Simba, Mlandege ndio kama ulivyoskia
Unguja. Simba imetoka sare tasa na Mlandege FC katika mchezo wao wa mwisho wa makundi lakini wametinga nusu fainali ikiwa imekusanya pointi nne kwenye kundi lao.
Simba sasa ni rasmi itacheza na Namungo hatua hiyo Januari 10 kwenye Uwanja wa Amaan.
Wakati Simba ikitinga hatua hiyo kocha wao Pablo Franco amewalalamikia waamuzi kuwa hawapo makini na kazi yao ingawa amewapongeza wachezaji pamoja na wapinzani kuwa wameonyesha ushindani mkubwa.
Amesema kuwa mashindano hayo ya Kombe la Mapinduzi anayatumia pia katika kukiandaa kikosi chake kuelekea michuano yao ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo waanza kucheza mechi za hatua ya makundi mwezi ujao.
Kwa upande wa kocha wa Mlandenge, Abdul Aziz Bakechi Junior amesema kuwa lazima wakiri kwamba wamecheza na timu kubwa na yenye wachezaji wenye uzoefu mkubwa katika soka.
"Hata wachezaji wangu wamecheza vizuri na ndio maana tumetoka nao sare, mchezo haukuwa rahisi kwetu lazima tukubali tumekutana na timu bora," amesema