Simba imsikilize Keisha
Muktasari:
- Natanguliza maneno haya baada ya kile kilichotokea katika pambano la watani wa jadi ambalo lilimalizika kwa matokeo ya sare ya 1-1.
MWIMBAJI mwenye kipaji kikubwa nchini, Keisha aliwahi kuimba juu ya uvumilivu. Aliimba katika moja ya nyimbo zake na kuonyesha kwa nini kila binadamu ana haja ya kuwa na uvumilivu.
Baada ya mchezo wa wikiendi iliyopita kati ya Simba na Yanga ni dhahiri kuwa watu wa Simba wanapaswa kurejea na kusikiliza tena mashairi ya Keisha. Kwa kifupi, tabia ni jambo la aina ya tofauti mno. Tabia njema ni zao la uvumilivu katika kuonewa, wivu na kashfa. Tabia iliyokosa uvumilivu hufanya watu kukosa thamani wakati mwingine mtu anakuwa dhaifu kuliko mnyama.
Bali wale wenye tabia njema na ya kistaarabu, huonekana bora kuliko mnyama. Sifa zake huenea kama nuru ya jua.
Natanguliza maneno haya baada ya kile kilichotokea katika pambano la watani wa jadi ambalo lilimalizika kwa matokeo ya sare ya 1-1.
Ni dhahiri, shahiri mwamuzi wa pambano hilo Martin Saanya alishindwa kwenda na kasi ya mchezo tangu mpira unaanza hadi mwisho, kinachotia ukakasi ni jinsi ambavyo hata waamuzi wasaidizi walishindwa kumsaidia, hivyo kusababisha hali ya sintofahamu miongoni mwa mashabiki.
Makosa ya mwamuzi yalikuwa ni kushindwa kumudu mchezo hasa katika matukio ya rafu zilizofanyika mwanzoni mwa mchezo, akidhani kutoa kadi kungeathiri mchezo, jambo ambalo lilimfanya ashindwe kumudu mchezo kwa jumla.
Achilia mbali utata wa bao la Ibrahim Ajibu ambalo mwamuzi wa pembeni alilikataa kwa madai alikuwa ameotea. Nirudi kwa goli la Amissi Tambwe ambalo ndilo lilizua mzozo miongoni mwa wapenzi wa soka nchini.
Ukirudia kutazama bao hilo la Tambwe ni dhahiri alishika kabla hajafunga. Katika kona aliyokuwa mwamuzi wa pembeni na namna Tambwe alivyogeuka ingekuwa ngumu kwake kuona kilichotokea, kwa maana nyingine mshika kibendera alifanya makosa ya kibinadamu.
Ila lawama zinafaa kupelekwa kwa mwamuzi wa kati kushindwa kuwa eneo sahihi kwa wakati sahihi, alipaswa kukimbia na kasi ya ule mpira tokea ukipigwa, ila hakufanya hivyo. Mwamuzi huyu alifanya kosa la kiufundi, hakuwa katika afya na utimamu wa mechi kubwa namna ile.
Hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB), wanapaswa pia kujibu kuhusu hili, historia ya mwamuzi haikuruhusu kupewa mechi kubwa ya Simba na Yanga, kwani alikuwa ndio kwanza anatoka katika adhabu ya kufungiwa, halafu akatwishwa mzigo wa mechi kubwa ya ligi.
Mashabiki baada ya bao la Tambwe walifanya vitendo visivyo vya kiungwana, kistaarabu na kivumilivu. Makosa ya waamuzi wa soka yapo duniani kote tena kwa Tanzania siyo habari mpya tena.
Goli la mfano huo liliwahi kufungwa na Diego Maradona katika robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1986 dhidi ya England, bao lililopewa jina la ‘Goli la Mkono wa Mungu’ na mashabiki wakajawa na hasira ila hawakuleta fujo.
Lionel Messi 2007 naye aliwahi kufunga bao la mkono dhidi Getafe ila mashabiki walionyesha uungwana na tabia za kistaarabu.
Hata katika Kombe la Dunia pale Afrika Kusini, Frank Lampard alifunga bao dhidi ya Ujerumani ila waamuzi wakalikataa, mashabiki wakawa na hasira ila hawakuvunja viti au kuleta fujo. Kwa hiyo makosa kwa waamuzi ni jambo la kawaida katika soka.
Tabia katika hali yoyote ama umaskini au utajiri, katika ujinga au elimu, tabia ilikuwa jambo la aina ya kipekee kabisa, tabia ilibaki kama mwongozo sawia katika maisha. Naelewa hisia za mapenzi ya soka wakati mwingine hizi timu za Simba na Yanga zimekuwa kama dini ya mashabiki. Ila katika hali yoyote lazima tuwe na tabia za kuvumilika.
Refa akishapuliza filimbi yake ni sheria na hakuna namna anayoweza kubadilisha maamuzi hata kama yeye mwenyewe akigundua amefanya makosa, hivyo ni vyema tukajifunza somo la uvumilivu na kuheshimu maamuzi ya refa na adhabu ya waamuzi wanaoboronga tuwaachie mamlaka zilizowateuwa.
Vitendo hivi vya utovu wa nidhamu havitoi picha nzuri kwa soka letu, bali vinatia hasara klabu husika na kuweza kusababisha upotevu wa amani. Tunasahau hasira ni hasara. Hapana shaka mashabiki walichukizwa na maamuzi, walijawa na hasira na uchungu wa matusi, lakini walipaswa kuwa wavumilivu.
Jambo jingine katika mpambano huo ni kitendo cha nahodha wa Simba Jonas Mkude naye kutojua majukumu yake kama kiongozi wa wachezaji uwanjani na kujikuta akizidisha moto wa hasira kwa mashabiki.
Yamkini Mkude asingeonyesha utovu wa nidhamu, naamini matokeo yasingekuwa kama yalivyokuwa. Naye anahitaji kubeba kipande cha lawama kwa yaliyotokea ikiwemo, sare ya mechi.
Mwisho, nilipongeze Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kulinda usalama hasa wakati wa mechi. Ila pamoja na kwamba sina taaluma ya mafunzo ya kipolisi, njia iliyotumika kuwatuliza mashabiki ingeweza kuleta madhara makubwa kuliko madhara ya viti. Hivyo wakati mwingine kuwe na mbinu bora za ulinzi ambazo ni rafiki hasa kuketi karibu na mashabiki na hata kama nguvu ya ziada ikihitajika kutumika katika fujo basi mazingira yazingatiwe.
Mwandishi Noel Shao ni Mchambuzi wa Masuala ya Kijamii, Kisiasa na Michezo anapatika kwa simu namba 0769735826