyotajwa kuwa Dola 40,000 (zaidi ya sh100 milioni).
Kwa wakati huo, usajili huo ulionekana kama hatua kubwa kwa klabu ya Simba na kwa mchezaji ambaye alikuwa bado anatafuta nafasi yake katika soka la kimataifa.
Mashabiki wa Simba walikuwa wakisubiri kuona kama kijana huyo kutoka Uganda angeweza kuhimili presha ya kuvaa jezi ya moja ya klabu kubwa zaidi Afrika Mashariki.
Okwi hakuhitaji muda mrefu kuwajibu. Ndani ya uwanja alionyesha uwezo mkubwa. Alikuwa mshambuliaji ambaye mabeki walimchukulia kwa tahadhari kila alipokuwa na mpira.
Alikuwa na tabia ya kukimbia nyuma ya safu ya ulinzi, kupokea mipira mirefu, kutumia nguvu zake na kasi yake kutengeneza nafasi.
Lakini zaidi ya yote, alikuwa na uwezo wa kufunga. Kwa mashabiki wa Simba, Okwi hakuwa tu mchezaji mwingine aliyesajiliwa; alianza kuwa sehemu ya matumaini yao.
Katika kipindi chake cha kwanza Msimbazi, alicheza mechi 38 na kufunga mabao 18.
Hapa anaeleza; "Nilipofika Simba nilikuta mashabiki wenye mapenzi makubwa sana, kila mechi walitaka ushindi, ilikuwa presha, lakini ndiyo ilinifanya nikue kama mchezaji," anasema Okwi.
MEI 6, 2012: SIKU AMBAYO OKWI ALIANDIKA HISTORIA
Katika historia ndefu ya debi ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga, kuna mechi ambazo zimebaki kwenye kumbukumbu za mashabiki kwa miaka mingi.
Moja ya hizo ni ile ya Mei 6, 2012. Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ulikuwa umejaa mashabiki waliokuja kushuhudia vita ya jadi kati ya Simba na Yanga.
Lakini kilichotokea siku hiyo hakikuwa kawaida. Simba iliichapa Yanga mabao 5-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara, ushindi ambao hadi leo unatajwa kuwa miongoni mwa matokeo makubwa zaidi katika historia ya derby hiyo.
Nyota wa siku hiyo alikuwa Okwi. Alifunga mabao mawili na kuwa mwiba mkubwa kwa safu ya ulinzi ya Yanga.
Mabao mengine ya Simba yalifungwa na Felix Sunzu, Patrick Mafisango (marehemu) na Juma Kaseja. Ilikuwa siku ambayo mashabiki wa Simba waliona thamani halisi ya mshambuliaji wao kutoka Uganda.
Okwi alikuwa na kila kitu ambacho mashabiki walikipenda; kasi, ujasiri na uwezo wa kuamua mechi. Baada ya mechi hiyo, jina lake likazidi kuwa kubwa zaidi Tanzania.
"Nilijua ukubwa wa Simba na Yanga, lakini baada ya ile mechi ndipo nilielewa kwa nini watu waliuita huu ni mchezo wa maisha. Furaha ya mashabiki baada ya ushindi ule ilikuwa ya kipekee, ile ni kati ya mechi ambazo zitaendelea kuishi kwenye maisha yangu," anasema.
MAISHA YA SOKA NJE YA TANZANIA
Baada ya mafanikio yake Simba, Okwi alianza kuvuka mipaka ya Afrika Mashariki.
Mwaka 2013 alisajiliwa na klabu ya Tunisia, Étoile Sportive du Sahel, kwa ada iliyotajwa kuwa Dola 300,000, moja ya ada kubwa za uhamisho kwa mchezaji kutoka Tanzania wakati huo.
Hata hivyo, safari hiyo ilikumbwa na changamoto za kiutawala na masuala ya malipo yaliyohusisha klabu hizo.
Baadaye alirejea Afrika Mashariki na kucheza tena SC Villa na Yanga kabla ya kurudi Simba.
YANGA UKURASA MFUPI LAKINI
Okwi ni kati ya wachezaji wachache wa kigeni ambao walipata bahati ya kucheza Simba na Yanga, alitua Jangwani 2013.
Uhamisho huo ulikuwa miongoni mwa matukio yaliyovuta hisia kubwa kwa mashabiki wa soka nchini, hasa kwa sababu Okwi tayari alikuwa ameacha alama kubwa akiwa na Simba, klabu ambayo ina ushindani mkubwa wa jadi na Yanga.
Kufika kwake Yanga kulikuwa na matarajio makubwa. Mashabiki walitarajia kuona mshambuliaji ambaye alikuwa amewatesa mabeki wengi akiwa Simba sasa akisaidia kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya timu yao.
Akiwa Yanga, Okwi alicheza msimu wa 2013/14 na akufunga mabao tisa katika mechi 18 za ligi.
Hata hivyo, kipindi chake Yanga kilikumbwa na changamoto za kimkataba na masuala ya malipo, jambo lililosababisha mvutano kati yake na klabu hiyo.
Kutokana na kutokuwepo kwa makubaliano kuhusu malipo yake, Okwi alifikia hatua ya kukataa kucheza baadhi ya mechi za mwisho za msimu wa 2013/14, kabla ya baadaye kurejea Simba mwaka 2014 baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuridhia uhamisho huo.
OKWI WA PILI SIMBA
Mwaka 2014 Okwi alirejea Simba na mwaka 2017 akarudi tena kwa mara ya tatu. Safari hii alikuwa mchezaji aliyekuwa amekomaa zaidi.
Alikuwa na uzoefu wa kucheza mazingira tofauti na alijua namna ya kukabiliana na presha, kipindi cha 2017 hadi 2019 kilikuwa miongoni mwa vipindi bora zaidi katika maisha yake.
Alicheza mechi 53 na kufunga mabao 36 akiwa Simba. Alikuwa mmoja wa wachezaji waliokuwa wakibeba matumaini ya timu katika mashindano ya ndani na kimataifa.
MAJARIBU YA ULAYA NA NCHI MBALIMBALI
Mwaka 2015 Okwi alipata nafasi ya kucheza Ulaya baada ya kusaini mkataba na SønderjyskE ya Denmark.
Ingawa hakukaa muda mrefu Ulaya, ilikuwa sehemu muhimu katika safari yake kwa sababu ilimpa uzoefu wa aina nyingine ya soka.
Baadaye alicheza katika nchi mbalimbali kama Libya akiwa na Al Ittihad, Iraq akiwa na Al-Zawra’a na Erbil SC, kabla ya kurejea Rwanda kucheza na Kiyovu Sports.
Kila nchi aliyopita ilimpa somo jipya na kuongeza sura nyingine katika maisha yake ya soka.
UGANDA CRANES
Pamoja na mafanikio ya klabu, Okwi atakumbukwa zaidi kama mmoja wa wachezaji muhimu wa Uganda Cranes.
Alianza kuitumikia timu ya taifa mwaka 2009 na kwa miaka 14 alikuwa sehemu ya kizazi kilichobeba matumaini ya Uganda.
Alicheza mechi 95 za kimataifa na kufunga mabao 28.
Katika mashindano ya CECAFA alikuwa mmoja wa wachezaji waliotawala.
Mwaka 2010 alifunga mabao manne na kuwa kushika nafasi ya pili kwenye mashindano hayo.
Mwaka 2011 alifunga mabao matano na kumaliza akiwa mfungaji bora pamoja na Meddie Kagere wa Rwanda na Olivier Karekezi.
Alivaa pia kitambaa cha unahodha wa Uganda na kuwa mfano kwa wachezaji waliokuja nyuma yake.
MWISHO WA SAFARI
Baada ya miaka 18 ya soka la kulipwa, Okwi anafunga ukurasa wa maisha yake ya kucheza mpira akiwa ameacha alama kubwa.
Safari yake haipimwi kwa mabao pekee.
Inapimwa kwa furaha aliyowapa mashabiki, changamoto alizopitia, mataifa aliyowakilisha na kizazi cha wachezaji alichoweka njia.
Kutoka mtoto wa Kampala mwenye ndoto ya kucheza soka, hadi kuwa mmoja wa majina makubwa Afrika Mashariki, Okwi ameandika hadithi yake.
Miaka 18 imepita, lakini jina la Okwi litaendelea kuishi kwenye kumbukumbu za soka la Uganda, Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
MSIKIE ANACHOSEMA
Baada ya miaka 18 ya kuvaa jezi tofauti, kusafiri nchi mbalimbali na kushuhudia pande nyingi za mchezo huo, Okwi anasema wakati umefika wa kushukuru kwa kila hatua aliyopitia.
"Kwanza kabisa namshukuru Mungu kwa kunipa uwezo, afya na nafasi ya kucheza mpira kwa muda wote huu. Soka limenipa mengi sana katika maisha yangu. Nimekutana na watu wengi, nimejifunza mambo mengi na nimepata nafasi ya kuiwakilisha nchi yangu," anasema Okwi.
Anakumbuka safari yake haikuwa rahisi kama ambavyo watu wengi waliiona nje ya uwanja. Nyuma ya mabao, ushindi na mafanikio kulikuwa na maumivu, changamoto na nyakati ambazo alilazimika kuwa imara.
"Kila kitu nilichopitia kimenijenga. Kuna wakati ulikuwa mgumu, kuna wakati ulikuwa mzuri, lakini kila hatua ilikuwa sehemu ya safari yangu. Nilijifunza kutokata tamaa na kuendelea kupambana," anasema.
Kwa Okwi, moja ya mambo makubwa anayoyaacha kwenye soka ni kumbukumbu alizojenga na watu aliokutana nao katika safari hiyo.
"Ninawashukuru makocha wote walionifundisha, wachezaji ambao nilicheza nao, viongozi wa klabu na zaidi sana mashabiki. Mashabiki ndiyo moyo wa soka. Bila wao hakuna maana ya sisi kucheza," anasema.
Anapozungumzia Tanzania, macho yake yanaonyesha heshima kubwa kwa nchi ambayo ilimpa nafasi ya kujitangaza zaidi Afrika Mashariki.
"Tanzania imekuwa sehemu kubwa sana ya maisha yangu. Simba ilinipa nafasi kubwa, ilinipa fursa ya kuonyesha uwezo wangu na mashabiki walinionyesha upendo mkubwa sana. Sitaisahau Simba na sitawasahau mashabiki wake," anasema.
Okwi pia anakumbuka ushindani wa Kariakoo kati ya Simba na Yanga, ambao ulimfanya kuelewa ukubwa wa soka la Tanzania.
Baada ya kufunga ukurasa wa kucheza, Okwi anasema bado ana mapenzi makubwa na soka na anaamini uzoefu alioupata unaweza kusaidia kizazi kijacho.
"Soka limenipa maisha. Sasa ni wakati wa kuangalia hatua nyingine. Lakini bado nitakuwa sehemu ya mchezo huu kwa namna nyingine. Nataka kusaidia vijana kujifunza na kuelewa kipaji pekee hakitoshi," anasema.
Kwa wachezaji wanaokuja nyuma yake, Okwi ana ujumbe mmoja nidhamu ndiyo msingi wa mafanikio.
"Kipaji kinaweza kukufikisha mahali, lakini tabia, kujituma na kuheshimu mchezo ndivyo vinavyokuweka hapo. Mchezaji anatakiwa kila siku ajifunze na kupambana kuwa bora zaidi," anasema.
Kutoka mtoto wa Kampala aliyekuwa na ndoto ya kucheza soka, hadi kuwa nahodha wa Uganda Cranes, shujaa wa Simba na mmoja wa washambuliaji waliotengeneza historia Afrika Mashariki.
"Ninaondoka nikiwa na amani. Nimefurahia safari yangu, nimewapa watu furaha na nimejifunza mengi. Hiyo ndiyo zawadi kubwa kwangu," anamalizia Okwi.